Ikiwa mtu ni mwamini wa kweli utakuta hapo mwanzoni alipomwamini Kristo, hakuona kuwa kuvaa vimini ni dhambi, lakini kwa kuwa Roho wa Mungu yupo ndani yake, anamfundisha na kumpa kanuni juu ya kanuni kila siku ili kumfanya kuwa mkamilifu, utaona baadaye anaona si sawa kuwa na zile nguo hivyo anachoma vile vimini, alivyokuwa anavaa kadhalika hapo mwanzo alikuwa anaona ni sawa tu kwa mwanamke wa kikristo kuvaa suruali lakini kwa kuwa Roho wa Mungu yupo ndani yake, Neno la Mungu likimjia kumwambia atupe hizo suruali, kwamba haimpasi mwanamke kuvaa mavazi yampasayao mwanamume, hatashangaa kwasababu atajua kuwa maagizo hayo yanalandana na utakatifu ambao ndio Mungu anautaka. Lakini utakuwa mtu mwingine ambaye yeye yupo chini ya kanuni za kidhehebu au za kidini, sasa kwa kuwa dini yake haisemi kuwa mwanamke kuvaa vimini na suruali pamoja na wanja na hereni ni machukizo mbele za Mungu, siku ambapo atasikia kwa mara ya kwanza Neno hilo utamwona anaanza kupinga pasipo hata kutafakari, atadai kwamba maadamu sizini mimi sina hatia, lakini hajui kuwa anaambiwa hivyo kwa faida yake mwenyewe ili aukamilishe utakatifu wake wa kutokuzini, kwasababu biblia inasema amtazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha zini naye, sasa ni kweli yeye anaweza akawa hajatamani wala hajazini, lakini yupo mwingine kazini juu yake, kwasababu ya mavazi yake ya uchi uchi, Na Bwana Yesu alishasema mtu yeyote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake kisha akatupwe baharini. Je! hapo mtu kama huyo atakuwa na la kujitetea siku ile ya Hukumu?.