TAFUTA HEKIMA, MAARIFA, UFAHAMU NA BUSARA.

TAFUTA HEKIMA, MAARIFA, UFAHAMU NA BUSARA.

Jina la Mwokozi Mkuu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia.

Mithali 2:10 “Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;

 11 Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi. 

Haya ni mambo manne ambayo ni muhimu sana kuwa ndani yetu.

  1. Hekima – Ni uwezo wa kupanga na kupambanua mambo
  2. Maarifa- Ni elimu au taarifa kuhusiana na jambo fulani
  3. Ufahamu- Ni hali  ya kuweza kufahamu jambo Fulani kwa kina
  4. Busara- Ni hali ya kuona mbele (yaani mambo yajayo) na kuamua lililo sahihi. Mithali 27:12

Mambo haya manne ni Bwana pekee anayeweza kuyatoa.. Mithali 2:6 “Kwa kuwa Bwana huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu” .

Zifuatazo ni faida kuu tatu (3) za kupata Hekima, Maarifa, ufahamu na busara.

  1. KUOKOKA NA NJIA YA UOVU.

Hii ni faida ya kwanza ya kupata Hekima, Ufahamu, busara na Maarifa; “Kumwokoa mtu na njia ya uovu”

Mithali 2:10 “Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;

11 Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi. 

12 ILI KUKUOKOA NA NJIA YA UOVU, Na watu wanenao yaliyopotoka; 

13 Watu waziachao njia za unyofu, Ili kuziendea njia za giza; 

14 Wafurahio kutenda mabaya; Wapendezwao na upotoe wa waovu; 

15 Waliopotoka katika njia zao; Walio wakaidi katika mapito yao”

Njia ya Uovu ni njia yoyote ile ambayo itampelekea mtu kufanya maovu, mfano wa hayo ni yale yanayotajwa katika Wagalatia 5:19-21 “uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo”.

2. KUKUOKOA NA MALAYA:

Mithali 2:16 “…Ili kuokoka na malaya, Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake..”

Mtu aliye Malaya ni yule anayefanya uasherati aidha kwa lengo la kutafuta pesa au kujifurahisha, na hili ni neno linalotumika kuwakilisha jinsia zote mbili za watu wenye tabia hizo. Na Malaya anaweza kuwa ni mtu aliye ndani ya ndoa au nje ya ndoa.

Mtu mwenye busara (Maana yake anayeona mbele), hawezi kunaswa na mtego wa Malaya.. Mfano wa mtu aliyekuwa na busara katika biblia ambaye aliokoka na mtego wa Malaya ni Yusufu, ambaye alitegewa mtego na mke wa Potifa, lakini aliushinda mtego ule wa ibilisi.

Lakini kama Yusufu hangekuwa na Busara akilini mwake, basi angenaswa katika mtego ule wa  uasherati alipobembelezwa na mke wa Potifa, na hivyo angekuwa amejiingiza katika matatizo makubwa sana, ambayo yangehatarisha hata maisha yake ya kimwili na kiroho.. kama biblia inavyosema hapa..

Mithali 2:16 “Ili kuokoka na malaya, Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake;

17 Amwachaye rafiki wa ujana wake, Na kulisahau agano la Mungu wake. 

18 Maana nyumba yake inaelekea mauti, Na mapito yake yanakwenda kwenye wafu. 

19 Katika hao wamwendeao harudi hata mmoja, Wala hawazifikilii njia za uzima”

Soma tena maandiko mengine yanayohusu tabia za Malaya, jinsi anavyobembeleza katika Mithali 7:7-23, Mithali 22:14 na Mithali 23:27.

Ukiona mtu kanaswa na mtego basi ni matokeo ya kupungukiwa Hekima, busara, maarifa na ufahamu.. kama biblia inavyosema katika Mithali 6:32 “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake” .Kwasababu mtu aliyejaa mambo hayo hawezi kunaswa na mitego hiyo.

3. KUKUPELEKA KATIKA NJIA YA WATU WEMA

Faida ya kwanza tuliona ni “kumwokoa mtu katika njia ya uovu” lakini Hii ya tatu na ya mwisho, ambayo ni “Kukupeleka mtu katika njia ya watu wema”.. Hekima, busara, Maarifa na ufahamu haviishii tu kumwokoa mtu na njia mbaya na kumwacha hapo katikati bali pia kumpeleka/kumwongoza katika njia nzuri.

Mithali 2:20 “Ili upate kwenda katika njia ya watu wema, Na kuyashika mapito ya wenye haki.

21 Maana wanyofu watakaa katika nchi, Na wakamilifu watadumu ndani yake. 

22 Bali waovu watatengwa na nchi, Nao wafanyao hila watang’olewa”.

Watu wema wana Njia yao, wapo katika mkondo wao, si kila mahali wanapita, na hao ndio wanaodumu katika nchi, … Sasa ili kuiona hiyo njia waliyopo basi Hekima, Busara, Maarifa na ufahamu vinahitajika. Na vyote hivyo vinatoka kwa Mungu.

Sasa swali? Mtu anapataje Hekima, Ufahamu, Busara na Maarifa ili kuepukana na hayo yote, na kupata faida hizo.

Tukitaka Hekima, Maarifa, Ufahamu na Busara biblia imetupa kanuni rahisi katika kitabu cha Ayubu.

Ayubu 28:20 “Basi hekima yatoka wapi? Na mahali pa ufahamu ni wapi? 

21 Kwa kuwa imefichwa mbali na macho ya wote walio hai, Na kusitirika na ndege wa angani. 

22 Uharibifu na Mauti husema, Tumesikia habari zake kwa masikio yetu. 

23 Mungu ndiye aijuaye njia yake, Naye anajua mahali pake. 

24 Maana anatazama hata miisho ya nchi, Na kuona chini ya mbingu nzima. 

25 Apate kuufanyia upepo uzito wake; Naam, anayapima maji kwa kipimo. 

26 Hapo alipoiwekea mvua amri, Na njia kwa umeme wa radi. 

27 Ndipo alipoiona na kuitangaza; Aliithibitisha, naam, na kuichunguza. 

28 Kisha akamwambia mwanadamu, Tazama, KUMCHA BWANA NDIYO HEKIMA, NA KUJITENGA NA UOVU NDIO UFAHAMU”.

Kumcha Bwana na kuepukana na Uovu ndio chanzo cha Hekima, maarifa, busara na ufahamu.

Maana yake Jishughulishe sana na masuala ya kiMungu sana, Jifunze Neno la Mungu, kusanyika na wengine katika maombi, ibada na kufanya uinjilisti na mambo mengine yote yanayofanana na hayo, kwa kufanya hivyo ndivyo Hekima, na hayo mambo mengine yatakayoingia ndani yako na kujaa.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?

Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.

Mjombakaka ni nani kwenye maandiko? (Walawi 11:29)

Nini maana ya “Mwenye hekima huvuta roho za watu”

Mwandishi wa kitabu cha Zaburi ni nani?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Michael Paul
Michael Paul
1 year ago

Kweli kabisa,ili tuepukane na uovu wa kila namna ni kumtegemea Mungu