FAHAMU MAJIRA ULIYOPO NA NINI UNAPASWA UWE NACHO.

FAHAMU MAJIRA ULIYOPO NA NINI UNAPASWA UWE NACHO.

Kiwango cha uelewa kuhusu wokovu au Mungu waliokuwa nacho Kiwango cha uelewa, hutupaswi tuwe nacho sisi kwa wakati huu, tunapaswa tuende zaidi ya pale, Hata mambo ya kidunia yanatufundisha, elimu ya kidato cha 4 aliyokuwa nayo mtu wa mwaka 1960, Si sawa na elimu ya kidato cha 4 aliyonayo mtu wa sasa hivi.

Wakati ule, elimu hiyo ilimtosha mtu kupata kazi hata ngazi za juu katika mashirika makubwa, lakini kwa sasahivi elimu hiyo haina thamani yoyote japokuwa ni elimu ile ile.

Ndivyo ilivyo hata katika ukristo, wakati mwingine unajiuliza ni kwanini hauisikii nguvu ya wokovu ndani yako, japokuwa utasema umeokoka, na umefuata vigezo vyote vya kuokoka kama tu watu wa kale walivyofanya, lakini bado huoni ndani yako moto kama waliokuwa nao wale, Ni kwasababu tunataka tuishi kama watu wa zamani, kama kipindi cha mitume, kama kipindi cha Martin Luther, kwamba ukimkiri Yesu kwa kinywa ya kuwa ni Bwana na tena ukaamini kwamba alikufa akafufuka utaokoka (Warumi 10:9)..Hilo tu basi!..

Kwa kudhani kwamba hilo tu linatosha kutufanya tuimalize hii safari salama. Ndugu hilo lilitosha kwa wakati wao, ambao kwanza hawakupata neema ya kuwa na mikusanyiko ya vitabu vyote vya maandiko kama tulivyonavyo sisi, Au kama walikuwa navyo basi hawakuruhusiwa kuvisoma (Fuatilia historia utaona), hiyo ni moja, pili, shetani alikuwa hafanyi kazi kwa nguvu kama anavyofanya sasa hivi.

Ikiwa hutaki kuongeza maarifa yako kuhusu Mungu katika nyakati hizi, na umeng’ang’ana tu kusema mimi nilishaokoka basi, nataka nikuambie kuwa ukristo wa namna hiyo safari hii hautakufikisha popote. Hilo pekee halitoshi kukufikisha popote, wala kutufikisha popote!.

Hili ndio kanisa pekee linaloonekana lina makundi mawili ya wakristo (yaani Wanawali werevu na Wanawali wapumbavu. Math.25). Ikiwa na maana kutakuwa na wakristo wenye bidii ya kupata maarifa, na wakristo ambao hawatakuwa na ujuzi wowote mioyoni mwao, na biblia inaonyesha  wale werevu tu ndio watakaoenda kwenye unyakuo. Jambo hilo halikuwahi kuonekana katika vipindi vyote vya kanisa huko nyuma..

Na katika wakati ambao ni mgumu kuliko wakati wote uliowahi kutokea katika historia ya dunia basi ni huu!, kwasababu hili ndio kanisa la mwisho lijulikanalo kama Laodikia, “ndio tonge la mwisho linalokomba mboga yote” na shetani analijua hilo, huu ndio wakati wake wa kufanya kazi kwa nguvu zaidi ili kuwaangusha wengi, Hivyo wewe na mimi tunaojiita mkristo tusipojua ni nini tunapaswa tuwe nacho kwa majira haya, ndugu basi tumekwisha!.

Ukisoma kitabu cha Ufunuo, utaona wapo wale wenye uhai 4, wanaosimama mbele ya kiti enzi cha Mungu, mmoja akiwa na uso kama wa Simba, mwingine wa Ndama, mwingine kama wa mwanadamu na Mwingine kama wa Tai (Ufu 4:7).

Sasa hizo nyuso zao na mionekanayo yao sio urembo tu, hapana bali zilikuwa zinafunua nguvu za Roho Mtakatifu katika nyakati tofauti tofauti za kanisa..Sasa mwenye uhai wa kwanza hadi yule wa Tatu, walifanya kazi kwa vipindi vya makanisa 6 ya mwanzo, kwa urefu wa Habari hiyo fungua hapa >> UFUNUO: Mlango wa 4

Lakini yule mwenye uhai wa 4 ambaye ndiye mwenye uso wa Tai, alianza kutenda kazi katika kanisa la 7 na la mwisho lijulikanalo kama Laodikia, ambalo ndio tunaishi mimi na wewe, na kanisa hili lilianza mwaka 1906, (hilo linajulikana na wanazuoni  wote na wana theolojia wote duniani, sio jambo la kutengeneza)..

Sasa kama tulivyosema, Sio kwamba huyo mwenye uhai wa 4 ndio anayetenda kazi hapana, bali Ni Roho ya Mungu yenye tabia ya Tai ndio iliyoachiwa kwa kanisa la Mungu tangu huo wakati na kuendelea (Mwaka 1906- Pentekoste ya mwisho ilipoanza)

Hivyo mimi na wewe tunaishi katika  Upako huo wa Roho ya Tai.

Sasa ni kwanini iwe ni Tai na sio wale wengine, labda simba, au ndama, au mwanadamu?.

Ni kwasababu kanisa la sasa hivi linahitaji wakristo wenye jicho la TAI,..Kumbuka tai ni ndege anayeona tokea mbali kuliko kiumbe kingine chotechote duniani, Tai anaona kwa umbali ambao wewe mwenyewe huwezi kumwona angani. Anaweza kuona vitu vya mbali sana, vidogo sana,..tofauti na ndege wengine kama kuku, kuku yeye anaona hapa chini tu, lakini kile kinachotokea maili mbili mbele hawezi kukiona.

Hivyo jicho hilo la Tai ni jicho la kinabii, Kwamba wakristo wote waliopo duniani leo hii Roho hii inapaswa iwepo juu yao, ili wawezi kuushinda ulimwengu huu wa sasa, vinginevyo watakachukuliwa tu maji..Na ndio maana kusema tu Umeokoka, hilo halitoshi kwa majira haya..Ni lazima uwe na jicho la kinabii.. Na jicho la kinabii sio kuona maono usiku, wala wachawi, wala kutabiri…Bali ni utashi wa kujua wakati tuliopo, na kuona mambo yajayo, ambayo bado hayajafika yatakayoupata ulimwengu, na hivyo kuchukua tahadhari mapema.

Mungu alijua kabisa wakati huu udanganyifu utakuwa mkubwa duniani, na watu watamsahau Mungu kupindukia kama alivyosema watu watakuwa wa kupenda anasa kuliko kumpenda Mungu (2Timotheo 3:4), alijua kabisa kutatokea mapinduzi makubwa ya kiteknolojia, alijua kabisa kutakuwa na mwingiliano mkubwa wa watu na wa-kiutamaduni katikati ya mataifa, alijua kabisa dini nyingi zitaongezeka duniani, kiasi kwamba mpaka sasa duniani zipo dini Zaidi ya 4,300, ukristo ni mmojawapo na madhehebu yasiyoweza kuhesabika.

Alijua kabisa lile wimbi kubwa la makristo wa uongo, na manabii wa uongo, alilolitabiri zamani halitatokea wakati mwingine wowote, bali katika wakati wetu huu wa siku za mwisho.

Alijua kabisa wale watu wa kudhahaki, wale wanatakaosema yupo wapi huyo Yesu mnayemngojea mbona harudi, watazaliwa katika wakati wetu, (2Petro 3:3-4) mambo ambayo hapo nyuma hayakuwepo.

Alijua kabisa ile siri ya kuasi itakuwa inatenda kazi kwa nguvu, katikati ya ukristo, kiasi kwamba watu wengi watazombwa na nguvu hiyo..

Na ndio maana katika kizazi hichi chetu aliiachilia Roho ya Tai, Ili kukabiliana na udanganyifu uliopo sasa hivi. Na ni lazima kila mtu awe nayo, kwasababu ni kwaajili yetu.

Sasa dalili za mtu ambaye hana Roho hiyo ni ipi?

Ukiona hupendi kuongeza maarifa na kutaka kujifunza kitabu cha Ufunuo kinachozungumzia mambo yajayo, na vitabu vingine vya manabii, basi ujue Roho huyo bado hajaanza kutenda kazi ndani yako. Watu wengi tunadhani Mungu hana agenda yake ya kutimiza mambo, tunadhani tupo tu tunangojea siku Fulani ya unyakuo ifike halafu tuondoke kana kwamba hapa katikati Mungu hafanyi kazi yoyote.

Kama ulikuwa hufahamu Bwana Yesu alisema, kabla ya kurudi kwake atamtuma Eliya, ili kuigeuza mioyo ya wana iwaelekee baba zako, kwa kanisa letu Mungu alishaanza kutimiza hiyo agenda, na bado ataendelea kuitimiza,..Zipo ngurumo saba, ambazo zimezungumziwa katika Ufunuo 10:4. Ambazo hazijaandikwa kabisa katika maandiko, na hizo ni sharti zije zifunuliwe katika siku za mwisho kabla Kristo hajarudi, hapo ndipo Mungu atakapoitimiza siri yake yote (Ufu 10:7), kwasasa hivi siri ya Mungu bado haijatimizwa yote.

Hatujui sauti za ngurumo hizo 7 zitakuwa ni nini, Lakini siku zitakaposemwa duniani, wale wanawali wapumbavu hawataelewa chochote. Hata leo hii Mungu anasema, lakini usipokuwa na jicho la Tai huwezi kuona..Huwezi kuona hizi ni siku zenyewe, kwasababu macho yako yanaona tu ya ulimwengu huu, wapo ambao hata Ugonjwa wa Corona wanaona kama ni ugonjwa wa kibailojia tu, umetengenezwa na watu!. Huwajui kuwa hizi ndizo tauni Yesu alizozizungumzia zitatokea siku za mwisho (Luka 21:11).

Yapo mambo mengi, ya kujifunza wakati huu, Hivyo usiridhike na dini yako tu, au dhehebu lako tu, Chukua biblia yako, itafakari, na huko huko Roho Mtakatifu atakufundisha siri zake nyingi, na mipango yake, ukiwa msomaji wa biblia mzuri, itakuwa ni rahisi kuzijua hila za ibilisi kwa haraka, na kutokupotezwa na udanganyifu wa shetani wa siku hizi za mwisho.

Na zaidi sana kumwomba Mungu azidi kutuongezea jicho hilo la Tai ndani yetu kila siku. Kwasababu pasipo kuwa nalo hilo, hakuna Unyakuo.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

KWANINI UKATE TAMAA?

Ulokole ni nini? Na kwanini wakristo waliookoka wanaitwa walokole?

UTAWALA WA MIAKA 1000.

FAIDA ZA MAOMBI.

SHUKURU KWA KILA JAMBO.

HAPO NDIPO WATU WALIPOANZA KULIITIA JINA LA BWANA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Mary Mbodze
Mary Mbodze
2 years ago

Amen Amen barikiwa mtumishi wa Mungu