MUME / MKE BORA KUTOKA KWA BWANA UTAMWONA UKIWA KATIKA MAZINGIRA GANI?

MUME / MKE BORA KUTOKA KWA BWANA UTAMWONA UKIWA KATIKA MAZINGIRA GANI?

Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze Neno la Mungu ili tupate maarifa sahihi ya kuishi hapa duniani.

Na leo tutaona mazingira ambayo ukikaa katika hayo basi Mungu atakujalia umwone mke/mume sahihi aliyekuchagulia toka mbali.

Tofauti na mazingira ya kiulimwengu ambayo yenyewe ili yakupe mke/mume wa kidunia ni sharti uwe katika mazingira ya kidunia..yaani uvae vimini, ujitembeze na suruali barabarani, unyoe viduku, uishi kama wasanii wa kidunia, uwepo disco na kwenye party party kila wakati n.k. ili uonekane.

Ukikaa katika mazingira kama hayo hakika dunia itakupatia unachokitafuta..

Lakini leo tutajifunza mazingira ya ki-Mungu… Ili Mungu akuonyeshe mke/mume sahihi tokea mbali je! Ukae katika mazingira gani.?

Tutamtazama Isaka mtoto wa Ibrahimu. Kama wewe ni msomaji wa biblia utakumbuka mpaka wakati mama yake anakufa hakuwa na mke bado.

Lakini siku moja Baba yake alipoona ni wakati sasa wa Isaka kuwa na mke alimtuma Kijakazi wake mmoja kwenda kumtafutia mke kutoka katika nchi ya mbali nchi sana ya baba zake. ..kwani hakutaka kumpatia mke kutoka katika miji ile waliyokuwepo.

Kuonyesha kuwa haijalishi utazungukwa na vijana wengi wazuri mahali ulipo, hiyo bado haikufanyi udhani mke/mume Mungu aliyekuchagulia ni lazima atoke hapo.

Sasa utaona mara baada ya yule kijakazi kutumwa kwenda kumtafutia Isaka mke na kumpata alipokuwa anarudi..Huku nyuma kuna tabia na desturi ambayo Isaka alikuwa nayo ambayo nataka leo tuione kwasababu hapa ndipo kiini cha somo letu kilipo.. Tusome..

Mwanzo 24:62-66

[62]Basi Isaka alikuwa amekuja kwa njia ya Beer-lahai-roi, maana alikaa katika nchi ya kusini.
[63]Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja.
[64]Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia.
[65]Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika.
[66]Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda.

Rudia tena Mstari wa 62 unasema…

‘Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni’.

Unaona, Pindi tu alipotoa mguu wake na kwenda kondeni kutafakari..alipojijengea desturi ya kwenda maporini mbali na makazi ya watu ili tu kupata utulivu na Mungu wake, kuutafakari ukuu wake na uweza wake na maajabu yake na ahadi zake..huko huko Mke wake alitokea..na akamwona tokea mbali..

Pengine yeye alidhani mjini alikoondoka ndipo wake wanapotokea lakini..alishangaa kule kule kondeni kwa mbali sana ngamia wanakuja wamembeba bibi arusi wake..

Hiyo ni kuonyesha Isaka haukuwa na hulka kama za vijana wengine walizokuwa nazo..alipendelea zaidi kumtafakari Mungu kuliko kuzurura zurura huko na huko.

Matokeo yake akampata Rebeka, mwanamke ambaye tunamsoma mpaka leo, licha ya kuwa alikuwa ni mwanamke anayemcha Mungu lakini bado alikuwa ni mzuri sana wa uso..Mwanzo 26:6-7

Ndugu, ikiwa unamuhitaji mke mzuri na anaye mcha Mungu basi kuwa kama Isaka..lakini ikiwa unamuhitaji Yezebeli basi ishi mfano wa hao vijana wa kidunia wanavyoishi leo hii..

Na hili pia lipo kwa upande wa pili wa mabinti..ikiwa unataka uolewe na mwanamume ilimradi tu mwanamume basi jiweke kama hao mabinti wa kidunia wanavyojiweka wanaotembea nusu uchi barabarani na kujipambapamba kama vile Yezebeli ili waonekane wanavutia..
Utampata unayemtafuta.

Lakini kinyume chake ni kuwa ukitulia katika kusudi la Mungu..unatumia muda mrefu kwa Mungu wako kuliko kutanga tanga..unamtakafakari tu yeye..nakwambia Mungu utakuongoza kwa Isaka wako tokea mbali..kama vile Rebeka alivyomwona Isaka akimfuta kutokea mbali..

Uhitaji kujionyesha onyesha ovyo..kwasababu anayekuletea mke/mume ni Mungu, si mwanadamu..wewe kaa katika kumtakafakari yeye maisha yako yote.

Kuoa utaoa, kuolewa utaolewa tu!..ukiishi maisha yanayopendeza Mungu si uongo utakutendea tu.

Daudi alisema..

Zaburi 37:25
[25]Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee,
Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa
Wala mzao wake akiomba chakula.

Mungu hawezi kuacha kumpa mteule wake kitu kilicho chema, na kizuri.. Hawezi kuruhusu mke/mume pasua kichwa atokee mbele ya njia yake, mtu anayemcha yeye. Hilo haliwezekani..

Hivyo kama bado hujaokoka. Tubu leo anza maisha yako upya na Bwana Yesu kwa kumaanisha kabisa..Toba ya kweli inaambatana na kuucha ulimwenguni, mkatae shetani na kazi zake zote na vimini vyake vyote, na suruali zote na viduku vyote..kamtafakari Mungu huko makondeni, hata kama utaonekana mshamba..

Ishi maisha ya kumlingana Bwana..Na bila shaka wakati utafika atamtuma malaika wake kwenda kukuletea mwenzi sahihi..Kama Ibrahimu alivyomtuma kijakazi wake, kumletea Isaka Rebeka.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 1: Upande wa wanaume)

Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji zilikuwaje?

Je! “Mke wa ujana wako” ni yupi kibiblia?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
5 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Grace Sami
Grace Sami
1 year ago

Nabarikiwa sana , naomba mmniadd kwenye group yenu wa Whatsapp
Kupitia namba 0756046255

florahmrema52@gmail.com
florahmrema52@gmail.com
1 year ago

Nimefurahia mafundisho yenu yananibadilisha

E.S.M
E.S.M
2 years ago

nimefurahishwa na tovuti yenu sana na Mungu awabariki