MKARIBIE BWANA ZAIDI ILI UFANYIKE NGUZO.

MKARIBIE BWANA ZAIDI ILI UFANYIKE NGUZO.

Mkaribie Bwana.

Shalom, karibu tujifunze Neno la Mungu..

Miongoni mwa watu waliokuwa wanamfuata Bwana Yesu kulikuwa na makundi manne..1) Makutano 2)Wanafunzi 3)Mitume 12 na 4) Nguzo.

Kundi la kwanza ambalo ni makutano, hawa walikuwa tu wanakusanyika kusikiliza mahubiri ya Bwana Yesu ambao mara zote Bwana alikuwa anazungumza nao kwa mifano, na kuwaponya magonjwa yao..baada ya hapo walikuwa wanarejea katika shughuli zao na maisha yao ya kawaida.

Kundi la pili ambalo lilikuwa ni la wanafunzi wa Yesu, hawa walikuwa wapo kama 70 hivi au zaidi kidogo..Kundi hili ni lile ambalo lilikuwa linamfuata Bwana Yesu lakini si kila mahali…Ni baadhi ya watu ambao waliamua kujitoa kumtumikia Yesu sehemu zote alizokuwa anakwenda…na hawa pia Bwana alikuwa anawatuma kuhubiri injili kila mahali ambapo Bwana alipokuwa anataka kwenda. (Soma Luka 10:1).

Kundi la tatu lilikuwa ni Mitume…Mitume hawa walikuwa 12 tu, na waliteuliwa na Bwana Yesu kati ya lile kundi la wanafunzi 70 waliokuwa wanamfuata Yesu.

Luka 6: 13 “Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume”

Kundi la mitume ndio lilikuwa linamkaribia sana Bwana kuliko wale wanafunzi 70 na makutano..Hawa kila mahali Bwana alipokuwa na wao walikuwepo, walikula nae na kunywa naye…na mbele za Bwana ni kama vile walipendelewa zaidi kuliko wanafunzi wengine kwasababu kila mfano ambao Bwana aliokuwa anawafundisha makutano usioeleweka wao ndio walikuwa wanapata fursa ya kwenda kumwuliza akiwa peke yake, maana ya mifano hiyo, nafasi ambayo makutano wala wale wanafunzi wengine hawakuipata.

Lakini lilikuwepo kundi la mwisho ambalo ni la kipekee sana..ambalo hilo lilikuwa karibu sana na Bwana zaidi ya makundi hayo matatu yaliyotangulia…na kundi hilo lilitwaliwa kutoka miongoni mwa wale wanafunzi 12…Na hao walikuwa watatu tu ambao ni (Petro, Yohana na Yakobo)..Hawa watatu walijulikana kama NGUZO.

Wagalatia 2:9 “tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; YAKOBO, na KEFA na YOHANA, WENYE SIFA KUWA NI NGUZO, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;”

Kefa ni jina lingine la Petro(soma Yohana 1:42). Hawa watatu walijulikana kama nguzo…Maana yake walikuwa wanauhusiano wa kipekee na Bwana zaidi ya mitume wote, zaidi ya wanafunzi wote na zaidi ya makutano yote.

Utaona hawa watatu kila mahali ambapo Bwana alitaka kwenda peke yake (labda mlimani kusali, au kuwafunulia siri za ndani sana) aliwachukua hawa watatu tu Yohana, Yakobo na Petro, na si mitume wengine waliosalia..Hebu tuangalie mifano michache kulithibitisha hili..

Luka 9:27 “Nami nawaambia kweli, Wapo katika hawa wanaosimama hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata wauone kwanza ufalme wa Mungu.

28 Baada ya maneno hayo yapata siku nane, aliwatwaa PETRO NA YOHANA NA YAKOBO, AKAPANDA MLIMANI ILI KUOMBA.

29 Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta.

30 Na tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya”

Unaona hapo walikuwepo mitume wote lakini Yesu aliwachagua tu hao watatu kwenda nao mlimani..kusali na huko akawafunulia ufunuo mkubwa namna ile, na wakaisikia sauti ya Mungu ikisema huyu ni mwanangu mteule wangu, msikieni Yeye. Ufunuo huo waliouona tu hawa watatu, na Bwana aliwaambia wasimwambie mtu mwingine yoyote mpaka atakapofufuka katika wafu. Maana yake ni kwamba wanafunzi hawa walikuwa na siri nyingi ambazo Bwana aliwafunulia ambazo mitume wengine hawakuzijua.

Tutazame mfano mwingine tena..

Mathayo 26:36 “Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe.

37 Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka.

38 Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.

39 Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.

40 Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?”

Hapo utaona Bwana alitenga makundi mawili..kundi la kwanza ambalo ndilo lile la mitume 9 aliliacha kule kwenye bustani ya Gethsemane….hakuenda nalo kuomba usiku ule, badala yake akawachukua Petro, na wale wana wawili wa Zebedayo ambao ni (Yohana na Yakobo), hao ndio akaenda nao kusali..na hao ndio aliowaambia wakeshe waombe pamoja na yeye wasije wakaingia majaribuni..kwasababu shetani ndio aliokuwa anawawinda zaidi kwasababu walikuwa na Bwana zaidi..Na kama wewe ni msomaji wa biblia utagundua kuwa wakiwa kule waliona tena ishara nyingine wakati Yesu akiwa anaomba jasho lake lilikuwa kama matone ya damu, na pia waliona malaika wakija kumtia nguvu…

mambo hayo mitume wengine waliosalia hawakuyaona…

Na hawa watatu, hata wakati wa Pentekoste na kuendelea ndio mitume Bwana alitembea nao kwa viwango vikubwa sana..mpaka watu wote wakawaita kuwa ni NGUZO YA KANISA. Kitabu cha Ufunuo wa Yohana, ambacho kimebeba siri nyingi za ufunuo wa siku za mwisho, na ujio wa Bwana Yesu kimendikwa na Yohana huyu…ambaye ndiye mmoja wao wa wale watatu.

Sasa kwanini wanafunzi hawa watatu waliteuliwa na Bwana kuwa karibu zaidi na yeye kuliko wengine wote?

Jibu ni kwamba, kwasababu walimpenda Bwana zaidi..Mungu hana upendeleo hata kidogo..kila dakika, kila muda walikuwa wanamtafakari Bwana, wanamfikiria yeye, wanamtumikia yeye, na wamejikana nafsi na kusema lolote liwalo tutamfuata Yesu Bwana wetu popote aendapo, kwa moyo huo Bwana akawapenda zaidi na hivyo kuwakaribisha wamsogelee zaidi kuliko wengine…Kama ni mwanafunzi wa Biblia utamjua Petro alivyokuwa anampenda Bwana…ilifika wakati akamwambia Bwana wajapochukizwa wote kwaajili yako mimi sitachukizwa..ijapokuwa alikuwa ni dhaifu lakini angalau hata alikuwa anaujasiri wa kusema hivyo tofauti na wengine…

Hali kadhalika Yohana na Yakobo ni hivyo hivyo,..walimpenda Bwana mpaka ikafikia wakati wakamwendea Bwana wao na kumwomba katika ufalme wake waketi mmoja mkono wake wa kuume na mwingine wa kushoto…(walimpenda Bwana mno na hivyo Bwana akawapenda zaidi). Yohana ilifika wakati akawa anaegemea kifuani mwa Yesu kila mahali…na ilifika kipindi Bwana akawaambia wazi wazi kuwa mmoja wao atamsaliti..na kila mmoja akawa anawasiwasi ni nani amtajaye..na Bwana akamfunulia Yohana peke yake kwamba ni Yuda kwa sauti ya chini, wengine hawakusikia.. kwasababu alikuwa karibu sana na yeye kifuani mwake…

Yohana 13:23 “Na palikuwapo mmoja wa wanafunzi wake, ameegama kifuani pa Yesu, ambaye Yesu alimpenda.

24 Basi Simoni Petro akampungia mkono, akamwambia, Uliza, ni nani amtajaye?

25 Basi yeye, hali akimwelekea Yesu kifua chake, akamwambia, Bwana, ni nani?

26 Basi Yesu akajibu, Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote”.

Tabia ya hawa watatu kuwa tayari chochote Bwana alichowaambia ndizo zilizowafanya kuwa karibu zaidi na Bwana kuliko wengine, Bwana alipotaka kwenda kuomba walikuwa tayari kutaka na wao kwenda kuomba..walikuwa hawaonyeshi dalili za uvuvi ingawa walikuwa na madhaifu, walijinyima kila kitu ili tu wampendeze Yesu.

Vivyo hivyo Neno la Mungu linasema..Yakobo 4:8 “Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili”.

Unapojikana nafsi na kumpenda Mungu zaidi, na kumfanya yeye ndio wakwanza kila mahali, hapo ndipo unapojitengenezea daraja zuri la Mungu kukukaribia zaidi..ndipo unapoongeza daraja zuri la Mungu kukupenda zaidi ya wengine, kukufunulia siri nyingi zaidi ya wengine…kukutumia na kukubariki. Unapoutafa uso wa Mungu kwa kusali, kufunga, kutenda mema zaidi ya wengine..mema yako yanapimwa mbele za Mungu kila siku na yanapoonekana yamezidi ya wengine wengi ndipo na wewe thamani yako inapanda mbele za Mungu, lakini kama leo ukiambiwa tu usali..hata dakika mbili humalizi, kusoma tu neno ni mara moja kwa wiki, na hata ukisoma unasoma tu mistari na sio mada nzima..hapo utafanyikaje NGUZO mbele za Mungu.?

Hivyo tusiridhike na uhusiano wetu na Mungu..Tuzidi kumkaribia Bwana..kutoka kuwa wanafunzi wake, hata mitume wake hata Nguzo..

Ufunuo 3: 12 “Yeye ashindaye, nitamfanya kuwa NGUZO katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo tena kabisa, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, na jina la mji wa Mungu wangu, huo Yerusalemu mpya, ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, na jina langu mwenyewe, lile jipya”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Maran atha!


Mada Nyinginezo:

MUUNGANIKO WA MADHEHEBU NI MPANGO WA MPINGA-KRISTO.

INGIENI KWA KUPITIA MLANGO ULIO MWEMBAMBA.

YULE JOKA WA ZAMANI.

KUOTA UNAANGUKA .

NAO WALIOKUWA WAMEKUSUDIWA UZIMA WA MILELE WAKAAMINI.

TIMAZI NI NINI

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
YOHANA NIZO
YOHANA NIZO
2 years ago

UBARIKIWE

Nabii wa Mungu
Nabii wa Mungu
4 years ago

Nimebarikiwa na mafundisho kumtumikia Mungu kunahitaji kujikana na ya ulimwengu huu Bali kubaki kumtumikia Mungu daima.