Ni muhimu kupambana sana mpaka kufikia hatua ya Mungu kuwa kila kitu kwetu, maana yake hata watu wote wakikuacha, au kukutenga, au kukusahau, bado MUNGU ni faraja tosha kwako zaidi ya watu elfu, au ndugu elfu.
Tukifikia hii hatua tutakuwa watu wa furaha siku zote, na watu wa kuishi bila kutegemea sana hamasa kutoka kwa watu au vitu.
Tukiweza kufikia kiwango kwamba faraha kutoka kwa watu haziwi sababu kuu za msukumo wetu kue delea mbele, tutakuwa watu wakuu sana mbele za Mungu.
Pia tukiweza kufikia kiwango kwamba maneno mabaya au dhihaka au kukatishwa tamaa na watu haziwi sababu ya kukata tamaa na kuumia, pia tutakuwa watu wa kuu sana mbele za watu.
Wakristo wengi tunahamasika sana pale tunapohamaishwa na watu, tunapata nguvu zaidi pale tunapotiwa nguvu na watu, na pia tunavunjika moyo sana pale tunapovunjwa moyo na watu, lakini haikuwa hivyo kwa Bwana wetu YESU KRISTO, yeye faraja yake na huzuni yake ilikuwa kwa Baba..
Kiasi kwamba hata watu elfu wangemtukuza na kumtia moyo kama kutiwa huko moyo hakujatoka mwa Baba yake, hakukuweza kumhamasisha kitu.
Hali kadhalika hata watu wote wakitoa maneno ya kuvunja moyo au watu wote wakimwacha na akabaki peke yake, maadamu anaye Baba yake haikumvunja moyo wala kumkatisha tamaa, ndivyo maandiko yasemavyo..
Yohana 16:32 “Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami”.
Hapo Bwana YESU aliona saa inakuja kwamba kila mtu atamkimbia na atabaki peke yake na kweli huo wakati ulitimia pale askari wa Herode walipokuja kumkamata Bwana Yesu pale bustanini, maandiko yanatuonyesha walikimbia wote, na hata mwengine walikimbia uchi (Marko 14:51-52).
Lakini hatuoni Bwana Yesu akivunjika moyo kwa hilo tendo, kwasababu anajua na ana uhakika kwamba Baba yupo naye..
Anajua watu wote wakimwacha haimaanisha Baba yake kamwacha…
Lakini ulipofika wakati wa Baba kumwacha kwa kitambo kwasababu ya dhambi za ulimwengu, ndipo tunaona Kristo anajali na kuhuzunika..
Mathayo 27:46 “Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”
Na sisi hatuna budi kufika hii hatua, Mungu wetu, na Baba yetu abaki yeye kuwa faraja yetu ya mwisho, kiasi kwamba hata dunia nzima ikiondoka, Baba yetu atabaki kuwa hamasa yetu, faraja yetu, yaani awe mwanzo na mwisho kwetu.
Na hata dunia nzima ikutusifia na kutupa maneno ya hamasa, bado hamasa ya Baba yetu ndio itakayokamilisha furaha yetu.
Bwana Yesu atusaidie sana.
Zaburi 9:10 “Nao wakujuao jina lako wakutumaini Wewe, Maana Wewe, BWANA hukuwaacha wakutafutao”