Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Warumi.

by Admin | 20 December 2024 08:46 am12

Kitabu hichi kama kinavyojitambulisha, “Waraka wa Paulo kwa Warumi” mwandishi wake ni Mtume Paulo.

Kitabu hiki alikiandika akiwa Korintho mahali palipoitwa Kenkrea (Warumi 16:1)

Tofauti na nyaraka nyingine ambazo Paulo aliziandika kwa makanisa ambayo alikuwa tayari ameshayatembelea/ameyapanda hapo nyuma. Waraka huu tunaonyeshwa Paulo hakuwahi kufika Rumi. Lakini alisikia mwitikio wao wa injili, hivyo likawa ni tamanio lake pia awafikie na wao, lengo likiwa sio kupanda juu ya msingi wa watu wengine bali wajengane kiimani.(1-18),

Na kweli tamanio lake tunaona lilikuja kutimia baadaye, kama tunavyosoma kwenye kitabu cha matendo ya mitume, katika ile ziara yake ya mwisho kama mfungwa, alifika Rumi, na huko akafanikiwa kuhubiri injili sawasawa na tamanio lake (Matendo 27-28).

Hichi ni kitabu kinachoeleza misingi ya imani  ki-mpangilio . Kuanzia asili ya wokovu wetu, haki ya Mungu, na mwenendo wa kikristo. Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana kwa mkristo yoyote kukielewa vema kitabu hichi.

Migawanya mikuu ya kitabu hichi.

     1) Nguvu ya injili? (1: 1-17)

Baada ya Paulo, kueleza tamanio lake la kuwafikia katika utangulizi wake, tunaona katika mistari hiyo anasisitiza kwanini afanye hivyo? Ni kwasababu ya ‘Nguvu ya Injili yenyewe’, Akisema Injili ni uweza wa Mungu uuletao wokovu. Na hivyo haionei haya kuihubiri kwa watu wote..kwa wayahudi na watu wa mataifa pia.

  1. Hatia kwa wanadamu wote (1:18- 3:20)

Sehemu ya pili Paulo anaeleza jinsi wanadamu wote walivyopungikiwa na utukufu wa Mungu kuanzia watu wa mataifa ambao wameshindwa kuitii kweli ya Mungu iliyofunuliwa kwao kwa mambo yake yaliyo dhahiri kabisa yanayotambulika hata pasipo sheria, kwamba mambo ya asili yanafundisha haki ya Mungu, lakini walikataa kutii. Vilevile na wayahudi  pia ambao walikuwa na sheria lakini walishindwa kuyatenda yote kulingana na yaliyoandikwa. Hivyo hakuna hata mmoja mwenye haki,  wote wamewekwa chini ya hukumu ya ghadhabu ya Mungu, kwa kushindwa kutenda haki yote.

  1. Haki kwa Imani (3:21-5:21)

Kwa kuwa wanadamu wameshindwa kuwa wakamilifu, Paulo anaeleza njia ambayo Mungu ameitoa kwa  mwanadamu kuweza  kuhesabiwa haki. Ni njia ambayo inadhihirishwa bila matendo ya sheria, tunayoipata kwa kumwamini tu Yesu Kristo. Yaani pale mtu anapomwamini Bwana Yesu kwamba kifo chake kimeleta ukombozi wa roho yake, basi mtu huyo anakuwa amehesabiwa haki kuwa ni Mtakatifu mbele za Mungu.

Kulithibitisha hilo Paulo akaendelea kueleza  kwa mfano wa Ibrahimu jinsi Mungu alivyomhesabia haki bila sheria yoyote, na kwamba sisi pia tutahesabiwa kwa njia hiyo hiyo.

  1. Maisha mapya ndani ya Kristo (6:1-8:39)

Katika sehemu hii Paulo anaeleza maisha baada ya kuhesabiwa haki, kwamba mkristo anapaswa aendelee kutakaswa na kuwa kama Kristo. Lakini kutokana na mashindano kati ya mwili na roho. Ili aweze kuushinda mwili anapaswa ajifunze kuishi kwa Roho, kwa kuruhusu utendaji kazi wake ndani yake. Maneno hayo ameyarudia pia katika waraka wake kwa Wagalatia (Wagatia 5:16). Kwamba mtu anayeenenda kwa Roho kamwe hawezi kuzitimiza tamaa za mwili.

Lakini mbele kidogo anaendelea kuhimiza upendo wa milele wa Mungu, uliodhihirishwa kwetu kupitia Yesu Kristo, ambao hauwezi kutenganishwa na kitu chochote tukijuacho duniani au mbinguni.

  1. Uhuru wa Mungu wa kuchagua, na kusudi lake kwa Waisraeli (9:1- 11:36)

Kwenye sura hizi, Paulo anaeleza uhuru wa Mungu wa kuchagua, na siri iliyokuwa nyuma ya Israeli kukataa injili. Anaeleza mpango wake wa wokovu kwa mataifa na waisraeli, kwamba iliwapasa wao wakatae injili ili sisi watu wa mataifa tuipokee injili. Na hivyo anaeleza sisi pia tunapaswa tuupokee wokovu kwa unyenyekevu wote kwasababu tusipokaa katika kuamini tutakatwa, kama wao walivyokatwa.

  1. Tabia ya maisha mapya katika Kristo (Warumi 12:1- 15:3 )

Paulo anaeleza jinsi tunavyopaswa kuitoa miili yetu kama dhabihu iliyo hai takatifu yenye kumpendeza Mungu, tunawajibu wa kupendana sisi kwa sisi, tusiwe watu wa kulipa kisasi, tuishi kwa heshima, tuhudumiane katika karama mbalimbali tulizokirimiwa na Mungu, tutii mamlaka zilizowekwa, vinywa vyetu vitoe baraka, tumtumikie Mungu kwa bidii, tudumu katika sala, tuishi kwa amani sisi kwa sisi, pia tuweze kuchukiliana katika viwango mbalimbali vya imani bila kuhukumiana.

Kwa ufupi sura hizi zinaeleza tabia zetu zinapaswa ziweje baada ya wokovu.

  1. Hitimisho  (15:14- 19:27)

Paulo anaeleza mpango wake wa kuwafikia Warumi pindi atakapokuwa anasafiri kwenda Spania kuhubiri injili. Akiomba akumbukwe katika maombi dhidi ya watu wabaya, na mwisho anatoa salamu kwa watakatifu wote walio Rumi, pamoja na angalizo kwa watu waletao fitna katika injili waliyoipokea wajiepushe nao

KWA UFUPI.

Kitabu hichi kinaeleza

Haki ya Mungu ikoje, ambapo hapo mwanzo ilidhaniwa inapatikana kwa sheria au matendo ya mwanadamu, kumbe sio, hayo yalishindwa bali kwa njia ya Yesu Kristo, lakini pia kinaeleza namna ambavyo tunaupokea wokovu huo kwa neema kwa njia ya Imani, na pia jinsi Mkristo anavyopaswa aishi kulingana na wokovu alioupokea. Kwamba sio kwasababu amehesabiwa haki bure bila matendo, basi aishi maisha kama atakayo, hapana vinginevyo atakufa.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

NJIA/BARABARA YA WOKOVU NDANI YA KITABU CHA WARUMI.

Fahamu Mwandishi wa kitabu cha Waebrania ni nani.

Uchambuzi na Mwandishi wa kitabu cha Wagalatia

Je Kauli ya Mungu katika Warumi 11:4 na 1Wafalme 19:18 inajichanganya?.

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/12/20/uchambuzi-wa-kitabu-cha-warumi/