FUNGUO ZA UZIMA, MAUTI NA KUZIMU.

FUNGUO ZA UZIMA, MAUTI NA KUZIMU.

Shalom, mtu wa Mungu..karibu tujifunze Biblia…

Katika kisiwa cha Patmo, Bwana Yesu alimtokea Yohana alipokuwa ametelekezwa kule na kumwambia maneno mengi sana kama tunavyoyasoma katika kitabu cha Ufunuo. Na moja ya maneno aliyomwambia ni haya.

Ufunuo 1:17 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,

18 na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu”

Mtu aliye na funguo maana yake yeye ndie mwenye uwezo wa kuingia na kutoka, au ana uwezo wa kumruhusu mtu mwingine aingie au atoke. Ana uwezo pia wa kumfungia mtu nje au akamfungia ndani. Vilevile huwezi kuzungumzia funguo bila mlango.

Sasa kuna Malango makuu matatu katika maisha 1)  Lango la  MAUTI  na 2) Lango la KUZIMU na 3) Lango la UZIMA WA MILELE

  1. Lango la MAUTI.

Lango la mauti ni hatua ile ya mwisho kabisa mtu anapouacha mwili na kufa..Anakuwa anaingia katika upeo mwingine, ambao sio wa maisha haya ya duniani. Huko anakwenda kukutana na vitu vipya ambavyo havipo hapa duniani aidha vizuri au vibaya. Katika huu mlango au geti kabla ya agano jipya ilikuwa haiwezekani mtu aliyeenda huko arudie tena huku ulimwenguni. Ukifa hakuna kurudi, wanaoingia mautini wanakuwa wamefungiwa huko huko milele. Lakini baada ya Kristo na kuzitwaa funguo za Mauti, ndipo ukazaliwa uwezekano mpya wa wafu kurudia tena uhai… Na huo ulianza na Yesu mwenyewe kutoka kaburini na kurudia uhai, na siku ile tu alipokufa wapo wengine waliotoka makaburini Pamoja naye, wale waliokufa katika haki wakati wa agano la kwanza.

  1. Lango la Kuzimu.

Lango hili mtu analiingia baada ya kifo, Mtu aliyekufa katika dhambi, pasipo kutubu..anapokufa baada ya kuvuka lango la kwanza la Mauti, anaingia lango la pili la kuzimu. Huko ni sehemu mbaya isiyofaa. Na huko nako kuna malango mengine madogo madogo kumtenganisha mwovu na mwovu..hatutaingia huko sana. Lakini katika lango hili kuu la kuzimu, waliokuwa wamekufa katika uovu katika agano la kale, ilikuwa haiwezekani kutoka huko milele. Lakini Kristo alizitwaa funguo, na siku moja wafu waliopo kuzimu watatolewa huko kwaajili ya hukumu na wakiisha hukumiwa watatupwa katika ziwa la moto. 

Yohana 5:27  “Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu. 

28  Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. 

29  Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu”.

Hivyo hata wafu waliopo kuzimu siku moja watatolewa huko kwaajili ya hukumu. Ufunuo 20:13  “Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake”. Ufufuo huu sio mzuri kabisa kwasababu ni wa hukumu.

Na roho ya malango ya kuzimu inafanya kazi hata kabla ya mauti, roho hiyo ndiyo inayowavuta watu wengi waiendee njia iliyopotea, shetani na majeshi yake wanafanya kazi kwa nguvu sana kuhakikisha ni kundi kubwa linataingia kuzimu.

  1. Lango la UZIMA WA MILELE:

Lango hili ni ndio la lenye maana  kwetu wanadamu, kwasababu ndio lango la uzima wa milele. Tofauti na malango hayo mengine ambayo yanahitaji kifo ndipo uyaingie.. Lango hili la uzima wa milele halihitaji mtu ufe, linaanzia hapa hapa duniani..wakati huu huu mtu anapumua na kuishi katika mwili wake. Lango hili ni bure kuingia lakini linahitaji kupambana sana, kwasababu yupo mwingine adui yetu ambaye hatamani hata mmoja wetu aingie.

Lango hili ni lile Bwana Yesu alilolisema katika kitabu cha Luka..

Luka 13:24  “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. 

25  Wakati mwenye nyumba atakaposimama NA KUUFUNGA MLANGO, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako; 

26  ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu. 27  Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu. 

28  Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje”.

Kama tunapenda uzima wa milele basi lango hili lipo wazi mbele yetu leo, Bado Bwana Yesu hajalifunga na tunaingia ndani ya lango leo hili kwa kuyatii maneno yake yanayohubiriwa katika biblia takatifu na yanayohubiriwa na watumishi wake. Lakini tukiyakataa maneno yake basi mlango huu utafungwa mbele yetu.

Wapo watu wanaoishi hapa duniani ambao tayari wameshafungiwa mlango huu.(kwamfano watu waliomkufuru Roho Mtakatifu tayari wameshafungiwa, hao kamwe hawawezi kusamehewa tena kadhalika na watu baadhi ambao wameisikia injili kwa muda mrefu sana, wamepigiwa kelele sana, injili imerudiwa na kurudiwa masikioni mwao lakini hata kujigusa hawajigusi, wengi wameshafungiwa huu mlango hivyo kamwe hawataweza kusikia tena ile hamu ya kutubu na kuvutwa kwa Mungu).

Yesu ndiye mwenye funguo za hili lango na funguo hizo pia amewapa watumishi wake..Hebu tusome maandiko yafuatayao ili tuelewe Zaidi..

Yohana 20:21  “Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. 

22  Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. 

23  Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa”.

Umeona hapo? Wale waliotumwa na Yesu kuhubiri wamepewa amri ya kuwafungia watu dhambi..Na hawawafungii kwa kutamka mdomoni kwamba “Fulani nakufungia dhambi” hapana hiyo sio tafsiri yake..Tafsiri ya kuwafungia watu dhambi iliyozungumziwa hapo ni hii >>

Mathayo 10:14  “Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung’uteni mavumbi ya miguuni mwenu.

15  Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule”.

Kwahiyo mtu anaposikia injili na kuidharau tena kuikejeli..Yule mtumishi wa Mungu Roho Mtakatifu anapomwongoza aondoke mahali pale..hao waliosalia hapo nyuma, ndio Habari yao imeisha!..hawatapata tena neema kamwe, wataendelea katika njia hiyo hiyo! Mlango umefungwa tayari. Hali kadhalika wanapoikubali na kuitii, basi wanafunguliwa mlango ambao malango ya kuzimu hayataiweza..maana yake hao watu watakaoitii injili inayohubiriwa na mtu yule aliyetumwa na Mungu..basi ni ngumu sana kupotea…Watakuwa wana ulinzi Fulani wa daima ambao hata wakirudi nyuma kidogo nguvu ya Mungu itawarudisha kwenye mstari kwasababu tu! Waliitii injili ya Kristo. Bwana Yesu alimwambia maneno haya Petro.

Mathayo 16:18  “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. 

19  Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni”

Petro ni mfano wa watu wote waliothibitishwa na Mungu na kuwekwa wakfu kwa ajili ya kazi yake.

Hivyo dada/kaka unayesikia maneno haya. Kama unapenda kuishi Maisha yasiyo na mwisho…miaka milioni kwa mamilioni yasiyo na shida wala taabu, wala uchungu…Njia ni moja tu, nayo ni Yesu. Yeye ndiye mwenye funguo za Uzima wa Milele, na funguo hizo amewapa watumishi wake pia..Ukitaka kuishi, ukitaka uzima..Mkubali Yesu. Ukimkubali Yesu malango ya kuzimu yatakukwepa..kuna nguvu fulani itaachiliwa juu yako ambayo atakuweka katika mstari uliyoonyooka..Lakini kama hutaki kuishi milele, basi malango ya Mauti na kuzimu yanakungoja, hivyo chagua chaguo jema, Yesu ndiye lango na anakupenda!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

KUZIMU ni mahali pa namna gani, Je! huko wanaishi watu wakifa na kwenda kupata mateso au ni vinginevyo?

USIUZE URITHI WAKO.

HASIRA YA MUNGU KUKUWAKIA, KWA KUTOMZUNGUZIA TU MUNGU IPASAVYO.

FAHAMU MAJIRA ULIYOPO NA NINI UNAPASWA UWE NACHO.

MWANAMKE ULIYEKOMAA KI-UMRI, ITAMBUE HUDUMA YAKO.

NI KITU GANI PETRO NA YOHANA WALIKIGUNDUA KABURINI?

UHARIBIFU HAUNA KIFUNIKO.

Kuna ufufuo wa aina ngapi?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments