UFUNUO: Mlango wa 3 part 3

UFUNUO: Mlango wa 3 part 3

Sehemu ya tatu:

Jina kuu la Bwana wetu YESU KRISTO litukuzwe. Karibu katika mwendelezo wa uchambuzi wa kitabu cha Ufunuo, Leo tukimalizia sehemu ya mwisho ya sura hii ya tatu. Ambapo tutaona kanisa lile la LAODIKIA. Tulishatazama makanisa mengine 6 yaliyotangulia pamoja na wajumbe wao, na jumbe walizopewa kutoka kwa Bwana.Kama haujayapitia unaweza ukayapitia kwanza ili tuende pamoja katika kanisa hili la mwisho, Tunasoma…

Ufunuo 3: 14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu”.

Kama tulivyotangulia kujifunza tunaona ule utambulisho wa kwanza Bwana anaoutoa kwa kanisa, huwa una uhusiano mkubwa sana na ujumbe wenyewe wa kanisa husika. Hapa Bwana anasema ” yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu “. Na hasemi “yeye aliye na ule ufunguo wa Daudi, au yeye mwenye uso ung’aao kama jua. au yeye aliyekuwa amekufa kisha akawa hai” kama alivyokuwa anasema katika makanisa yaliyotangulia, hapana bali anasema “anenaye yeye aliye Amina, SHAHIDI MWAMINIFU na wa Kweli”. Ikiashiria kuwa katika kanisa hili anatazamia kuona UAMINIFU, kama aliokuwa nao yeye tangu mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

Kwa ufupi kanisa hili la Laodikia lilianza kati ya kipindi cha mwaka 1906 WK na litaisha na siku ya ujio wa Bwana mara ya pili (yaani Unyakuo). Na mjumbe wa kanisa hili ni WILLIAM BRANHAM. Na tafsiri ya neno LAODIKIA ni “HAKI ZA WATU”. Katika Asia ndogo ambapo haya makanisa 7 yalikuwepo, Mji wa Laodikia ndio uliokuwa umeendelea kuliko miji mingine, kama efeso, smirna, pergamo n.k. Ni mji uliokuwa tajiri kuliko yote, ulikuwa upo juu kibiashara na kiuchumi na kiusomi, hivyo ikapelekea na watakatifu waliokuwa katika mji huo kuwa na hadhi ya kitofauti na watakatifu waliokuwa katika miji mingine. Na ndio maana hatushangai kwanini Bwana Yesu kutoa ujumbe ufuatao;

“15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi”.

Unaona hapo? kutokana na mafanikio makubwa yaliyokuwepo katika ya hao watu, Ikawafanya watakatifu waridhike na kupoa sana kiroho pasipo hata wao kujitambua. Watu wa mji ule (wasiomjua Mungu) wakaanza kuweka mambo kwenye mizani, kila kitu nusu kwa nusu, kama tafsiri ya jina lake lilivyo “HAKI ZA WATU” Mambo kama haki sawa, yakazaliwa wanaume kwa wanawake,

Sasa hii roho ya haki sawa nayo ikapenyeza mpaka kwenye kanisa la Mungu.. Kwamba kwa Mungu kuna haki sawa, nusu kwa nusu, Mungu kidogo na Ulimwengu kidogo, Unasali kidogo unafanya anasa kidogo, unakuwa mtakatifu leo kesho unaendelea na mambo mengine, unatenda mema leo, baadaye unakula rushwa, leo unakuwa wa rohoni kesho wa mwilini, hivyo hivyo leo moto kesho baridi (Yaani vuguvugu). Na kibaya kibaya zaidi kutokana na utajiri wake wa nje waliokuwa nao kanisa hili lilikuwa Laodikia, shetani akalipiga UPOFU mkubwa juu yake, likawa halijitambui tena kama linakwenda mbali na ukweli. Jaribu kutengeneza picha upo uchi, na hujitambui kama upo hivyo..Hiyo ni hatari kubwa sana.

Kwa kuwa Bwana anaona mbele alilifanya kanisa hilo kuwa unabii wa watu wa nyakati fulani itakayokuja miaka mingi huko mbele nao sio wengine zaidi ya sisi watu wa kizazi hichi tunachoishi leo ambacho kilianza tangu kipindi cha miaka ya 1906, Hivyo ndugu ni muhimu sana kufahamu kuwa tunaishi katika kanisa linalofanana na lile la Laodikia.

Kama vile mji ule ulivyokuwa tajiri kuliko miji mingine yote sita, kadhalika na dunia ya sasa tunayoishi ndio dunia iliyoendelea na iliyotajirika kuliko nyakati nyingine zote zilitangulia, kiuchumi, kiteknolojia na kielimu n.k.. Kiasi kwamba dunia leo hii ni kama kijiji, utandawazi umefikia viwango vya juu sana. Sayansi imefika hatua ya kwamba mwanadamu anaweza akaenda mwezini, mambo mengi sana yamevumbuliwa kuanzia karne ya 20, yaani kuanzia mwaka 1901 na kuendelea uvumbuzi wa mambo mengi ulitokea tukianza kueleza moja moja hatutamaliza. Mambo ambayo hayakuonekana katika karne zote zilizotangulia. Hii ni kuonyesha kwamba dunia ya sasa tunayoishi inafanana kabisa na mji ule wa LAODIKIA.

Kadhalika “haki za binadamu”, agenda za haki sawa kati ya wanawake na wanaume zilizuka katika karne hii hii ya 20, kwamba chochote mwanaume anachoweza kufanya hata mwanamke anaweza akafanya, hata mavazi mwanaume anayovaa hata mwanamke pia anaweza akayavaa, haki za watu kuoa mtu anayemtaka aidha mwanaume kwa mwanaume, au mwanamke kwa mwanamke haina shida n.k. mambo ambayo hayakuonekana katika karne zote za nyuma zilizotangulia.

Hivyo hiyo roho iliyokaa katika ulimwengu ikajiambukiza tena katika kanisa la KRISTO kama ilivyokuwa kwa wakati wa Laodikia. Kwa kuwa tunaishi katika kipindi cha mafanikio makubwa ya kielimu, kiuchumi na kiteknolojia, watakatifu wa wakati huu wakaanza kuendana pia na watu wa ulimwengu huu, na wao pia wakaanza kuiga mambo ya ulimwengu na kuyaleta katika kanisa la Mungu.

Kutokana na kwamba kuwa na utajiri wa vitu vingine vya nje, kama makanisa makubwa, vitendea kazi vya kisasa vya ibada kama vyombo vya muziki, vipaza sauti vikubwa vya kuwafikia watu wengi mambo ambayo hayakuwepo katika makanisa ya nyuma, vitu kama televisheni, radio na internet vimekuwa nyenzo rahisi za kuwafikia watu, kadhalika vyombo vya kisasa vya usafiri kama ndege, magari n.k. tofuati na hapo zamani watakatifu walikuwa wakitumia miguu, na punda kwenda kuhubiri injili, Ikawasababishia shabaha yao ihame kutoka katika mambo ya rohoni zaidi na kuhamia kwenye mambo ya mwilini. n.k. watakatifu wakaanza kujiona kwa vitu walivyonavyo Mungu anapendezwa nao,

Hivyo nguvu ile ile inayoiendesha dunia, ndio hiyo hiyo inayoiendesha kanisa, mambo yale yaliyotukuka katika dunia ndiyo yanayotukuka ndani ya kanisa la leo, Badala utakatifu utukuzwe ndani ya kanisa, inatukuzwa elimu, kwamba kipimo cha kuwa mchungaji au umekubaliwa na Mungu ni kiwango cha elimu na sio utakatifu, kadhalika utajiri wa Fedha imetukuzwa zaidi kuliko utajiri wa Rohoni, kiasi kwamba kipimo cha mtu kubarikiwa na Mungu sio kukua kiroho hapana bali kuwa na fedha nyingi..Injili inayoweza kumfaa mtu kwasasa ni injili ya mafanikio na sio injili ya toba.

Kadhalika vyeo vilivyotukuka duniani vinavyotumika kuongozea ustaarabu wa kidunia vimepewa heshima kubwa zaidi kanisani kuliko vyeo Mungu alivyovikusudia viwepo kwa uongozo wa kanisa. Kiasi kwamba ili uonekane umekubaliwa na Mungu ni lazima Uwe Raisi wa dhehebu fulani, M/kiti, Katibu/ Papa/ Mkurugenzi, Dokta, Profesa n.k. na sio Karama fulani ya rohoni kama unjilisti, uchungaji, ualimu, mitume na manabii, au karama nyingine za Roho kama miujiza,lugha, unabii uponyaji n.k. zimewekwa nyuma na hazina nafasi yoyote katika kanisa la sasa.

Dunia tunayoishi leo hii ni ya “HAKI ZA KIBINADAMU”, kadhalika na kanisa nalo limechukua hizo tabia, kwamba hata mavazi anayovaa mwanaume hata mwanamke wa kikristo anaweza kuyavaa, kwamba karama za uongozi ambazo Mungu aliziweka kwa wanaume tu, kulingana na (1Timotheo 2:12) kama vile uchungaji, ualimu na utume, hata mwanamke anaweza akazifanya; Imefikia hatua kwamba ndoa za jinsia moja zinazofungishwa na watu wa ulimwengu zinafungishwa pia Kanisani..Na bado watu hao wanajiita wakristo na kibaya zaidi shetani amewapiga upofu hawajijui kwamba wapo uchi, vipofu, maskini, na wanyonge….Ni uvuguvugu wa hali ya juu sana. Kristo ametupwa nje.

Kumbuka katika kila nyakati kulikuwa na mjumbe wa kanisa hilo ambalo Mungu alimnyanyua kutoa nuru ya wakati huo, Tuliona katika kanisa la Tano Bwana alimnyanyua Martin Luther na wengine kama wakina Calvin na Zingwli, kadhalika katika nyakati ya sita Bwana alimnyanyua John Wesley na wenzake. Vivyo hivyo na katika hili kanisa la mwisho Bwana alimnyanyua mjumbe wake WILLIAM BRANHAM na ujumbe wa kuwarudisha watu katika NENO na watoke katika hali ya uvuguvugu iliyopo sasa katikati ya madhehebu na kutoka katika mifumo ya yule mwanamke kahaba (Kanisa Katoliki) na pia Bwana alimpa ujumbe wa kutangaza kuja kwa pili kwa Kristo.

William Branham ni nani?.

William Branham alizaliwa huko Kentucky, Marekani mwaka 1909alizaliwa katika familia ya kimaskini sana, baba yake alikuwa ni mtengenezaji wa pombe, hivyo aliishi katika mazingira ya kushawishika na ulevi, alipofikisha umri wa miaka 7 anasema siku moja wakati anatoka kuteka maji kisimani alisikia sauti juu ya mti ikimwambia, “Usikae unywe pombe, wala kuvuta sigara,kwani kuna kazi ya yeye kufanya utakapokuwa mtu mzima”, aliogopa sana lakini maneno hayo aliyaweka moyoni, kwani aliogopa kuwaeleza watu maono aliyokuwa anayaona kwasababu wengi miongoni mwa wachungaji walikuwa wakimwambia hayo ni maono kutoka kwa shetani, lakini ilifika kipindi akampa Kristo maisha yake, na kukata shauri kumtumikia Mungu, ndipo Bwana akaanza kumtumia kwa namna ya kipekee, Siku moja wakati anabatiza umati mkubwa wa watu katika mto mmoja huko Marekani unaitwa Ohio, alipokuwa anambatiza mtu kama wa 17, nyota kubwa ilishuka juu yake akiwa pale mtoni, watu wote wakaishuhudia na ndipo akasikia sauti ikimwambia “Kama vile Yohana mbatizaji alivyotumwa kutangaza kuja kwa kwanza kwa Kristo, vivyo hivyo ujumbe wako utatangaza kuja kwa pili kwa Kristo”. Habari ya tukio hilo ilisambaa sana na kuchapishwa katika magezeti na vyombo vya habari vya Marekani.

Na alipofikisha umri wa miaka 37, siku moja alipokuwa anasali usiku malaika wa Bwana alimjia na miongoni mwa maneno aliyoambiwa ni; “Kama akiwa mwaminifu atakapoomba hakuna kitachoweza kusimama mbele yake hata kansa, aliambiwa pia atawaombea wafalme na ujumbe wake utafika duniani kote,” . Hivyo kuanzia huo wakati Ishara na miujiza ya kupita kawaida viliambatana naye, mambo ambayo hapo nyuma yalikuwa hayaonekani, karama za upambanuzi wa roho ziliambata naye siku zote za huduma yake, siku moja wakati anahubiri Mungu kutaka kuithibitisha huduma yake NGUZO YA MOTO ambayo ilikuwa ikimfuata tangu kuzaliwa kwake, ilitokea hadharani na kukaa juu yake, mamia ya watu waliokuwa pale waliiona, na ikapigwa picha, hiyo ilikuwa ni mwaka 1950, Picha hiyo upesi ilipelekwa kwa George J. Lacy, Mchunguzi Mweledi wa Hati Zinazoshukiwa wa F.B.I. ya Marekani, ambaye aliihakiki picha hiyo kwa maoni yake ya kitaalamu. Hati rasmi iliyotolewa na Bw. Lacy kuhakiki kuwa ile ilikuwa ni picha ya kwanza ya kimiujiza iliyothibitishwa kisayansi. Hii ilikuwa ni mapema zaidi kabla ya kompyuta na kamera za tarakimu, wala haingeweza kuelezewa kwa njia zozote zinazojulikana na sayansi, mbali na kwamba kulikuwa na Nuru halisi juu ya kichwa cha William Branham. Leo hii picha hiyo hiyo inaweza kuonekana kwenye Maktaba ya Bunge la Marekani, katika makao makuu ya taifa, Washington DC. (Tazama picha chini).

Kwahiyo historia ya maisha na huduma ya William Branham ni ndefu kidogo hatuwezi kuielezea yote hapa ila kama utahitaji utaipata mwisho wa ukurasa huu.

Hivyo ishara zote na miujiza Mungu aliyomjalia William Branham viliambata na ujumbe, Na ujumbe wenyewe ulikuwa ni Kuwarudisha watu kwenye misingi ya Neno la Mungu, Kuwarejesha watu katika Imani ya kanisa la mwanzo, na kwamba watu wa Mungu watoke katika mifumo ya dini na madhehebu ambayo Mungu ameikataa, na kujiandaa kwa kuja kwa pili kwa Kristo, Kadhalika Bwana aliwanyanyua na wengine kama ORAL ROBERT, TL OSBORN, na BILL GRANHAM na wengine baadhi. Wote hawa ni ili kuangaza nuru ya Mungu katika kanisa la mwisho tunaloishi sasa. Hivyo uamsho wa Roho ulikuwa ni mkubwa sana katikati ya karne ya ishirini, tofuati na tunavyoona sasa hivi, kuzuka kwa wimbi kubwa la manabii wa uongo na waalimu wa uongo, na miujiza bandia kama tunavyoona sasa.

Sasa turudi katika kanisa hili la LAODIKIA Bwana anasema;

“15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi”.

Unaona hapo, kanisa tunaloishi ni vuguvugu, kwa wingi wa vitu tulivyonavyo tumejikinai, Na Bwana anasema atatupika kama tusipotubu.. Bwana anasema..

“18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami”.

Ujumbe huo unajieleza wenyewe kwamba ni wakati wa kurudi na kufahamu ujumbe wako wa saa wa nyakati unayoishi.. unaweza ukajiona ni moto kumbe ni baridi kwasababu umeshindwa kufahamu ni nyakati gani unaishi. na ujumbe wa wakati huu ni kurudi kwenye misingi ya NENO LA MUNGU ambayo tumeiacha ili tuwe moto na sio vuguvugu, tuache kuchanganya neno la Mungu mapokeo ya kidini, tuache kuchanganya Neno la Mungu na mambo ya ulimwengu huu kama kanisa la Laodikia lilivyokuwa (Kwani ni sawa na kufanya uasherati wa kiroho)..Leo hii unafanya ibada, kesho upo disco, jumapili unavaa vizuri, jumatatu unavaa vimini, leo unakuwa mwaminifu kesho unakula rushwa, leo unazungumza ukweli kesho unadanganya na kutukana, n.k.huko ndio kuwa vuguvugu, au KUTOKUWA MWAMINIFU na Kristo katika kanisa hili anataka kuona UAMINIFU kama yeye alivyojitambulisha hapo mwanzo kuwa YEYE NI MWAMINIFU TANGU MWANZO.

Na Bwana anamalizia kwa kusema..

“21 Yeye ashindaye, nitampa KUKETI PAMOJA NAMI KATIKA KITI CHANGU CHA ENZI, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.

22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”.

Unaona hapo? Kanisa hili ndilo lililopewa thawabu kubwa kuliko makanisa yote yaliyotangulia, kwamba kwa yeye atakayeshinda kwa kuwa mwaminifu kama yeye alivyokuwa atapewa nafasi ya kuketi pamoja naye katika kiti chake cha Enzi” Je! hupendi thawabu kama hiyo?..Wote tunaipenda hivyo tukizijua thawabu hizi njema Mungu alizotuandalia huko, tutaishi maisha ya kujilinda sana asije mwovu akalitwaa taji letu katika nyakati hizi za hatari.. Kumbuka pia hakutakuwa na kanisa linguine zaidi ya hili. Hatua iliyobaki ni unyakuo tu.

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Huu ndio mwisho wa ujumbe Bwana alioutoa kwa yale makanisa saba. Kwa neema za Mungu tutazidi kuzitazama sura zinazoendelea. Kwa Mwendelezo >>>Ufunuo: Mlango wa 4

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.


Mada Zinazoendana:

WILLIAM MARRION BRANHAM NI NANI?

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
8 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Mtasingwa Faraja
Mtasingwa Faraja
1 year ago

Kweli kabisa

Kifaru Malale
Kifaru Malale
3 years ago

unalisema ukweli, yani madhehebu ,mengi siku izi. kipimo cha kuonesha kukubalika na Mungu ni mafanikio yako kidunia, Mungu akubaliki kwa maziwa haya yasiogoshiwa

Anonymous
Anonymous
3 years ago

Yaani Mungu akubariki sana sana kwa maarifa haya ya Neno la Mungu, kwa kufungua mafumbo haya makubwa

Rogath
Rogath
4 years ago

Asante kwa mafundisho haya mungu akubariki