KANUNI YA KUFUNGUA MILANGO YA BARAKA.

by Admin | 29 January 2025 08:46 am01

Fahamu kanuni muhimu ya kufungua milango ya Baraka za rohoni na mwilini.

Neno la MUNGU linasema..

Waefeso 1:3 “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ALIYETUBARIKI KWA BARAKA ZOTE ZA ROHONI, KATIKA ULIMWENGU WA ROHO, NDANI YAKE KRISTO”.

Ni lini tulibarikiwa na baraka zote za rohoni?..Je ni jana au leo??.. Nataka nikuambie kuwa si jana, wala juzi wala mwaka uliopita wala si siku ile ulipozaliwa…. bali ni tangu siku ile damu ya Mwokozi YESU ilipomwagika msalabani tayari tulishabarikiwa,

Na si kubarikiwa tu, bali pia tayari tulishaponywa tangu siku ile Kristo aliposulibiwa, tayari tulishashinda tangu siku ile Kristo aliposulibiwa..

Sasa swali ni hili, kama tayari Baraka na ushindi tulishapewa tangu siku ile ya pale Kalvari, kwanini sasa hatuzioni hizo Baraka zetu katika roho na katika mwili?

Hili ndilo swali la msingi kujiuliza.. kwanini hatuzioni hizo Baraka tulizobarikiwa miaka mingi iliyopita.

Sababu kuu ya sisi kutoshiriki Baraka zote za rohoni ambazo tayari zilishaachiliwa juu yetu, miaka elfu mbili (2) iliyopita pale Kalvari ni “shetani”.

Anachokifanya adui ni kuzuia kupokea zile Baraka, na si kuzuia zisitoke!.. Tayari Mungu alishatubariki..wala hatuwezi kumwomba tena atubariki, ni sisi kupambania kilicho chetu.

Sasa ili tuweze kupokea kilicho chetu, ni lazima tupambane vita, na vita hivyo ni vile vya kiroho, kwani shetani na majeshi yake yamesimama kuhakikisha hatupokei kilicho chetu.. shetani hamzii MUNGU kutoa, bali anatuzuia sisi kupokea… Na MUNGU tayari alishatoa, ila shetani anazuia tusipokee..

Ni sawa na mzazi aliyemtumia mwanae aliyeko shuleni fedha za matumizi kupitia anwani ya shule, halafu mwalimu mmoja azifiche zile fedha zisimfikie mtoto, hapo mtoto mwenye busara akishajua katumiwa fedha ana wajibu wa kuzifuatilia, na kuulizia na kama kuna shida kwa mwalimu, na kama akiona kuna shida basi aweza kushitaki ili tatizo litatuke, kwasababu atajua shida si mzazi bali ni mwalimu (sasa huu ni mfano tu).

Na mambo ya rohoni ni hivyo hivyo, BWANA MUNGU wetu alishatubariki kwa Baraka zote za rohoni.. kazi tuliyobakiwa nayo ni kushughulika na vizuizi vya sisi kupokea hizo Baraka.

Na silaha zifuatazo ndizo zinazoweza kuvunja vizuizi vyote na kuachia kilicho chetu.

   1. MAOMBI

Maombi (hususani yanayohusisha mfungo) ni silaha ya kwanza ya kuzipinga hila za adui zinazozuia Baraka zetu.. Mtu aliyejizoeza kuomba ni rahisi kupokea Baraka zote zilizoahidiwa na MUNGU, na mtu anayepungukiwa maombi ni kinyume chake.

   2. KUSOMA NENO.

Maombi bila Neno la Mungu ni sawa na bendera iliyokosa mlingoti… Mtu aombaye huku Neno la Mungu limejaa ndani yake, ni rahisi sana kuteka Baraka zake tofauti na yule asiyekuwa msomaji wa NENO, na kusoma Neno kunakozungumziwa hapa si kushika vifungu vya biblia, La!.. Unaweza kuwa umeshika vifungu elfu vya biblia na bado usiwe umelijua Neno.

Bali kusoma Neno kunakozungumziwa hapa ni  kule kujifunza kitabu baada ya kitabu na kujua maudhui ya kila kitabu katika ufunuo wa Roho.

    3. UTAKATIFU

Utakatifu wa mwilini na rohoni ni mkuki wa kumpiga yule mwovu aachie vinavyotuhusu.. kinyume chake uchafu na maisha ya dhambi ni kifungo kinachozuia Baraka zetu.

Sasa utauliza Baraka za rohoni na mwilini ni zipi?

Mfano wa Baraka za rohoni ni Amani, furaha, upendo, uvumilivu, upole, utu wema na mambo mengine yote mema yanayofanana na hayo, kwa ufupi ni Roho Mtakatifu na matunda yake (Wagalatia 5:22).

Na baraka za mwilini hamna haja ya kuziandika maana zinajulikana, ambazo ni zile zote zinazohusu mahitaji ya mwilini.

Je umepungukiwa na Baraka?…fahamu kuwa Maombi, Neno na Utakatifu ndio dawa ya kutibu hilo tatizo, wala usimnung’unikie MUNGU kwanini hakubariki.. yeye tayari alishatubariki, ni sisi kupambana kupata vilivyo vyetu..Anza mapambano hayo kuanzia sasa ikiwa tayari umeshampokea Bwana YESU.

Na kumbuka mapambano haya hamna siku yatapoa, hata baada ya kuwa mtumishi.. ni jambo endelevu daima mpaka safari ya maisha inaisha, kwani pia kuna kupokonywa na yule aliyetuzuia tusipokee, ikiwa hatutasimama katika mambo hayo makuu matatu, na mengine yanayofanana na hayo.

Hivyo ukristo ni mapambano, ni vita, lakini vyenye nafasi kubwa ya kushinda Zaidi ya kushindwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Warumi 8:37 “Lakini katika mambo hayo yote TUNASHINDA, NA ZAIDI YA KUSHINDA, kwa yeye aliyetupenda”.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

KAMA MWIZI USIKU WA MANANE.

MILANGO YA KUZIMU.

NITAONGEZAJE NGUVU ZANGU ZA ROHONI?

CHAKULA CHA ROHONI.

MILANGO YA KUZIMU.

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/01/29/kanuni-ya-kufungua-milango-ya-baraka/