Ipi Tofauti ya Agano jipya na Agano la Kale?.

by Devis | 19 June 2025 08:46 am06

Ili tuelewe vizuri utofauti uliopo kati ya Agano jipya na la kale,  tutafakari mifano ya kawaida ya maisha;

Hebu tafakari juu ya Elimu ya Awali (msingi) na Elimu ya Sekondari.. Utaona ulipokuwa shule ya msingi ulijifunza mahesabu ya  kujumlisha na kuzidisha kwa kutumia vitu vya asili kama vijiti au mawe.. Lakini ulipofika sekondari ulitumia kikokotoo (yaani calculator).

Sasa mabadiliko hayo hayaifanyi elimu ya msingi kuwa batili, kwasababu tu vipo vikokotoo..La bali zinaithibitisha zaidi ile elimu ya msingi.. kwasababu kikokotoo (calculator) kinapiga mahesabu yale yale ya kujumlisha na kuzidisha kwa kasi  na ufasaha zaidi.

Ni hivyo hivyo kwa Agano la kale na Agano jipya..

Mambo yaliyopo ndani ya Agano jipya ni mambo yale yale yaliyopo ndani ya agano la kale isipokuwa katika ufunuo bora zaidi na ufasaha mkubwa zaidi..

Tafakari tena mfano huu…

Toleo la kwanza la simu yako miaka 15 iliyopita..bila shaka lilikuwa ni mfano wa  “tochi”, lenye mipaka mingi ya matumizi lakini toleo la pili la sasahivi ni “smart” ambalo unaweza kuingia internet, kupakua applications, kutazama video na hata kusikiliza nyimbo.

Kwahiyo Toleo jipya halijaja kuondoa chochote kilichopokuwepo kwenye toleo la kale, isipokuwa limeboresha zaidi vile vilivyopo na kuongeza vingine vya ziada.. maana yake Kama mtu alikuwa anasikiliza tu sauti pekee, sasa katika toleo jipya atasikika sauti pamoja na picha ya anayeongea..

Hali kadhalika kama toleo la kwanza la simu lilikuwa linachukua muda kuwaka na linahifadhi nambari za simu za watu 100 tu, basi toleo jipya litakuwa linawahi kuwaka na pia kuhifadhi namba za watu hadi 1,000.

Ni hivyo hivyo katika habari ya Agano la kale na Agano Jipya..  

Agano jipya ni toleo bora zaidi la agano la kale,  ni kitu kile kile isipokuwa kimeandikwa na kutendeka katika ubora mkubwa zaidi, na ufunuo mkubwa zaidi..

Kwamfano katika agano la kale, kafara na dhabihu zilikuwa ni za wanyama lakini tunapokuja katika Agano jipya dhabihu zimeboreshwa zaidi,  badala ya kutumika damu za wanyama, inatumika damu ya MTU, YESU KRISTO (Ambayo ni bora zaidi).

Vile vile katika Agano la kale, amri ziliandikwa kwenye mbao za mawe kule mlima Sinai, lakini katika agano jipya amri na sheria za Mungu zinaandikwa katika mioyo yetu kiufunuo zaidi.

Yeremia 31:31  “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.

32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.

33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu”.

Katika Agano la kale Uzinzi ulijulikana katika mwili tu (Kutoka 20:14) lakini katika Agano jipya uzinzi unajulikana katika mwili na roho kwa ufunuo bora zaidi (Soma Mathayo 5:28)

Katika Agano la kale uuaji ulijulikana katika mwili tu (Kutoka 20:13), lakini katika Agano jipya uuaji unajulikana katika mwili na roho kwa ufunuo bora zaidi (Soma Mathayo 5:21-22).

Katika Agano la Kale ni watu wachache tu ndio walishukiwa na Roho wa Mungu, (ambao walikuwa ni Manabii na Waamuzi) lakini katika Agano jipya watu wote wanayo fursa la kushukiwa na Roho Mtakatifu (Matendo 2:17-18).

Kwahiyo Agano  jipya ni mwendelezo wa Agano la kale katika ubora zaidi na utimilifu na ufunuo mkamilifu, ndio maana Bwana YESU alisema hakuja kuitangua torati bali kuitimiliza.

Mathayo 5:17 “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza”.

Na Roho Mtakatifu ndiye Msaidizi wetu tuliyepewa ambaye atatusaidia kulielewa Agano la Kale na Agano jipya, hivyo hatuna budi kumtafuta huyo kwa bidii zote.

Na Roho Mtakatifu ni ahadi ya Bure kwetu kwa watu wote pasipo kujali umri (Matendo 2:37-38), tukimpata Roho Mtakatifu basi tutazidi kuielewa Biblia.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Orodha ya majina ya Miji ya Biblia (Agano la kale) na Sasa

Je! habari ya Yusufu, inabeba ujumbe gani kwa agano jipya?

Neno “Mashehe” tunaliona likitajwa katika biblia(Agano la kale); Hawa mashehe ni wakina nani?

MAWE YALIYOKWISHA KUCHONGWA MACHIMBONI.

NGUVU YA UPENDO WA KRISTO.

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/06/19/ipi-tofauti-ya-agano-jipya-na-agano-la-kale/