UFUNUO: Mlango wa 4

UFUNUO: Mlango wa 4

Shalom! Karibu tujifunze Neno la Mungu, leo tukiendelea na ile sura ya 4, tulishakwisha kuona katika sura zilizotangulia jinsi Mungu alivyotembea katika yale makanisa 7 yaliyokuwa Asia ndogo, yaliyowakilisha makanisa 7 katika nyakati saba tofauti tofauti kuanzia wakati wa Pentekoste hadi wakati wa kurudi kwa Bwana wetu Yesu Kristo mara ya pili, na tuliona pia sisi tunaishi katika kanisa la mwisho, linalojulikana kama Laodikia, na kwamba baada ya hili hakutakuwa na kanisa lingine la nane, kadhalika pia kila kanisa lilikuwa na mjumbe wake, na kanisa hili la mwisho mjumbe wake alikuwa ni Ndugu.William Branham ndiye Mungu aliyemnyanyua kubeba ujumbe wa nuru ya wakati huu wa mwisho. Hivyo ukiwa haujapitia sura zilizotangulia ni vizuri ukazipitia kwanza , ili tuende pamoja.

Sasa katika sura hii ya nne tunasoma..“1 Baada ya hayo naliona, na tazama, mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo”.

Hapa tunaona Mtume Yohana ambaye anamwakilisha bibi-arusi wa Kristo (Kanisa), akisikia sauti ambayo ndio ile iliyokuwa inazungumza naye hapo kwanza kutoka mbinguni, na sauti hiyo sio ya mwingine zaidi ya sauti ya Bwana wetu YESU, ikimwambia “Panda hata huku nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo “. Unaona hapo kabla Yohana hajajua lolote mlango ulimfungukia kwanza mbinguni, ikimaanisha kuwa hakuna mtu yeyote atakayeweza kupokea ufunuo wowote ule wa Roho kama mlango wa mbinguni haujamfungukia,.Kanisa/mtu ni lazima awe wa rohoni kwanza ndipo liweze kuelewa mambo ya mbinguni, vinginevyo halitaweza kuyaona yaliyo juu likitegemea mifumo au mapokeo ya kibinadamu peke yake.

Na tunasoma pia ile sauti ikamwambia “Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi KUWAKO BAADA YA HAYO”. Ikiwa na maana kuwa, yale maono aliyoonyeshwa kwanza, kama tulivyotangulia kusoma huko nyuma, Yohana alivyomwona YESU KRISTO katika ule mwonekano mwingine, mwenye uso kama jua, macho kama miale ya moto, miguu kama ya shaba n.k. alimwona akitembea katika vile vinara saba, pamoja na nyota saba katika mkono wake, n.k. haya yote yalifunga sehemu ya kwanza ya maono…Na sasa hapa anafungua sehemu ya pili ya maono mengine ambayo yatakuwa pia ni msingi wa mambo mengine tutakayokuja kuyaona huko mbeleni yahusuyo mihuri saba, kama tu vile yale maono ya kwanza yalivyokuwa msingi wa kufahamu tabia za makanisa saba. Na ndio maana hapo anasema ” Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo. “..Hivyo ni muhimu kuyazingatia haya maono pia kwasababu tusipoyaelewa hapa mwanzoni basi sehemu zinazofuata za kitabu cha Ufunuo zitakuwa ni ngumu kuelewa,..

Tuliona kila kitu Yohana alichoonyeshwa katika lile ono la kwanza linalohusu mwili, tabia na mwonekano wa Kristo (Ufunuo 1) vilikuwa na maana kubwa katika yale makanisa 7 yaliyofuata (Ufunuo 2&3), Kwamfano ile miguu ya shaba ilikuwa na sehemu yake katika ujumbe wa kanisa husika, kadhalika na yale macho kama mwali wa moto, na ule upanga utokao kinywani mwake, na vile vinara saba na zile nyota saba zilizokuwa mkononi mwake n.k. yote haya tuliona jinsi yalivyokuwa na mahusiano makubwa sana katika kuelezea nyakati saba za kanisa..Vivyo hivyo na hapa pia katika hii sehemu ya pili ya maono, ambayo Yohana aliitwa juu kuonyeshwa mambo mengine tofauti na aliyoyaona hapo kwanza..Tusome;

Ufunuo 4:2 “Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti;

3 na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi.

4 Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu.

5 Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zilikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu.

6 Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma.

7 Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye.

8 Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja.

9 Na hao wenye uhai wanne wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele,

10 ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi, wakisema,

11 Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa”.

Mstari wa pili unasema..Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti;

3 na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi”.

Hapa Yohana anaonyeshwa kiti cha Enzi na “MMOJA” Kumbuka sio watatu, ameketi katika Kiti hicho, na anaonekana pia mithili ya jiwe la yaspi na akiki,. Sasa kumbuka mawe haya kwa wakati wa agano la kale yalikuwa ni mawe yenye uzuri wa kipekee na ya thamani kubwa sana,yalitumiwa na makuhani katika kifuko cha kifuani (Kutoka 28:15), ni mawe 12 yaliyotumika kama Urimu na thimimu na mojawapo ya hayo mawe ndio Yaspi na akiki, Hivyo hapo mawe hayo yanafunua UZURI wa Mungu, na thamani ya Uzuri wake kwetu sisi wanadamu pia Yohana aliona kile kiti kimezungukwa na upinde wa mvua ikifunua rehema na neema za Mungu pamoja na uthabiti wa maagano yake, Kumbuka baada ya Gharika Mungu kwa rehema zake aliuweka ule upinde wa mvua kama Ishara ya kughahiri hasira yake itakapokuja kutokana na maovu ya watu.

Tukiendelea tunaona pia, Yohana alionyeshwa wazee 24 wamekizunguka kile kiti cha Enzi, wamevikwa mavazi meupe na juu ya vichwa vyao walikuwa na mataji ya dhahabu, pamoja na taa 7 mbele ya kile kiti cha enzi ambazo ndio Roho 7 za Mungu, Kadhalika pia alionyeshwa wale wenye uhai wanne wamekizungu kiti cha enzi wote kwa pamoja wakimpa Mungu utukufu

Kwahiyo Mungu alikuwa anamuonyesha Yohana, mahali kiti chake cha enzi kilipo,kwamba ni lazima kiwe kimezungukwa na wale wazee 24, pili kiwe kimezungukwa pia na wale wenye uhai wanne Na tatu kiwe na Taa saba mbele yake…Hapo kiti cha enzi cha Mungu kimekamilika..hakuonyeshwa kama kimezungukwa na miji au makasri na magorofa ya dhahabu hapana.

Sasa huyu aliyeketi katika kiti cha enzi ni nani?

Kwa maelezo yake marefu tutakuja kumuona vizuri katika sura inayofuata ya tano.

Lakini sasa tuwatazame wale wazee 24 ni akina nani?.

Kwanza ni vizuri kufahamu mbinguni hakuna wazee 24, walioketi kando kando ya Mungu hapana, kumbuka yale ni maono, na wale wazee 24 ni ROHO 24 za Mungu zinazotengeneza ufalme wake katikati ya wanadamu, na ndio maana zimechukua taswira ya mwanadamu. Sasa hizo roho 24 ziliachiwa ulimwenguni kulitengeneza taifa la Mungu katikati ya wanadamu,.Na tunafahamu kuwa ufalme wa Mungu (KANISA) umeundwa na mataifa mawili,nayo ni Wayahudi na Wakristo.

Hivyo mwanzo kabisa Bwana alipoanza kuunda ufalme wake alianza na taifa la mwilini (yaani Israeli), na tunajua taifa la Israeli limegawanyika katika makabila 12, Mungu aliruhusu hivyo makusudi ili kulitengeneza taifa lake. Hivyo Bwana aliachia hizi roho 12 za kwanza kukaa juu ya kila kabisa ili kulijenga taifa la Israeli ambalo ni sehemu moja ya ufalme wake. Ndipo hizi roho zikaanzia kwa wana 12 wa Yakobo na kuendelea.

Lakini baadaye Mungu alipokusudia kuunda sehemu ya pili ya ufalme wake, ndipo akawajia watu wa mataifa (sisi), hivyo kama tu alivyoanza na misingi 12 katika taifa la Israeli kadhalika na huku pia alianza na misingi 12, kujenga sehemu ya pili ya ufalme wake, hivyo akaachia Roho nyingine 12 zilizokuja kukaa juu ya wale mitume 12 wa Bwana Yesu. 

Wefeso 2: 20 ” Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni”.

Ile injili tuliyoipokea sisi kwa mikono ya mitume wa Bwana ndio imekuwa chachu mpaka leo hii ukristo umeenea duniani kote, Hizo ndio zile Roho 12 nyingine zilizoifanya hiyo kazi, kwahiyo kwa ujumla watakatifu wote wa agano la kale na wa agano jipya ndio wanaokizunguka kiti cha enzi cha Mungu katika roho, ndio wale wazee 24…Na ndio maana utaona wamevikwa mavazi meupe kuashiria usafi na weupe wa watakatifu na mataji kuashiria mamlaka ya kifalme kwa ushindi waupatao kutoka kwa yule adui.

Kadhalika na wale wenye uhai wanne, ni Roho nne za Mungu zinazowakilishwa na tabia za wale wanyama wanne. Utaona pia walikuwa wamejaa macho mbele na nyuma, ikiashiria kuwa wapo kwa kazi ya ulinzi, wanaona vitu vitakavyokuja kabla hata havijawasili, wanaona mambo yaliyopita na yanayokuja.

Kwamfano mwenye uhai wa kwanza alionekana akiwa na mfano wa simba, inamaanisha kuwa ni Roho ya Mungu iliyokuwa ikililinda (Kanisa la Mungu), kwa wakati husikia ikijifunua kama tabia ya Simba. Tunajua simba siku zote sio mwoga, ni jasiri, hivyo tutakuja kuona huko mbeleni ni wakati gani hii Roho ilijidhihirisha hivyo katikati ya watu wa Mungu.Kadhalika na yule mwenye uso kama wa ndama, na yule mwenye uso mfano wa Tai arukaye n.k. wote hawa wanabeba tabia fulani inayoendana na maumbile yao..hizi roho zimechukua mfano wa malaika zina mabawa na kupaa tofauti na wale wazee 24, zenyewe zilikuja kwa mfano wa wanadamu,..

Kadhalika tunaona pia Taa saba za moto mbele ya kile kiti cha enzi. Hizo ni roho saba za Mungu, ambazo tulishakwisha kuziona zenyewe kwenye sura zilizotangulia zikitembea katika yale makanisa saba ya Mungu.

Kwahiyo kwa ujumla katikati ya vitu hivyo vyote ndipo kiti cha enzi cha Mungu kilipo, yaani ndani ya kanisa lake (Israeli na Mataifa), linaloongozwa na hizo Roho saba, na Roho za wenye uhai wanne, Hivyo ni muhimu kufahamu ni roho gani inayoliongoza kanisa ulilopo sasa, kadhalika na ni Roho ya mwenye uhai yupi aliye juu yako na juu ya wakati wa kanisa ulilopo vinginevyo hutaweza kukiona kiti cha enzi cha Mungu au kumshinda shetani kwa namna yoyote ile katika wakati huu unaoishi.

Kumbuka shetani naye anacho kiti chake cha enzi, na chenyewe pia kimezungukwa na roho chafu nne, ndio wale wapanda farasi wanne ambao tutakuja kuwaona katika sura ya 6, na anazo roho nyingine chafu saba, ndizo zilizokuwa zinatembea pia katika makanisa saba ya Mungu kulichafua kanisa la Mungu na kupoteza watu Ndio zile Bwana Yesu alizozizungumzia katika..

Mathayo 12: 43 ” Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate.

44 Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa.

45 Mara huenda, akachukua pamoja naye PEPO WENGINE SABA walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa KIZAZI HIKI kilicho kibaya. “

Unaona hapo katika ile siku ya Pentekoste Bwana alilijenga tena kanisa kwa kulitakasa kwa Roho wake, kwa wakati ule Kanisa lilikuwa kamilifu lakini mitume wa kweli walipoondoka,mitume wa uongo wakanyanyuka kuunda misingi ya kanisa lingine la uongo na kuanza kuchanganya kweli ya Mungu na mafundisho ya kibinadamu, hivyo ikapelekea ile roho (pepo) ambalo Bwana Yesu alilitoa pale Kalvari kurudi tena katika kanisa la Mungu kwa taswira mbaya zaidi, lilirudi katika mwishoni wa kanisa la kwanza, kadhalika na katika kanisa la pili likaongezeka lingine la pili, na katika kanisa la tatu, na la nne, mpaka kanisa la saba, mapepo yote saba maovu yakalivaa kanisa, na ndio maana hali ya kanisa hili la Laodikia ni mbaya kuliko makanisa yote yaliyotangulia…Lakini siku zote mbegu halisi haiwezi changanyikana na ya uharibifu Bwana alishalianza kuwatenga watu wake na kanisa hilo la uharibifu tangu zamani.

Hivyo ni muhimu kufahamu pia kiti cha enzi cha shetani kilipo, kwasababu yeye naye anachokiti chake cha enzi Soma Ufunuo 2: 13 ” Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; ….” Unaona hapo?

Ikiwa na maana kuwa hata yeye naye analo kanisa lake aliloliunda ndipo aketipo yeye. Na kanisa hilo ni Kanisa Katoliki. Hilo ndilo linaloongozwa na (mapepo) yale saba maovu, na wale wapanda farasi wanne, ambao kwa ujumla roho hizi zilishughulika sana kupambana na uzao wa Mungu na kuuharibu kama tutakavyokuja kuona katika sura ya sita.

Kama vile Mungu alivyotwaa mwili na kuishi katikati yetu na kufanyika mfalme wa kanisa la Mungu, kadhalika shetani naye amemtia mtu mafuta akae badala yake katika kiti chake cha enzi, na si mwingine zaidi ya mpinga-kristo (PAPA atakayekuja) aliye kichwa cha kanisa hilo la uongo.

Hivyo ndugu jiulize je! umeketi katika kiti cha enzi cha Mungu au cha shetani??..Kama unadai umeketi katika kiti cha enzi cha Mungu, na bado haupo katika misingi ya mafundisho ya mitume 12(BIBLIA), na haufahamu kanisa unaloishi!, na hauifahamu Roho inayoliongoza kanisa lako? basi ni dhahiri kabisa kwamba unaketi katika kiti cha enzi cha shetani pasipo hata wewe kujijua, kwasababu ile roho ya uhai yenye macho mbele na nyuma ambayo ingepaswa ikuongoze haipo juu yako ambayo ingekupa wewe uhai na macho ya kuweza kuona mambo ya mbele na ya nyuma na kukuwezesha wewe kuzijua fumbo za shetani imeondoka. Na pia kumbuka viti vyote vya enzi (cha MUNGU na cha shetani) vinaundwa hapa hapa duniani..Hivyo jitathimini maisha yako. je! umeoshwa kwa damu ya YESU KRISTO na kujazwa Roho Mtakatifu? Huyo tu ndiye atakayekuongoza katika kweli yote na sio dini au dhehebu. Mkumbuke muumba wako siku za ujana wako kabla haijakaribia miaka utakayosema sina furaha katika hiyo (Mhubiri 12).

Ubarikiwe. Kwa Mwendelezo >>> Ufunuo: Mlango wa 5

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.


Mada Zinazoendana..

SEHEMU ISIYO NA MAJI.

MKUU WA GIZA.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
5 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Baba sam
Baba sam
2 years ago

Asante Sana kwa mafundisho mazuri

Heriamani Norbert
Heriamani Norbert
2 years ago

Nimefurahi sana kupata mafundisho haya, nitazidi kujifunza nawe, Mungu ahimidiwe sana

Kifaru Malale
Kifaru Malale
3 years ago

amina mtumishi wa Mungu, asante kwa mafunuo haya ya kuhusu kiti cha enzi cha Mungu pamoja na jinsi shetani anavyojitahid kuiga vya Mingu