by Admin | 14 December 2024 08:46 am12
Maandiko yanaonyesha kuwa kitu pekee cha asili kinachoweza kutenganisha watu wawili walio katika Ndoa ni KIFO.
Warumi 7:2 “Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, amefunguliwa ile sheria ya mume.
3 Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine.”
Lakini inapotokea Mtu anachukua nafasi ya KIFO, yaani anaivunja ndoa yake mwenyewe au ya Mtu mwingine iliyo ya Halali, basi mtu huyo kibiblia ni MFU, au jina lake lingine ni KIFO/MAUTI..Sasa utauliza KIFO kinaweza kuwa MTU jibu ni Ndio!.
Ufunuo 6:8 “Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda JINA LAKE NI MAUTI, na Kuzimu akafuatana naye…”
Kwahiyo Mtu anayechukua nafasi ya KIFO, katika ndoa yake mwenyewe au ya mwingine, huyo jina lake ni MAUTI kibiblia, awe mwanamke au mwanaume, huyo ni MAUTI, ni Mfu anayetembea.
Utauliza ni wapi tena katika maandiko, panaonyesha mtu aliyeharibu ndoa ya mwingine aliitwa MFU?
Mwanzo 20:2 “Ibrahimu akamnena Sara mkewe, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akapeleka watu akamtwaa Sara.
3 Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, UMEKUWA MFU WEWE kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu”.
Umeona hapo?.. MUNGU anamwambia Abimeleki kuwa yeye ni MFU kwa kitendo tu cha kumchukua mke wa Ibrahimu.
Hebu jiulize hapo kwanini Mungu hajamwambia Mfalme Abimeliki kuwa umekuwa Najisi, au umekuwa Mjinga, au umekuwa Mpumbavu.. badala yake anamwambia amekuwa MFU!!!.. Maana yake pale alipo alikuwa ni Marehemu anayeishi.. Siku yoyote anashuka kaburini, na kila atakachojihusisha nacho kitakufa pia.
Hiyo pia ni hali ya Mtu anayeharibu ndoa yake mwenyewe au ya mwingine, kiroho jina lake ni MFU/MAUTI.
Na kumbuka maandiko yanasema Mauti anafuatana na Kuzimu.. Ufunuo 6:8 “Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda JINA LAKE NI MAUTI, na Kuzimu akafuatana naye…”
Maana yake huyu mtu anayeitwa MAUTI, anakwenda sambamba na kuzimu, na mwisho ni ZIWA LA MOTO.
Ufunuo 20:14 “Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto”.
Je Mke au Mume uliye naye ni wako? Au wa mtu mwingine?… Unajua ni maumivu gani unayasababisha kwa mwingine unapomchukua Mke wake au Mume wake??..
Labda ulimchukua pasipo kujua maandiko au enzi bado hujaokoka, lakini sasa umejua …Mrudishe huyo mwanamke/mwanamume kwa aliyewake wake hata kama una watoto naye, (weka naye tu mipango ya namna ya kuwatunza watoto), lakini usiendelee kuishi naye kwani unafanya UZINZI, mrudishe kwa mume wake/mke wake, akikataa Mwache aishi mwenyewe, wewe utakuwa umejifungua katika kifungo cha Mauti….Vunja agano na Mauti kwa namna hiyo…
Isaya 28:18 “Na agano lenu mliloagana na mauti litabatilika, tena mapatano yenu mliyopatana na kuzimu hayatasimama; pigo lifurikalo litakapopita, ndipo ninyi mtakapokanyagwa nalo”.
Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.
KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 1: Upande wa wanaume)
KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 2: Upande wa wanawake)
NDOA NA IHESHIMIWE NA WATU WOTE.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/12/14/usifanyike-kifo-katikati-ya-ndoa-ya-mwingine/
Copyright ©2025 unless otherwise noted.