Huyu “Yeye ashindaye”  Ni mtu mmoja maalumu au wengi?

by Admin | 20 October 2024 08:46 pm10

SWALI: Huyu “Yeye ashindaye”  anayezungumziwa katika kila mwisho wa jumbe za makanisa saba. Ni mtu mmoja maalumu au wengi?


JIBU: Tunasoma Bwana Yesu alipotoa agizo au onyo kwa yale kanisa  saba mwishoni alimalizia na kutoa thawabu. Lakini thawabu hiyo aliielekeza kwa yule ashindaye tu.

Kwa mfano ukisoma juu ya lile kanisa la Thiathira alisema..

Ufunuo wa Yohana 2:26

[26]Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa, 

Sasa swali huulizwa je? kuna mtu mmoja maalumu ambaye anaonekana atashinda? na kupokea tuzo hiyo ya kuwa na mamlaka juu ya mataifa au ni mjumuiko wa watu.

Ni raisi kudhani tuzo hiyo imeelekezwa kwa mtu fulani mmoja lakini ukweli ni kwamba inamuhusu kila mtu…ni sawa na mwalimu awaambie wanafunzi wake atakayefaulu mtihani wangu..nitamlipia ada ya muhula mmoja. 

Sasa yeye kutumia lugha ya umoja “atakaye” na sio “watakao”…hamaanishi kuwa amemlenga mtu fulani mmoja.

maana yake ni kuwa yeyote yule atakayefaulu, basi atalipiwa ada, iwe ni mmoja, au wawili au wote. watalipiwa. Kwasababu wamefaulu. Kigezo ni kufaulu sio atakayefaulu kuliko wote.

Vivyo hivyo na Bwana alichokimaanisha hapo kwenye hayo makanisa saba. Lengo lake ni wote washinde lakini inaonekana ni kama si wote watakaoshinda…bali wale watakaoshinda watazipokea hizo thawabu.

Hivyo ni kujitahidi…kwasababu kuna uwezekano wa wengi kukosa thawabu hizo.

 Mtume Paulo alitumia mfano wa wachezaji ambao hushiriki katika mchezo, kwamba wachezao ni wengi lakini apokeaye tuzo ni mmoja..(1Wakor 9:24)

Lakini hakumaanishi kwetu sisi atakuwa mmoja, ni mfano tu alitumia kueleza uhalisia kwamba kuna kunga’ng’ana ,sio jambo rahisi rahisi…fahamu kuwa sisi wakristo hatuna mashindano ya ukubwa na nafasi mbinguni…tunashindana ili tuyatende yale tuliyoagizwa na Bwana kikamilifu na sio kuzidiana…

Ndio maana mahali pengine akasema watatoka wengi, kutoka mashariki, na magharibi kuja kuketi na Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote, (Luka 13:28-29) Umeona kumbe wazee wetu hao, ni kama vile wamewekwa sehemu moja na wengine watakuja kuungana nao. Na wote watakua kitu kimoja na wao, lakini pia angalizo ni kwamba watakaofikia hapo si wengi sana.

Mathayo 8:11

[11]Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; 

Kwahiyo ni kujitahidi hapo tusikose..Kwa kumaanisha kweli kweli kujitwika misalaba yetu na kumfuata Yesu. Na kujitenga na dhambi, na hakika thawabu hizo tutazifikia wote.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 1)

TEMBEA NDANI YA SUKOTHI YAKO.-Maafundisho maalumu kwa watumishi

JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 4)

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/10/20/huyu-yeye-ashindaye-ni-mtu-mmoja-maalumu-au-wengi/