YULE JOKA WA ZAMANI.

YULE JOKA WA ZAMANI.

Kwanini Shetani ni joka wa zamani?


Shalom, ni kwa neema za Mungu wetu tumeliona tena jua leo..wapo ambao hawakupata nafasi hiyo, hivyo hatuna budi kumshukuru sana Mungu wetu. Karibu tujifunze Neno la Mungu chakula cha kweli cha roho zetu.

Biblia inasema katika..

Ufunuo 20:1 “Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake.

2 Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu;”

Shetani anajulikana kama joka wa zamani..ikiwa na maana kuwa ameishi muda mrefu, na ameishi katika hali hiyo hiyo ya ujoka tangu zamani…Na kama unavyojua kitu chochote ambacho kimeishi muda mrefu, kwa mfano mtu aliyeishi muda mrefu ni lazima atakuwa anajua mambo mengi…wazee wenye umri mkubwa wanakuwa wanajua mambo mengi zaidi kuliko vijana..

Kwasababu wamekumbana na mambo mengi katika maisha yao na wamejifunza mambo mengi, wamejifunza kutokana na makosa yao na kutokana na makosa ya watu wengine…hivyo hawawezi kufananishwa hata kidogo na watoto waliozaliwa hivi karibuni.

Vivyo hivyo shetani naye anajulikana kama joka wa zamani…

maana yake ni kwamba anajua mambo mengi sana yamhusuyo mwanadamu…alikuwepo tangu Edeni, anamjua Adamu kwa sura na tabia hajamsahau,..anamjua Hawa…anamjua Nuhu, na alikuwa anashuhudia jinsi dunia ilivyokuwa inaangamizwa kwa gharika…alikuwepo anatazama…Bado anaikumbuka sura ya Ibrahimu na ya Sara…anakumbuka ni wapi walipomsumbua katika maisha yao..Anamkumbuka Musa..na bado anazijua tabia zake zote na anaujua udhaifu wake..Anayo sura ya Danieli na ya Nebukadneza, na ya Eliya kichwani mwake na anazikumbuka tabia zao…Na zaidi ya yote anamfahamu sana Mkuu wa Uzima Yesu Kristo, anakumbuka matukio yote tangu anazaliwa mpaka alipokuwepo kule jangwani akimjaribu, na alipokufa na kufufuka, anajua nguvu zake na mamlaka yake aliyonayo sasa…

Vivyo hivyo anawajua watu, anawajua watu na tabia zao, anajua wanapenda nini, na hawapendi nini…Ameviona vizazi vyote tangu Adamu mpaka sasa…Hebu jiulize wewe tu mpaka umri ulioufikia sasa ambao pengine haujazidi hata miaka 60 lakini tayari umeshajua tabia za baadhi ya watu na baadhi ya makabila kiasi kwamba pengine hata ukimwona tu mtu Fulani tayari umeshajua kundi la kumweka hata kabla ya kuendelea mbele sana…Sasa kama wewe na miaka yako hiyo 50 tu tayari unajua jamii za watu na tabia zao…Unafikiri shetani atakuwa anawajua wanadamu kwa kiwango gani?..maana yeye tangu Edeni mpaka leo yupo.

Nataka nikuambia anawajua wanadamu vizuri..anajua ni wapi pa kuwashikia watoto, watu wazima na wazee…kwasababu mwanadamu ni Yule Yule…na biblia inasema hakuna jipya chini ya jua…anajua namna ya kummaliza mtu mchanga kiroho pindi tu anapotaka kujaribu kumtafuta Mungu…kwasababu alishajaribu kwa watu kadhaa huko nyuma wa vizazi vilivyopita na akafanikiwa…Anajua ni jinsi gani anaweza kuwaangusha watumishi wa Mungu..kwasababu alishajaribu huko nyuma na akafanikiwa kwa baadhi hivyo anatumia huo huo uzoefu kwa watu wa vizazi vyote. Anajua jinsi ya kuwazuia watu wasisali, wasimtafute Mungu n.k kwasababu alishaijaribu hiyo njia huko nyuma na ikafanya kazi.

Ndugu mpendwa usipoingia ndani ya Yesu kisawasawa hutamweza shetani kwa vyovyote vile anazo akili nyingi za kukuzidi wewe na mimi, ukisema humtaki Bwana Yesu na kwamba unaweza kujizuia usizini bila hata ya kuwa ndani ya Kristo, unapoteza muda wako! Siku moja utazini tu..alishawajaribu watu kama nyie huko nyuma na akawanasa hivyo wewe sio wa kwanza kuwaza hivyo au kujaribu hivyo..Ukisema naweza kufanya hichi chema au kile bila kuwa ndani ya Yesu..nataka nikuambie ni muda tu unaupoteza..watu kama nyie shetani alishawatafutia suluhisho lake pengine hata zaidi ya miaka 2000 iliyopita huko nyuma…wewe unaweza kukiri ni wa kwanza lakini kumbe hata ni wa milioni 10 kwenye kalenda zake na orodha zake za watu waliojaribu kufanya kama wewe huku wakiwa nje ya Kristo na akawashinda..

Hivyo wewe uliyezaliwa juzi huwezi kumzidi hekima Yule aliyekuwepo miaka mingi iliyopita huko nyuma…(Hujui ni kwanini shetani anaitwa mungu wa ulimwengu huu? Ni kwasababu anajua mambo ya wanadamu sana kuliko mwanadamu yoyote yule).

Ndio maana Bwana Yesu alimwambia kwamba siku zote anayawaza yaliyo ya wanadamu na si ya Mungu.. Kwanini? kwasababu anakesha kumsoma mwanadamu na namna ya kumtawala. Kasome (Mathayo 16:23)..

Hivyo utauliza kama shetani anayajua mambo ya wanadamu kiasi hicho, kiasi kwamba hakuna upenyo wa kuweza kumzidi ni nani basi atasalimika?

Jibu ni kwamba pamoja na ukongwe wake wote wa kuwafahamu wanadamu, yupo mmoja ambaye ni mkongwe zaidi yake..Na huyo si mwingine zaidi ya Mungu mwenyezi aliye Baba yetu ambaye tunamwabudu sisi kupitia Yesu Kristo(Danieli 7:9). Huyo anajulikana kama MZEE WA SIKU.

Danieli 7:13 “Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia HUYO MZEE WA SIKU, wakamleta karibu naye.

14 Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa”.

Baba yetu anatujua kuliko shetani anavyotujua..shetani anauzoefu wa kutuangusha lakini Hekima iliyo kwa Mungu inauwezo hata wa kuyajua mawazo yake na nia yake na mipango yake, na kuyaangusha chini mawazo yake..chochote anachotaka kukifikiria kwa uzoefu wake, sisi tulio ndani ya Kristo tayari tunauwezo wa kuitegua mitego yake..hekima ile ya Kiungu inaingia ndani yetu ambayo inatupa uwezo wa kuzitambua na kuziangusha fikra zote za shetani. Lakini hekima hiyo wanapewa wale tu wanaomwamini mwanae mpendwa Yesu Kristo.

Wengine wote walio nje ya Kristo kamwe hawataweza kumshinda Yule joka wa zamani ambaye ni Ibilisi..watapelekwa kule shetani anakotaka waende..hata kama hawataki, ndio maana mtu ambaye hajaokoka kisawasawa kamwe hawezi kuwa na Amani, na hawezi kuishinda dhambi, na mapenzi ya ulimwengu huu ndio anayoyatenda…wakati mwingine anapanga hiki lakini mwishoni kinaishia kuwa kingine…kwanini? Ni kwasababu anataka kujiongoza mwenyewe na kudhani anaweza kufanikiwa kwa nguvu zake na akili zake.

Hivyo kama hujaokoka, bado tumaini la kumshinda Yule joka lipo, Hekima ya kiMungu inataka kuingia leo ndani yako…usimsikilize shetani anayekuwambia akilini mwako sasahivi kwamba huwezi kuokoka kwamba unadhambi nyingi na Mungu hawezi kukusamehe…ndivyo alivyowaambia watu wengi wa vizazi vya nyuma na kuwaangusha..anatumia ukongwe wake tu…lakini wewe leo mkatae na mkane kwa vitendo…Amua leo kuacha dhambi, na kutubu, amua kuacha kwenda disko, amua kuacha kusengenya, amua kuacha ulevi na uasherati na Bwana atakupenda sana…Na hekima ya ajabu itokayo kwa yule MZEE WA SIKU, (YEHOVA) Mungu wetu,itaingia ndani yako itakayoweza kutambua mitego yake na hila zake…

Mithali 2:6 “Kwa kuwa Bwana huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu;

7 Huwawekea wanyofu akiba ya hekima kamili; Yeye ni ngao kwao waendao kwa ukamilifu;

8 Apate kuyalinda mapito ya hukumu, Na kuhifadhi njia ya watakatifu wake.

9 Ndipo utakapofahamu haki na hukumu, Na adili, na kila njia njema.

10 Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;”

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 78900131

Mada Nyinginezo:

ANGUKO LA UFALME WA SHETANI:

ZIFAHAMU HUDUMA KUU (10) ZA SHETANI DUNIANI.

NI NANI ALIYEWALOGA?

JINSI NEEMA YA MUNGU ILIVYOKUWA KUBWA KWA MKE WA LUTU.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments