Karibu tujifunze biblia.
(Masomo maalumu kwa wanandoa).
Waebrania 13:4 “Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu”.
Hapa biblia inataja vitu viwili; 1) NDOA NA IHESHIMIWE NA WATU WOTE, na 2) MALAZI YAWE SAFI.
Tutazame moja baada ya lingine.
1.NDOA NA IHESHIMIWE NA WATU WOTE.
Hapa anasema “Na iheshimiwe na watu wote”..maana yake si mtu mmoja tu au wawili au watatu, bali wote. Sasa swali ni makundi gani ya watu wanaopaswa kuiheshimu ndoa, na ndoa inaheshimiwaje.
Kundi la kwanza la watu wanaopaswa kuiheshimu ndoa, ni wanandoa wenyewe!..(Na kumbuka ndoa ni ile ya mume mmoja na mke mmoja). Na kundi la pili ni watu wa nje, wasiohusiana na hiyo ndoa.
Kwa wanandoa wanapaswa kuiheshimu ndoa yao kwa kuzuia kitu chochote ambacho kinaweza kuifanya ndoa hiyo iwe ndaifu au ivunjike. Na vitu vinavyoweza kufanya ndoa iwe ndaifu au kuvunjika kabisa ni pamoja na kukosa maelewano, Ugomvi, mafarakano, kukosa utii na upendo,uvumilivu, na uaminifu..haya ni baadhi ya mambo yanayodhoofisha ndoa na hata kuivunja kabisa.
Hivyo wanandoa ni lazima wafanye wawezavyo kutunza upendo wao wa kwanza walipokutana, Amani yao kwanza, furaha yao kwanza, maelewano yao kwanza, na mengineyo mazuri waliyokuwa nayo kipindi wanakutana. Kwa kufanya hivyo watakuwa wameiheshimu ndoa yao na itadumu daima.
Na kwa namna gani wanandoa wanaweza kurudisha upendo wao wa kwanza?…si kwanjia nyingine bali ile ya kutubu na kunyenyekea, na kujazwa Roho Mtakatifu, kwamaana yeye pekee (Roho wa Mungu) ndiye mwenye kutoa matunda yanayohitajika katika ndoa..
Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.
Kundi la pili la watu linalopasa kuheshimu Ndoa, ni watu wa nje wasio wanandoa. Ikiwa na maana kuwa mtu yeyote wa nje iwe ndugu, au rafiki, au jamaa, au jirani, au mpita njia, hapaswi kuwa sababu ya ndoa ya mwingine kudhoofika au kuvunjika.
Maana yake kama huhusiki na ndoa hiyo, basi hupaswi kupanda mbegu za fitina katika hiyo ndoa, hupaswi kufanya wanandoa wachukiane, watengane, waumizane, au wafanye lolote litakalowatolea heshima wanandoa hao. Unachopaswa kufanya ni kuwaombea na kuwashauri ikiwa wamefungua mlango huo!, na ushauri unaopaswa kuwapa ni ule wa kibiblia na si wa kidunia.
Vile vile wewe kama mtu usiyehusika na ile ndoa, hupaswi kumtamani mke/mume wa jirani yako, wala kujaribu kumshawishi uwe naye!..ni lazima uiheshimu ndoa yake, vile vile hupaswi kuanzisha mahusiano yoyote yenye viashiria vya kukushuku, au kuleta tashwishi kuhusu uhusiano wako na yeyote katika ndoa, ni lazima ukae mbali kwa kadiri uwezavyo, isipokuwa kwa sababu maalumu ambazo zitaweza kueleweka katika pande zote mbili. (Kwa kufanya hivyo utakuwa umeiheshimu ndoa ya mwingine).
2.MALAZI YAWE SAFI.
Hili ni jambo la Pili: Malazi yawe masafi.
Malazi yanayozungumziwa hapa ni mahali wanandoa wanapokutana kimwili, maana yake mahali hapo panapaswa pawe pasafi daima, pasiwe pachafu!. Na uchafu unaozungumziwa hapo si usafi ule wa vumbi katika kitanda, au jasho la mwili, (huo unafaa lakini sio unaozungumziwa hapo).
Uchafu unaozungumziwa hapo ambao ni najisi ni uchafu wa Zinaa, pamoja na kukutana kimwili kinyume na maumbile kwa wanandoa.
Unapokuwa mwanandoa ni amri kutokutana kimwili na mwanamke/mwingine tofauti na uliyefunga naye ndoa!, unapolala na mtu mwingine hapo umefanya malazi kuwa machafu, na ni dhambi kubwa!. Vile vile katika kukutana ni lazima iwe kwa namna ya asili. Na si kinyume na maumbile!. Biblia inasema wafiraji hawataurithi uzima wa milele.
1Wakorintho 6:9 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, WALA WAFIRAJI, WALA WALAWITI”
Soma pia 1Timotheo 1:10.
Iheshimu ndoa yako, vile vile heshimu ndoa za wengine.
Je umeokoka?..Fahamu kuwa Kristo anarudi!, na tupo nyakati za hatari.
Maran atha.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group
Mafundisho mengine:
MAFUNDISHO YA NDOA.
MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.
Pale mwanandoa mmoja anaposhindwa kutimiza wajibu wake ufanyaje?
FAMILIA TAKATIFU: Marimu na Yusufu.
KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 2: Upande wa wanawake)
Rudi nyumbani
Print this post