by Devis | 16 June 2025 08:46 am06
SWALI: Nini maana ya Yeremia 31:30 “Bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake mwenyewe; kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi”.
JIBU: Zamani za agano la kale katika taifa la Israeli, kulikuwa na usemi maarufu, unaosema “Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi”.
Kikawaida zabibu au matunda mengine yenye asidi nyingi mtu alapo , huwa meno yanatia ganzi, lakini kamwe haiwezekani mtu mwingine akatiwa ganzi kwa ulaji wa mwingine.
Hapa Waisraeli wakiwa wanamaanisha kuwa adhabu za Mungu huwa zinatembea hata kwa kizazi cha watu, Lakini Mungu kwa kinywa cha Yeremia anawasahihisha kuwa hilo si jambo lake..Anawaambia kila mtu ataadhibiwa sawasawa na uovu wake, wala watoto hawatauchukua uovu wa wazazi wao..Jambo ambalo alilirudia pia kwa kinywa cha Nabii Ezekieli (Ezekieli 18:20).
Lakini pia ukisoma muktadha wa vifungu hivyo, utaona anatoa unabii wa agano jipya ambalo atalifanya na watu wake kupitia Yesu Kristo, akimaanisha kuwa wokovu wake pia , utakuwa ni wa mtu binafsi, mmoja mmoja. Tusome habari yote tokea juu.
Yeremia 31: 27 Tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapoipanda nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, mbegu ya mwanadamu na mbegu ya mnyama.
28 Tena itakuwa, kwa kadiri nilivyowaangalia, ili kung’oa, na kubomoa, na kuangusha, na kuangamiza, na kutesa; kwa kadiri iyo hiyo nitawaangalia, ili kujenga, na kupanda, asema Bwana.
29 Siku zile, hawatasema tena, Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi.
30 Bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake mwenyewe; kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi.
31 Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.
32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.
33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
Hivyo vifungu hivi, vinatupa kutambua kuwa wajibu wa kulitunza agano la Mungu ni la mtu binafsi, sawasawa na alivyokuja kulifunua katika agano jipya kupitia Yesu Kristo, kwamba ijapokuwa wokovu umeachiliwa kwa wote, lakini haupokelewi kijumuiya, kifamilia, au kikabila, bali kibinafsi.
Kila mtu atalibeba furushi lake mwenyewe. (Wagalatia 6:5)
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Tafsiri ya Yeremia 29:12 Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza.
Yeremia alikuwa na umri gani alipoitwa?
Mti wa MLOZI alioonyeshwa nabii Yeremia 1:12 tafsiri yake ni nini?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/06/16/kila-mtu-alaye-zabibu-kali-meno-yake-yatatiwa-ganzi/
Copyright ©2025 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.