HASIRA YA MUNGU KUKUWAKIA, KWA KUTOMZUNGUZIA TU MUNGU IPASAVYO.

HASIRA YA MUNGU KUKUWAKIA, KWA KUTOMZUNGUZIA TU MUNGU IPASAVYO.

Shalom, karibu tena tujifunze maneno ya uzima ya Mungu wetu YEHOVA.

Kuna wakati Mungu anaweza kukaa kimya na kuruhusu mambo Fulani yatokee, ili aone watu wake watamzungumziaje kuhusu jambo hilo, Na hapo ndipo tunapopaswa tuwe makini, kwasababu mtu akikosa kujua makusudi ya Mungu ni nini, halafu akamzungumzia tu kutokana na mawazo yake au uonavyo yeye, anaweza kujisababishia hasira yake iwake juu yako.

Kuna jambo moja la namna hiyo ambalo lipo hasaa kwetu sisi watu wa kanisa la Laodikia, ambalo tunamzunguzia Mungu isivyopasa. Kosa hilo lilifanywa na watu wa kale na sisi bado tunataka kulirudia Na leo hii tutaliona katika biblia.

Kosa lenyewe lilifanywa na wale marafiki watatu Ayubu (yaani Elfazi, Sofari na Bildadi). Mawazo yao yalianzia pale, walipoona Mungu kamletea Ayubu majanga makubwa kama tunavyoyasoma katika biblia.. Walipoona ghafla mali za Ayubu zimepukutika, baadaye tena familia yake ikaondoka, na zaidi ya yote, magonjwa ya mauti yakawa yanamwandama…

Hivyo hawa marafiki zake watatu ambao walikuwa ni wenye hekima kweli kama yeye, na wakati mwingine wenye upendo, kiasi kwamba kufunga safari toka mbali kuja kumfariji Rafiki yao, na kulia naye, ni jambo la upendo mwingi..Lakini walikosa kujua kitu kimoja..Wao walidhani kigezo pekee cha mtu kukubaliwa na Mungu ni kuwa na mali, na utajiri, na mafanikio na Maisha mazuri basi…

Hivyo watu wote waliokuwa wanawaona barabarani kama matajiri, na wenye mali, walihitimisha kuwa ni marafiki wa Mungu wakubwa, Halikadhalika wale wanaopatwa na matatizo na shida, wanatumika chini ya laana kubwa ya Mungu..Hilo tu ndilo lilikuwa kikwazo kwao, lakini mengine yote hawakuwa na hatia..

Sasa ulipofika wakati wa Rafiki yao kipenzi Ayubu kukutwa na majanga kama yale, ndipo wakahitimisha kuwa Ayubu sasa kuna mahali alimkosea Mungu, tena mahali pakuwa sana, na hivyo ni lazima akiri, na atubu makosa yake, wakawa wanamshurutisha kwa nguvu, wakijaribu kushuhudia mabaya yake kwa kila namna..kwa kumwambia maneno kama haya:

Ayubu 4:7 “Kumbuka, tafadhali, ni nani aliyeangamia akiwa hana hatia? Au hao waelekevu, walikatiliwa mbali wapi?

8 Kama mimi nilivyoona, hao walimao maovu, Na kupanda madhara, huvuna yayo hayo.

9 Kwa pumzi za Mungu huangamia. Na kwa kuvuma kwa hasira zake humalizika”.

Ayubu 8:3 “Je! Mungu hupotosha hukumu? Au, huyo Mwenyezi hupotosha yaliyo ya haki?

4 Kwamba watoto wako wamemfanyia dhambi, Naye amewatia mkononi mwa kosa lao;

5 Wewe ukimtafuta Mungu kwa bidii, Na kumsihi huyo Mwenyezi;

6 Ukiwa wewe u safi na mwelekevu; Hakika yeye sasa angeamka kwa ajili yako, Na kuyafanya makazi ya haki yako kufanikiwa.

7 Tena ujapokuwa huo mwanzo wako ulikuwa ni mdogo, Lakini mwisho wako ungeongezeka sana.

Ayubu 15:34 “Kwa kuwa jamii ya hao wasiomcha Mungu watakuwa tasa, Na moto utateketeza mahema yenye rushwa”.

N.k n.k, hatuwezi kuorodhesha mistari yote hapa, lakini soma kitabu cha Ayubu kuanzia sura ya 4-25, utaona, msimamo wao hao watu jinsi ulivyokuwa mkali na ule ule, Kwamba Ayubu kupatwa na misiba ile ni matokeo ya uovu wake aliomtendea Mungu, Pamoja na familia yake..

Lakini kwasababu Ayubu alikuwa anamjua Mungu vizuri, hakuhitimisha kuwa kupitia shida, au mtu kuwa maskini au kupungukiwa ni kwamba Mungu amekukataa, badala yake alianza kuwaeleza siri ambayo walikuwa hawaijui akawaambia, wapo watu ambao wamemkataa Mungu, ambao hawaamini hata uweza wa Mungu, lakini Mungu huyo huyo anawapa, afya, amebariki kazi za mikono yao, amewafanikisha kwa kila kitu watakacho, na zaidi ya yote wamepewa Maisha marefu, lakini mwisho wa siku watakufa na watashuka kuzimu kwa ghafla…Hivyo kigezo cha kufanikiwa sio kigezo kuwa Mungu amekukubali..

Ayubu 21:7 “Mbona waovu wanaishi, Na kuwa wazee, naam, na kuongezeka kuwa na nguvu?

8 Kizazi chao kinathibitika nao machoni pao, Na wazao wao mbele ya macho yao.

9 Nyumba zao zi salama pasina hofu, Wala fimbo ya Mungu haiwapigi.

10 Fahali wao huvyaza wala hapungukiwi na nguvu; Ng’ombe wao mke huzaa, asiharibu mimba.

11 Huwatoa kama kundi watoto wao. Na watoto wao hucheza.

12 Huimba kwa matari na kwa kinubi, Na kuifurahia sauti ya filimbi.

13 Siku zao hutumia katika kufanikiwa, Kisha hushuka kuzimuni ghafula.

14 Walakini walimwambia Mungu. Tuondokee; Kwani hatutaki kuzijua njia zako.

15 Huyo Mwenyezi ni nani, hata tumtumikie? Nasi tutafaidiwa nini tukimwomba?

16 Tazama, kufanikiwa kwao hakumo mkononi mwao; Mashauri ya waovu na yawe mbali nami.

17 Je! Ni mara ngapi taa yao waovu huzimishwa? Na msiba wao kuwajilia? Na Mungu kuwagawanyia uchungu kwa hasira yake?

18 Ili wawe kama mabua makavu mbele ya upepo, Kama makapi yaliyochukuliwa na dhoruba”?

Unaona? Hata baada ya kuelezwa maneno hayo, hilo halikuwafanya marafiki wa Ayubu wabadilishe mitazamo yao, msimamao wao bado ulikuwa ni ule ule, kwamba Ayubu kakosea mahali!, ndio maana yale yote yamempata…Mungu kamwe hawezi kuruhusu mabaya kama yale yamkute mja wake..hilo haliwezekani,

Lakini mwisho kabisa mwa kitabu cha Ayubu tunaona Mungu anasimama na kuanza kuzungumza sasa, akamwambia Ayubu maneno yafuatayo..

Ayubu 42:7 “Basi ikawa, baada ya Bwana kumwambia Ayubu maneno hayo, Bwana akamwambia huyo Elifazi Mtemani, HASIRA ZANGU ZINAWAKA JUU YAKO, na juu ya hao rafiki zako wawili; kwa kuwa ninyi HAMKUNENA YALIYO SAWA KATIKA HABARI ZANGU, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.

8 Basi sasa, jitwalieni ng’ombe waume saba, na kondoo waume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa nitamridhia yeye, nisiwatende sawasawa na upumbavu wenu; kwani ninyi HAMKUNENA MANENO YALIYONYOKA KATIKA HABARI ZANGU, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu”

Ni lipi tunafundishwa?

Kwa bahati mbaya, hata sasa mawazo kama haya mabovu yapo vichwani mwa baadhi yetu (Hususani wahubiri wa leo). Tunamwazia Mungu katika utajiri tu na mafanikio? Na mahubiri yetu kila siku ni hayo, na tunatumia mistari baadhi baadhi ya kusimami, kama walivyofanya wakina Bildadi, Sofari na Elfazi.

Ndugu unayosoma ujumbe huu, ikiwa na wewe unamnenea Mungu maneno kama hayo, ikiwa na wewe unamuhubiri Mungu kwa njia hiyo tu, ikiwa biblia unayoisoma unaona mistari tu kufanikiwa kimwili, na unawafundisha wengine hivyo..angalia sana..Hasira ya Mungu isije ikawa juu yako.

Kumbuka: (Sio kwamba tusihubiri mafanikio, la! Kwa Mungu yapo mafanikio, makubwa sana! lakini usihubiri kwamba wote ambao hawajafanikiwa na maskini wamepungukiwa na kitu kwa Mungu wao, hapo utakuwa hujamzungumzia Mungu vizuri). Hata ufanyaje huwezi elewa njia zote za Mungu, hivyo epuka kulazimisha kila jambo, na kutaka liwe kama wewe unavyotaka liwe. Sio kila mtu mwenye ulemavu ana laana!, sio wote wenye magonjwa ya muda mrefu yasiyopona kafungwa na nguvu za giza!..sio vipofu wote unaowaona au viziwi ni laana inawafuata… Wengine Mungu karuhusu wawe hivyo kwa makusudi yake yeye (kasome Yohana 9:1-3)

Yakobo 2:4 “ Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao?”

1Wakoritho 10:11 “Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani.

12 Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke”.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Je Mungu anawapenda watu wote au ana chuki?

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

Jehanamu ni nini?

JAWABU LA MAISHA YA MTU.

KUMTEGEMEA MWOKOZI Lyrics/Swahili.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments