JINSI MATENDO YA IMANI YANAVYOWEZA KULETA UTAMBULISHO MPYA KWA MTU.

by Devis | 1 May 2025 08:46 am05

Jina la Bwana na Mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe daima.

Je unajua matendo ya Imani, yanaweza kuleta utambulisho mwingine kwako tofauti na ule wa kwanza, na kibali kipya.

Turejee Biblia, kisa cha Daudi kumwua Goliati, biblia inaonyesha kuwa kabla ya Daudi kumwua Goliati, alikuwa anaishi nyumbani kwa Mfalme Sauli katika jumba la kifalme, na kazi yake pale ilikuwa ni kupiga kinubi, wakati roho mbaya ilipomjia Sauli.

1Samweli 16:21 “Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa mtu wa kumchukulia silaha zake.

22 Kisha Sauli akapeleka watu kwa Yese, akasema, Tafadhali, MWACHE DAUDI ASIMAME MBELE YANGU; MAANA AMEONA KIBALI MACHONI PANGU.

23 Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha”.

Hapa tunaona tayari Mfalme Sauli amemjua Daudi na tena amemfanya kuwa mchukua silaha wake, sasa ni ngumu kumfanya mtu kuwa mchukua silaha, kama bado hujamjua wala kumkubali.

Lakini tukiendelea kusoma habari hii mbele kidogo baada ya Daudi kumwua Goliati tunaona jambo lingine la kushangaza.. kwamba Sauli anamwuliza tena Daudi yeye ni mwana wa nani, kana kwamba alikuwa hamjui hapo kwanza..

1Samweli 17:54 “Naye Daudi akakitwaa kichwa chake yule Mfilisti na kukileta Yerusalemu; lakini silaha zake akaziweka hemani mwake.

55 Basi Sauli, hapo alipomwona Daudi akitoka ili kumwendea yule Mfilisti, alimwambia Abneri, jemadari wa jeshi, Je! Abneri, kijana huyu ni mwana wa nani? Abneri akamjibu, Ee mfalme, kama iishivyo roho yako, mimi siwezi kusema.

56 Basi mfalme akasema, Uliza wewe, KIJANA HUYU NI MWANA WA NANI.

57 Hata na Daudi alipokuwa yuarudi kutoka katika kumwua yule Mfilisti, Abneri alimtwaa, akamleta mbele ya Sauli, naye anacho kichwa chake yule Mfilisti mkononi mwake

58 Basi Sauli akamwuliza, Wewe, kijana, u mwana wa nani? Naye Daudi akamjibu, Mimi ni mwana wa mtumishi wako, Yese, mtu wa Bethlehemu.”

Kama Daudi asingefanya tendo lile la imani na kishujaa, la kumwua Goliati, Mfalme asingemjua Daudi, ingawa tayari alishajitambulisha kwake na hata kuishi naye… Baada ya tukio hilo tunazidi kuona kibali cha Daudi kuongezeka kwa kiwango kingine.

1Samweli 18:1 “Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe”.

Hapo kabla Yonathani huwenda alikuwa anamwona Daudi kama mwimba ngojera tu! kwenye nyumba ya mfalme.

Kama Goliati akiendelea kusimama katika maisha yako usipomwangusha kwa imani unaweza kuendelea kubaki pale pale, lakini kama ukichukua mawe matano kama Daudi na kumwangusha chini, basi hapo umefungua kibali kipya!..  Jina lako linakuwa sio lile lile tena, nafasi yako sio ile ile tena, kujulikana kwako kunakuwa sio kule kule tena.

Goliati ni roho yoyote inayojiinua ya vitisho, na Goliati wa kwanza katika maisha yetu ni Dhambi!.. Huyu ndiye anayesumbua!, ndiye anayeficha kibali chetu, ndiye anayeficha nafasi zetu na kutuzuilia kusonga mbele, tukiweza kumwangusha huyu na jeshi lote la wafilisti (magonjwa, shida, na mambo mengine yatesayo) yanakimbia, na tunabaki washindi na wenye kibali kingine.

Je umetubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha?..kama bado ni nini unasubiri?.. kumbuka kuomba msamaha sio kutubu, bali toba halisi inakamilishwa kwa kuacha matendo yote mabaya ya giza, maana yake baada ya kuomba msamaha wa dhambi kutoka kwa MUNGU, kinachofuata ni kuacha zile njia mbaya, ikiwemo kujitenga na makundi ya watu yanayopalilia dhambi iliyokuwa inakusumbua.

Vile vile kuacha kufanya vitu, au kuangalia vitu vilivyokuwa vinakukosesha, na pia kuacha kuvaa mavazi yaliyokuwa yanakaribisha dhambi maishani mwako. Kwa kufanya hivyo utakuwa umemwangusha Goliati na kubali chako kitaongezeka kama ilivyokuwa kwa Daudi.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Kwanini MUNGU alimzuia Daudi asimjengee HEKALU? (1Nyakati 17:12)

Daudi alikuwa na wake wangapi, na je ni halali kuwa na wake wengi?

Waanaki ni watu gani katika biblia?

JE! UNAWEZA KUWA NA GEUKO KAMA LA DAUDI?

Je! aliyemwua Goliathi ni Daudi au Elhanani.

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/05/01/jinsi-matendo-ya-imani-yanavyoweza-kuleta-utambulisho-mpya-kwa-mtu/