by Devis | 14 July 2025 08:46 am07
Musa (Mgongo)
Kristo (kioo)
Mbinguni (Dhahiri)
Ilikuwa ni shauku ya Musa kutaka Kuuona uso wa Mungu baada ya muda mrefu kukaa bila kumwona Mungu..
Lakini tukirudi kwenye maandiko yanasema, Mungu alizungumza na Musa uso kwa uso kama mtu anavyozungumza na rafiki yake.
Kutoka 33:11 Naye Bwana akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani.
Lakini iweje tena, aombe kuuona uso wa Mungu, na Mungu kumwambia huwezi kuuona uso wangu ukaishi?
Kutoka 33:20 Kisha akasema, Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi.
21 Bwana akasema, Tazama, hapa pana mahali karibu nami, nawe utasimama juu ya mwamba;
22 kisha itakuwa wakati unapopita utukufu wangu, nitakutia katika ufa wa ule mwamba, na kukufunika kwa
mkono wangu hata nitakapokuwa nimekwisha kupita;
23 nami nitaondoa mkono wangu, nawe utaniona nyuma yangu, bali uso wangu hautaonekana
Ukweli ni kwamba kuuona uso wa Mungu, sio kuona mwonekano Fulani, au umbo Fulani la Mungu. Hapana, bali ni kumjua yeye ndani ni nani.. Tangu zamani Mungu alikuwa akijifunua kwa wanadamu kupitia maumbile mbalimbali, ambayo yanaweza kuchukua taswira ya vitu, wanadamu au malaika(huitwa Theofania),. Hivyo kwa namna yoyote ile Mungu anapomtokea mtu kwa namna mojawapo ya hizo na kuisikia sauti yake kama vile mwanadamu mwenzako anavyozungumza na wewe, ni sawa na kusema Mungu amesema nawe uso kwa uso. Lakini haimaanishi kuwa umeouna uso wake. Kuuona uso wake ni kumjua yeye ni nani.
Sasa Mungu akamwambia, Musa, huwezi kuniona ukaishi, Kwanini amwambie vile, Je! Mungu ni kifo? Hapana, Mungu ni uzima, lakini Musa alikuwa bado hajakamilika kwasababu ya dhambi, hivyo utukufu wa Mungu asingeweza kuustahimili, kwasababu wakati wa kuustahimili ulikuwa bado, kwani ulihitaji kwanza ondoleo la dhambi kabisa.
Hivyo Mungu akamwonyesha sehemu yake ya nyuma (Mgongo). Lakini Uso hakuuona.. Ndipo akamjua Mungu kwa sehemu yeye ni nani..
Alipomwona alishangaa sana, kwa zile tabia na sifa, Mungu alizokuwa nazo, jinsi zilivyo tofauti na mawazo ya wanadamu.. Pengine alijua ataona mafunuo makubwa ya nguvu na uweza, na mamlaka, ya ukuu, na utukufu usioelezeka kibinadamu, lakini alipomwona Mungu alimwona ni mwenye huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye hukumu za haki.
Kutoka 34:5-7
5 Bwana akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la Bwana.
6 Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si
mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli;
7 mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si
mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba
zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.
Hata sasa, mtu anayemtambua Mungu kwa namna hii, basi ameuona mgongo wa Mungu.. Na pale mtu anapoiga tabia hizo basi, amemkaribia Mungu sana.
Lakini safari ya kuuona Uso wa Mungu, ilikuwa bado haijakamilika..
Hivyo wakati ulipofika, Mungu akamtuma mwanawe duniani, (Yesu Kristo), kutuonyesha sasa uso wa Mungu ulivyo..Maandiko yanasema hivyo;
Yohana 1:18 Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.
Umeona kumbe, hakukuwahi kutokea mtu duniani aliyeuona uso wa Mungu, na moja ya kazi kubwa aliyokuja kuifanya Yesu duniani ni kumfunua Mungu(uso wake) ni nani?
Na kwasababu hakuna mtu mwenye dhambi anayeweza kumwona Mungu akaishi, ilimbidi yeye mwenyewe awe fidia ya dhambi zetu, kwa kufa kwake pale msalabani, ili sisi tuhesabiwe kuwa hatuna dhambi (kwa neema), na ndipo sasa tustahimili kuuona utukufu wa Uso wa Mungu.
Na alipotukamilisha kwa namna hiyo, basi, akatuwezesha pia kumkaribia Mungu tumwone.
Yesu akatufunulia uso wa Mungu, kuwa yeye ni UPENDO. Na upendo wake si ule wa kibinadamu, , kwamba nakupenda kwasababu umenipenda, au umenitendea jambo zuri.. Hapana, bali ni ule usio na sharti wa kuonyesha fadhili hata kwa wanautuchukia..
Musa, aliishia kujua huruma tu za Mungu juu juu (kibinadamu), lakini hakujua kuwa hata jino kwa jino, ilikuwa ni makosa, kumwonea mwenzako hasira, au hata kumfolea ilikuwa ni makosa, yanayostahili hukumu, talaka Mungu hapendezwi nazo.. Musa hakujua kuwa Mungu anataka tumwone yeye kama BABA, ambaye ni ‘ABA’ yaani Baba mwenye mahusiano ya karibu na mwanawe, kama ilivyokuwa kwa Yesu na Mungu,yeye alidhani Mungu ni wa kutoa tu amri, sheria na hukumu, Musa hakujua kuwa mwenye dhambi (mfano wa mzinzi, mwanamke mchawi) hapaswi kutupiwa mawe, bali kuhubiriwa injili ili atubu.. Yote hayo Yesu alikuja kutufunulia, kiufasaha kabisa wala hakutuficha chochote..
Kwa jinsi nyingine ni kuwa sisi tumemwona Mungu kupitia Kristo, na kwa kupitia uhalisia wa maisha yake. Tukiyaishi maneno ya Kristo, basi tumemjua Mungu uso wake, kiufasaha kabisa..
Lakini Safari bado inaendelea… Uso wa Mungu katika kilele chake, bado hatujaufikia…
Utauliza kwa namna gani?
Ni kwamba kwasasa tunaouona kwa njia ya KIOO, bado hatujauona kiuhalisia kabisa kwa macho, japo tunaweza kusema kuona kwenye kioo hakuna tofauti na kuona kabisa kwa macho, lakini ladha huwa zinatofautiana, kumwona Raisi kwenye Tv, ni Yule Yule utakayemwona kwa macho, lakini ladha ni tofauti..
Hivyo Kristo alikuwa kama chapa (kioo) ya Mungu yenyewe, duniani..Yaani sisi tayari tumemwona Mungu kupitia Kristo Yesu..
Waebrania 1:3 Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;
Ndio maana maandiko bado yanasema, kwasasa tunaona kwa kioo, lakini wakati ule tumjua sana yeye alivyo..
1Wakorintho 13:12 Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana.
Wakati wa kuona dhahiri, wema wote wa Mungu, itakuwa ni mbinguni.
Tutamjua katika eneo gani?
Katika eneo lilelile la upendo, (sawasawa na ile 1Wakorintho 13 ilivyokuwa inaeleza habari hiyo tangu juu)
Hapo ndipo tutaufurahia upendo wa Mungu katika namna ambayo hatujawahi kuijua, kwa vile vitu tulivyoandaliwa na yeye mbinguni, milele…
Hivyo, hatuna budi sasa kutembea katika upendo wa Mungu kwasababu yeye ndio huo..
1Yohana 4:16 Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.
Hitimisho:
Hatua za kuuona Uso wa Mungu, zilianza, na Musa, (kwa mgongo), zikaja kwa Kristo (kwa kioo), na mwisho mbinguni, (dhahiri).
Je! Umempokea Kristo? Ikiwa bado, fahamu kuwa huwezi kamwe kumwona Mungu, hata iweje, mpokee leo, akuoshe dhambi zako, kwasababu kumbuka pia alimwambia Musa, hatamwesabia mtu mwovu kuwa hana hatia, yaani kila mmoja atapewa anachostahili. Ukifa katika dhambi zako, hakuna upendo huko kuzimu,hutatolewa huko na kuletwa mbinguni.. kwasababu umechagua mwenyewe giza. Yesu alisema Jehanamu ya moto ipo, na mtu asipomwamini yeye, atakufa katika dhambi zake. Hivyo ndugu, Ingia ndani ya Yesu leo upokee neema, hujui ni lini utaondoka duniani, usiishi tu kama mnyama, tubu dhambi mkimbilie Yesu, akuponye.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/07/14/safari-ya-kuuona-uso-wa-mungu/
Copyright ©2025 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.