by Admin | 3 February 2025 08:46 am02
Huu ni waraka wa Pili ambao mtume Paulo aliuandika kwa mwanae Timotheo akiwa kama mfungwa kule Rumi (2Timotheo 1:17)
Ni waraka wa Kitume zaidi, akimweleza Timotheo mambo mengi anayopaswa ayafanya, na ayaelewe kuhusiana na kazi ya Mungu.
Maudhui makuu ya Paulo yalikuwa ni haya;.
Haya ni maelezo mafupi katika maeneo hayo makuu:
> Paulo Anaanza kwa kumtaka Timotheo aichochee karama iliyo ndani yake, aliyoipokea kwa kuwekewa mikono na yeye. Akionyesha kuwa huduma ni kama moto ambao ili kuufanya uendelee kuwaka inahitaji wakati wote uchochewe.(2Timotheo 1:6-8)
> Anamsihi kama askari mwema, ajikite katika kazi moja ya injili, Asipeleke fikra zake katika shughuli za kidunia, akimtaka afahamu hilo ili aweze kuvipiga vita vizuri vya imani, bila kuvutwa na mambo mengi.
2 Timotheo 2:3-7
[3]Ushiriki taabu pamoja nami, kama askari mwema wa Kristo Yesu.
[4]Hakuna apigaye vita ajitiaye katika shughuli za dunia, ili ampendeze yeye aliyemwandika awe askari.
[5]Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali.
[6]Yampasa mkulima mwenye taabu ya kazi kuwa wa kwanza wa kupata fungu la matunda.
[7]Yafahamu sana hayo nisemayo, kwa maana Bwana atakupa akili katika mambo yote.
> Anamtaka pia ajionyeshe Kuwa amekubaliwa na Mungu, Mtu awezaye kuligawanya Neno la Mungu vema, (2:15)
> Azikimbie tamaa za ujanani (2:22)
> Awe tayari kuhubiri injili Wakati wote ufaao na usiofaa.(4:1-2)
> Awe na kiasi katika mambo yote, avumilie mabaya, atimize huduma yake. (4:5)
> Akumbuke pia akikubali kuishi maisha ya utauwa ataudhiwa.(3:12)
Paulo anatoa habari za tabia alizokutana nazo kwa baadhi wa wahudumu wenza,
makundi hayo ni kama yafuatayo;
> Walioshirika na yeye nyakati zote kwa uaminifu, mfano wa hawa ni Onesiforo na watu wa nyumbani mwake, pamoja na Luka(1:16).
> Waliotengana naye kwasababu njema za mtawanyiko wa kihuduma mfano wa hawa ni Kreste na Tito,(4:9b)
> Lakini wapo ambao walimwacha kwa kupenda dunia mfano wa hawa ni Dema.(4:9)
> Na wengine kwa kujiingiza kwenye mafundisho ya uongo mfano wa hawa ni Himenayo na Fileto.(2:17-18)
> Na wengine walifanyika kabisa wapinzani wake. Mfano wa hawa ni Iskanda mfua shaba.(4:14)
Lengo la Paulo kumjuza juu ya watu hawa ni kumtaka ajifunze kuvumilia, na pia kujiepusha nao hususani wale wapingamizi, na kuweka misingi ya kimafundisho kwa kuwatahadharisha watu wasiyafuatishe mafundisho mengine, kwani makundi hayo atakutana nayo, na yatakuwepo.
Paulo anampasha habari Timotheo uhalisia juu ya nyakati za mwisho, ambazo tangu wakati ule zilikuwa tayari zimeshaanza..
2 Timotheo 3:1-5
[1]Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.
[2]Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,
[3]wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,
[4]wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;
[5]wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.
makusudi yake ni kumtaka avumilie, na kusimama imara katika huduma, kwasababu nyakati ngumu atakutana nazo za watu wengi kujiepusha na mafundisho ya uzima.
Anasema pia kutazuka wimbi la waalimu wa uongo, wapinzani wa injili mfano wa Yane na Yambre, ambao watashindana na kweli, (3:8-9).
Hatua za kuchua:
> Adumu katika mafundisho na mwenendo wote alioupokea kwake (3:10, 14)
> Awakabidhi wengine mapokeo hayo. .(2:1)
> Ajiepushe na mashindano ya kidini, na maneno yasiyokuwa na maana (2:16, 23-26)
Mwisho.
Paulo anaeleza mwisho wake, na sababu ya kuvipiga vita vema na kusimama imara katika Imani, ni kwasababu aliiona ile taji ya haki aliyowekewa Na Mungu mbinguni. Akitumai na Timotheo atasukumwa kuvipiga vita vema kwa kuiona thawabu hiyo hiyo aliyowekewa mbinguni.
2 Timotheo 4:6-8
[6]Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika.
[7]Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda;
[8]baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.
Shalom.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Uchambuzi wa kitabu cha kwanza cha Paulo kwa Timotheo (1Timotheo)
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/02/03/uchambuzi-wa-kitabu-cha-2timotheo/
Copyright ©2025 unless otherwise noted.