Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo Bwana Yesu. Karibu katika kujifunza maneno ya uzima ya mwokozi wetu.
Leo tutaona jinsi “moyo wa toba ya kweli” unavyopokelewa kitofauti sana na Mungu. Kama tunavyoifahamu ile habari ya mwana mpotevu, jinsi alivyoingiwa na tamaa, ya kwenda kuanzisha maisha yake ya anasa mbali na baba yake. Na siku zilipozidi kwenda, mali zilipoisha, njaa kali ikamkuta Akaanza kula vyakula vya majalalani ambavyo viliwastahili tu nguruwe. Lakini Biblia inasema, hakung’ang’ania tu kuendelea kutaabika katika hali ile ile milele mpaka kufa kwake. Bali alijinyenyekeza akazingatia kurudi kwa baba yake akiwa na moyo wa toba, ili baba yake amfanye tu mtumwa. Na alipofanya vile, akiwa njiani anarudi, biblia inatumbia kuna tukio lilitokea.
Na tukio lenyewe ni “kuonekana kwake tokea mbali” . Tusome;
Luka 15:17 “Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. 18 Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; 19 sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. 20 Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. 21 Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. 22 Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; 23 mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; 24 kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia”
Embu tafakari, iweje, Baba yake ndio awe wa kwanza kumwona tokea mbali na sio watumwa ambao sikuzote wao ndio wanaosimama mlangoni mwa nyumba au kuzunguka zunguka huku na huko, au kwanini isiwe hata ndugu zake wengine, badala yake baba yake ndio anayekuwa wa kwanza kumwona?
Sio kana kwamba hao wengine walikuwa hawali mboga za majani, hawaoni mbali mambo yao kuwa hafifu, hapana, bali Baba yake alikuwa na jicho lingine la rohoni kama DARUBINI. Hilo lilikuwa linaona mahangaiko, na manyanyaso ya mwanaye tokea mbali, kiasi kwamba alipofanya geuko moyoni mwake, tayari baba yake alishahisi, na akiwa njiani anakuja tayari baba yake alishajua kuwa mwanawe yupo njiani. Hivyo kabla hata mtoto hajamwona Baba, kabla hata hajaifikia nyumba yao akiwa kilomita kadhaa mbali, tayari baba alikwenda kukutana naye na kukumbatia na kumbusu sana.
Ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu. Pale mtu anapokuwa na moyo wa toba ya kweli rohoni, haihitaji wewe kwenda kusema maneno mengi sana mbele za Mungu, kana kwamba ndio utasikiwa. Yeye anayo darubini yake, Lakini kule kuzingatia tu kurudi kwa Baba yako wa mbinguni, ukaanza kuchukua hatua. Hiyo ni toba kubwa sana ambayo itamfanya Mungu, kabla ya wewe kumfikia tayari ameshakufikia, haraka sana na kukupa tiba ya moyo wako, na raha nafsini mwako.
Hii ni kuonyesha kuwa toba ya kweli, ni ule moyo uliogeuka. Sio tu kuongozwa sala maalumu. Ndio tunajua sala ikiambatana na geuko ni vema sana, lakini ikiwa utasalishwa sala hizo elfu 10 halafu ndani yako, ni vilevile tu, hapo unapoteza muda wako ndugu.
Alikuwepo Yule mwanamke mwenye dhambi nyingi sana, alipokwenda kwa Bwana Yesu saa ile ile akaanza kulia akitubia dhambi zake, akidondosha machozi yake miguu pa Yesu, huku akiyapangusa kwa nywele zake. Lakini Yesu alipomwona akasema ‘Umesamehewa dhambi zako nyingi’, mwanamke Yule hakusalishwa sala yoyote.(Luka 7:36-50).
Ili Mungu afike kwako upesi, kuwa na toba ya kweli, ili upate kibali cha haraka kwa Mungu, sio wingi wa maombi yako, bali geuko la dhati. Na Bwana mwenyewe atakufikia kabla hujamfikia yeye.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
WALA HAKUACHA MTU ACHUKUE CHOMBO KATI YA HEKALU.
Kwanini Nuhu alimlaani Kaanani badala ya mtoto wake Hamu,
UMUHIMU WA KUISHI MAISHA YAMPENDEZAYO MUNGU SASA.
MUME / MKE BORA KUTOKA KWA BWANA UTAMWONA UKIWA KATIKA MAZINGIRA GANI?
JE! UKRISTO UNAMPA MTU DHAMANA YA KUWA TAJIRI?
Forodhani ni mahali gani?
Rudi nyumbani
Print this post
Neno la MUNGU huja kwa wakati kwangu nina ona niwakati wa kuzingatia na kuifuata haki.
Ubarikiwe sana,nimejifunza kitu hapo
Amina uzidi kubarikiwa…