NAO WALIOKUWA WAMEKUSUDIWA UZIMA WA MILELE WAKAAMINI.

NAO WALIOKUWA WAMEKUSUDIWA UZIMA WA MILELE WAKAAMINI.

Shalom, karibu tujifunza Neno la Mungu..

Matendo 13:46 “Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa.

47 Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana, Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia.

48 Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.

49 Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote”.

Ni jambo la kuogopesha kusikia kuwa wapo watu waliokusidiwa uzima wa milele, na wapo ambao hawajakusudiwa uzima wa milele. Na hilo linatupa picha kuwa suala la wokovu sio jambo la kubabaisha bali ni mpango wa Mungu mkamilifu ambao ulishapangwa tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu..alishakuwa na Idadi kamili ya watakaokolewa na akawaandika katika kitabu chake cha uzima..

Ufunuo 17:8 “ Na hao wakaao juu ya nchi, wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, watastaajabu wamwonapo yule mnyama…”

soma pia Waefeso 1:4

Na ndio maana Bwana Yesu alisema..

Yohana 6:44 “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho”.

Ikimaanisha kuwa tendo la kumwamini tu Kristo na kumfuata kwa uaminifu wote sio jambo la mtu tu kujiamulia, bali ni jambo ambalo Mungu alishalipanga kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu na hivyo akamchagua mtu huyo, kisha akamwekea mwiitikio huo ndani yake na ndio maana akamwamini na kumfuata bila kigugumizi chochote..

Na ndio maana hata wakati mwingine utamwona yupo ambaye kazaliwa katika ukristo, kalelewa katika mambo ya imani maisha yake yote, amekuwa akihudhuria kanisani miaka mingi na kwenye mikutano mbali mbali lakini bado suala la wokovu lisiwe ni jambo la muhimu sana katika maisha yake..Lakini wakati huo huo, utaona tena mtu mwingine ambaye amezaliwa katika mazingira yasiyomjua Mungu, au pengine muislamu, au mbudha hajui vizuri masuala ya wokovu, lakini siku moja akasikia tu mahali Fulani Kristo anahubiriwa, na muda huo huo akachomwa moyo, akaacha kila kitu na kumfuata Yesu kwa kutokujali kuwa ndugu zake watamchukuliaje..

Sasa Hapo unajiuliza inakuwaje?..Ni kwasababu yeye alikusudiwa uzima wa milele, na huyu mwingine hakukusudiwa.

Angalia tena sehemu nyingine biblia inasema..

2Timotheo 2:19 “Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu”.

SASA UTAJITAMBUAJE KUWA WEWE NI MMOJA WA WALE WALIOKUSUDIWA UZIMA WA MILELE, AU LA..

Kama tulivyosoma hapo juu anasema wote walioakusudiwa uzima wa milele WALIAMINI..Unaona? Waliamini kile walichohubiriwa wakati ule ule, maana yake wakaenda kubatizwa, wakadumu katika imani, na utakatifu, wakawa kila siku wanalitendea kazi lile Neno walilokuwa wanafundishwa na mitume..

Lakini wale wengine ambao hawakukusudiwa ambao walikuwa wanajiona wao ni watu wa dini, watu waliozaliwa katika imani hao ndio Mungu aliowakataa, matokeo yake wakabaki vile vile,..Na ndivyo ilivyo hata leo, Ukiona umeshahubiriwa injili, miaka nenda rudi, lakini ndani yako hakuna badiliko lolote, au wokovu unauchukulia kama jambo lisilokuwa la maana sana kwako, fahamu kuwa wewe hujakusudiwa uzima wa milele..Kwasababu ungekuwa umesudiwa uzima wa milele, usingepambana au kushindana na habari njema za Yesu Kristo, pale unapoambiwa utubu dhambi.

Biblia inasema njia ile ni nyembamba iendayo uzimani,..Pengine Ni Mungu anasema na wewe leo, ili umgeukie, pengine wewe ni mmojawapo wa waliokusudiwa uzima wa milele, na ndio maana unasikia Roho Mtakatifu akiugua ndani yako..Basi kubali wito huo haraka na kumpokea Yesu kwa moyo wako wote siku ya leo, ili uwe mmojawapo wa wale ambao majina yao yalishaandikwa katika kitabu cha uzima kabla hata ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu.

Ikiwa upo tayari kufanya hivyo leo hii, Kumkabidhi Yesu Kristo maisha yako.

Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako ili kuukamilisha wokovu wako.

Ubarikiwe sana

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

KWANINI YESU KRISTO NI WA MUHIMU KWETU SASA?

MUUNGANIKO WA MADHEHEBU NI MPANGO WA MPINGA-KRISTO.

 

UCHAWI WA BALAAMU.

YULE JOKA WA ZAMANI.

KWANINI MUNGU ALIMTUMIA MUSA KWA VIWANGO VILE?

USIPOWATAMBUA YANE NA YAMBRE, KATIKA KANISA LA KRISTO, UJUE UMEPOTEA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments