Kudhihaki ni nini kibiblia?

by Devis | 21 July 2025 08:46 pm07

Kudhihaki kibiblia ni kitendo cha kumbeza au kumkejeli mtu, shetani au Mungu, (maana yake kumfanya yule mtu aonekane hana heshima, au hana maana), dhihaka pia anaambatana na dharau, utani na hata matusi.

Katika Biblia tunaona kuna watu waliwadhihaki wanadamu wenzao, na wengine walimdhihaki ibilisi na ufalme wake, na wako waliojaribu kumdhihaki Mungu wa mbingu na nchi,..kwa ufupi tuitazame mifano hiyo.

    1. DHIHAKA KWA MWANADAMU.

     Dhihaka ya Ishmaeli kwa Sara.

Tunasoma kipindi Hajiri amempata Ishmaeli kwa Abrahamu, mtoto Ishmaeli alianza kumfanyia dhihaka mamaye mkubwa Sara, na matokeo yako ni kufukuzwa yeye pamoja na mama yake..

Mwanzo 21:9 “Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka.

10 Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka”.

Utasoma pia dhihaka za watu kwa watumishi wa Mungu katika 2Nyakati 36:16, Nehemia 4:1, Na pia sehemu nyingine utaona Mungu anawafanyia dhihaka wanadamu wanaoenda kinyume na shauri lake (Soma Zab 2:4 na Zab 59:8).

    2. DHIHAKA KWA SHETANI NA UFALME WAKE.

Kuna wakati Nabii Eliya alimdhihaki mungu-baali pamoja na makuhani wake.

1Wafalme 18:27 “Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe.

28 Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika”.

   3. DHIHAKA YA WANADAMU KWA MUNGU.

Hakuna mahali popote mwanadamu amefanikiwa kumdhihaki Mungu, kwasababu Mungu hadhihakiwi..

Wagalatia 6:7 “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.

8 Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele”.

Wapo waliojaribu kumdhihaki Mungu katika biblia lakini walikuja kujua baadaye kuwa Mungu hadhihakiwi.. Mfano wa hao, ni wale watumwa wa mfalme wa Shamu waliomdhihaki Mungu kwa kusema ana uwezo wa kuokoa tu milimani na si nchi tambarare, na matokeo yake waliziona kazi zake.

1Wafalme 20:23 “Basi watumwa wake mfalme wa Shamu wakamwambia, Mungu wao ni mungu wa milima; ndiyo sababu ya kutushinda sisi; lakini na tupigane nao katika nchi tambarare, na hakika tutawashinda wao.

24 Ufanye neno hili; uwaondoe hao wafalme, kila mtu atoke mahali pake, ukaweke majemadari mahali pao.

25 Kisha ujihesabie jeshi, kama jeshi lililokupotea, farasi kwa farasi na gari kwa gari; nasi tutapigana nao katika nchi tambarare, na bila shaka tutawashinda. Akaisikiliza sauti yao, akafanya kama hivyo.

26 Basi ikawa mwakani, Ben-hadadi akawahesabu Washami, akakwea mpaka Afeki ili apigane na Israeli.

27 Wana wa Israeli nao wakahesabiwa, wakapewa vyakula, wakaenda kupigana nao; wakatua wana wa Israeli mbele yao kama vikundi viwili vya wana-mbuzi; bali Washami wakaijaza nchi.

28 Akaja yule mtu wa Mungu, akamwambia mfalme wa Israeli, akasema, Bwana asema hivi, Kwa sababu Washami wamesema, Bwana ni Mungu wa milima wala si Mungu wa nchi tambarare; basi nitawatia makutano haya yote walio wengi mkononi mwako, nanyi mtajua ya kuwa ndimi Bwana.

29 Wakatua kuelekeana muda wa siku saba. Ikawa siku ya saba vikapangwa vita; wana wa Israeli wakawapiga miongoni mwa Washami siku moja watu mia elfu waendao kwa miguu.

30 Lakini waliosalia wakakimbia mpaka Afeki, mjini; na ukuta ukaanguka juu ya watu ishirini na saba elfu waliosalia. Ben-hadadi naye akakimbia, akaingia mjini, katika chumba cha ndani”.

Kwahiyo Mungu hadhihakiwi wala hajaribiwi wala hapimwi, wana wa Israeli jangwani walijaribu kumpima na maandiko yanasema wakayaona matendo yake..

Zaburi 95:8 “Msifanye migumu mioyo yenu; Kama vile huko Meriba Kama siku ya Masa jangwani.

9 Hapo waliponijaribu baba zenu, Wakanipima, wakayaona matendo yangu.

10 Miaka arobaini nalihuzunika na kizazi kile, Nikasema, Hao ni watu waliopotoka mioyo, Hawakuzijua njia zangu.

11 Nikaapa kwa hasira yangu Wasiingie rahani mwangu”.

Kwa hitimisho hatupaswi kudhihakiana sisi kwa sisi, wala kuwadhihaki watumishi wa Mungu, wala tusijaribu kumdhihaki MUNGU wa mbingu na nchi kwani yeye hadhihakiwi, lakini tunaweza kudhubutu kumdhihaki shetani na majeshi yake, kwa lengo la kumpa Mungu utukufu, na si kujiinua sisi, ikiwa tumesimama vyema na MUNGU, lakini  kama hatujasimama vyema na Mungu, kumdhihaki shetani ni hatari, na kuleta matokeo kama yale yaliyowateka wana wa Skewa (Soma Matendo 19:13-17).

Pia kama umeokoka Biblia imesema tutapitia vipindi vya dhihaka tu (soma) kama Bwana wetu YESU KRISTO pamoja na wanafunzi wake  alidhihakiwa sisi ni akina nani? (soma Luka 22:63, Matendo 2:13 na Waebrania 11:36) lakini yote katika yote tunafundishwa kusamehe, na kuvumilia, kwasababu siku za mwisho ilishatabiriwa kuwa watakuja watu wa kudhihaki wengi (Soma 2Petro 3:3 na Yuda 1:18)

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

HASIRA YA MUNGU KUKUWAKIA, KWA KUTOMZUNGUZIA TU MUNGU IPASAVYO.

Maana ya Mithali 29:9 Mwenye hekima akijadiliana na mpumbavu; Akikasirika au akicheka, pia hapana raha. 

NI NANI ALIYEWAONYA KUIKIMBIA HASIRA ITAKAYOKUJA?

Je Daudi aliwachukia viwete na vipofu? (2Samweli 5:6-9)

NAO WALIOKUWA WAMEKUSUDIWA UZIMA WA MILELE WAKAAMINI.

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/07/21/kudhihaki-ni-nini-kibiblia/