by Admin | 31 January 2025 08:46 am01
SWALI: Kwanini sehemu kadha wa kadha wana wa Israeli walipoonekana wanakwenda kinyume na Torati hutumia kauli ya
“atakatiliwa mbali na watu wake”. Nini maana ya hii kauli?
Mambo ya Walawi 7:27
[27]Mtu ye yote alaye damu, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.
JIBU: Ni kauli ya ujumla inayomaanisha huyo mtu atatengwa na kusanyiko la Israeli. Kutengwa huko kunaweza kuwa Kwa namna mbalimbali kutegemeana na aina ya kosa.
Hizi ndio aina kuu tatu za kukatiliwa mbali
Kifo kilihusika katika baadhi ya hukumu, ambazo Nyingine ni Mungu mwenyewe aliyezitekeleza (Walawi 20:3-6). Na nyingine Wanadamu. Kwamfano mtu yeyote aliyefumaniwa katika uzinzi, adhabu yake ilikuwa ni kupigwa Mawe Mpaka kufa.
Vivyo hivyo katika kuihalifu sabato, adhabu ilikuwa ni hiyo soma;
Kutoka 31:14
[14]Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.
Hii nayo ilikuwa ni aina nyingine ya kukatiliwa mbali, ambapo ulifutwa katika hesabu ya waisraeli, inayokufanya kupoteza haki ya kushiriki Ibada yoyote katika makusanyiko, au vipaumbele.
Hesabu 19:20
[20]Lakini mtu atakayekuwa najisi, naye hataki kujitakasa, mtu huyo atakatiliwa mbali katika mkutano, kwa sababu amepatia unajisi mahali patakatifu pa BWANA; hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake; yeye yu najisi.
Maana yake ni kuwa hauwi mshirika tena wa baraka za maagano ya Mungu, kama vile ulinzi na ahadi.
Mwanzo 17:14
[14]Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu.
Hata leo, katika agano jipya mambo mambo tunaweza kufanya yakatusababishia kukatiliwa mbali na rehema za Mungu.
Na adhabu hizo zinaweza kutekelezwa na wanadamu(watakatifu), na nyingine Mungu mwenyewe.
Kwamfano Biblia inatoa ruhusu kanisa kumtenga mtu ambaye anazoelea dhambi, (1Wakorintho 5:1-5)
Mungu mwenyewe anaweza kutekeleza hukumu hiyo, kwamfano tunaweza kuona kwa Anania na Safira, ambao walitumia njia ya hila katika mapatano ya Roho.(Matendo 5:1-11). Lakini pia kwa mtu ambaye anakusudia kuurudia ulimwengu baada ya kuipokea neema, hukumu kama hii huweza kumkuta. (Waebrania 10:26-27)
Kwahiyo jambo hili halikuwa tu kwa wana wa Israeli, lakini lipo hata sasa rohoni. Tusiwe watu wa kuzoelea dhambi tukidhani kuwa wakati wote Mungu ataturehemu. Usidanganyike ukishakatiliwa mbali si rahisi tena kumgeukia Mungu wako.
Shalom.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Tofauti kati ya makuhani na walawi ni ipi?
Maana ya Mithali 25:25 Kama vile maji ya baridi kwa mtu mwenye kiu
ALIPOKUWA ANGALI MBALI, BABA YAKE ALIMWONA.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/01/31/nini-maana-ya-kauli-atakatiliwa-mbali-na-watu-wake-walawi-727/
Copyright ©2025 unless otherwise noted.