UFUNUO: Mlango wa 5

UFUNUO: Mlango wa 5

Shalom! Karibu katika mwendelezo mfupi wa uchambuzi wa kitabu cha ufunuo, kwa neema za Mungu tulishatazama sura zilizotangulia tukaona ile sehemu ya kwanza ya maono Yohana aliyoonyeshwa katika sura ya kwanza, ilihusu sana sana ujumbe wa yale makanisa saba ambayo tunayasoma katika ile sura ya 3 na ya 4, hivyo kama haujafahamu bado ufunuo wa yale makanisa 7 katika wakati wetu tunaoishi sasa, ni vema ukapitia kwanza kule, ili tuende pamoja katika sura hii.

Katika hii sura ya tano, tunaona Yohana akionyeshwa mfululizo wa maono mengine tofauti na yale ya kwanza ambayo alionyeshwa katika sura ile ya kwanza, sehemu hii ya pili ya maono haya yalianzia katika ile sura ya nne, yakaendelea mpaka sura ya 5, ambapo tunaona Yohana alichukuliwa juu mbinguni na kuonyeshwa kiti cha enzi cha Mungu katika roho, na wale wazee 24 wakiwa wamekizunguka kiti cha enzi, na wale wenye uhai 4, kadhalika na zile Taa saba za moto ambazo ndio Roho 7 za Mungu, na mbele ya kiti cha enzi kulikuwa pia na bahari ya kioo kama bilauri ikifunua weupe na usafi wa watakatifu, na bahari ikifunua wingi wa watakatifu, tutakuja kuona vizuri katika ile sura ya 15 inaonekana bahari nyingine ya kioo isipokuwa hiyo imechanganyikana na moto, ikifunua watakatifu waliosafishwa kwa moto katika dhiki kuu,.

Tukirudi kwenye sura ya tano, tunaona mkazo umewekwa kwa yule aliyeketi katika kiti cha enzi, na kile alichokuwa amekishika katika mkono wake wa kuume..Tusome hapo.

Ufunuo 5: 1 “Kisha nikaona katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi kitabu kilichoandikwa ndani na nyuma, kimetiwa muhuri saba”.

Kumbuka hapo biblia inasema “yeye” ikimaanisha ni mmoja ambaye alishazungumziwa katika sura ya 4:2, ameshika KITABU kilichoandikwa NDANI na NYUMA. Na huyu si mwingine zaidi ya Elohim katika ofisi yake ya ubaba, ambaye yeye kabla ya kuumba ulimwengu vitu vyote vilikuwa ndani yake, yeye ndiye mjenzi wa vitu vyote vilivyokuwepo na vitakavyokuwepo, asiyekuwa na mwanzo wala asiyekuwa na mwisho, na kama yeye ndiye aliyebuni maisha na dunia na wanadamu, na malaika na viumbe vyote kama ni hivyo basi ni dhahiri kuwa yeye ndiye mwenye siri na misingi ya vitu vyote. Kuanzia mwanzo wao mpaka mwisho wao, Na hakuna yeyote atakayeweza kuvumbua jambo lolote kwa uweza wake au nguvu zake mwenyewe isipokuwa kwanza kafunuliwa na Mungu (Elohimu).

Kama vile tunafahamu leo hii mtu akibudi chombo chake labda tusema ni gari, siku akitaka kwenda kumpa mtu mwingine labda kumuuzia au kumrithisha hawezi kumpa hivi hivi tu bila kuambatanisha na mwongozo (MANUAL) fulani, ili kumsaidia yule anayepokea kuweza kukifahamu na kukitumia chombo hicho kwa ufasaha zaidi sawa sawa na jinsi kilivyokusudiwa kiwe. Kwa kupitia mwongozo ule atafahamu uwezo wa usafiri wa chombo chake, atafahamu wakati unaopaswa kukifanyia marekebisho, atafahamu aina ya nishati itakachotumia, atafahamu tahadhari za kuchukua wakati wa matumizi ili kisimletee madhara yoyote kwake bali faida n.k..

Vivyo hivyo na Mungu (Elohimu) kama muumbaji wa kila kitu alipoiumba dunia kwa hekima zake nyingi, na kuamua kumpa mwanadamu hakumpa pasipo mwongozo, wa jinsi ya kuindesha hii dunia na kuitunza ili iweze kumuhifadhi mtu milele asipatikane na madhara yoyote na aishi kwa amani na furaha siku zote alizowekewa mbele yake, Hivyo huu mwongozo (MANUAL) alianza kupewa mtu wa kwanza Adamu pale Edeni, Mungu alianza taratibu taratifu kumpa maarifa na kanuni za kuishi na kuitawala dunia milele.

Lakini tunaona Adamu mwanzoni kabisa mwa maagizo yale aliharibu mpango mzima, kwa kutokutii na kufuata yale aliyoambiwa ikapelekea ule mwongozo kutokuwa na maana tena mbele yake (ukafichwa) kwasababu mambo yote ameshayaharibu tangu mwanzo.

Kwamfano wewe unalo gari lako, umelibuni kwa utashi mwingi, na umekusudia kumrithisha mwanao liwe lake moja kwa moja, lakini wakati unaanza tu kumwonyesha gari kwa nje, matairi, vioo, milango, site mirrors n.k. yeye unashangaa tayari kashafungua mlango na kupiga ufunguo kasha kukanyaga mafuta na kuanza kuondoka,kumbuka na hapo hajawahi kuendesha gari hata siku moja, ni mara yake ya kwanza, ila amesikia tu! Ukishawasha gari weka “D” kisha kanyaga mafuta gari litaenda..wewe unadhani ni jambo gani litatokea hapo kwa mtu kama huyo? Ni dhahiri kuwa atasababisha ajali?? Na mwisho wake ni mauti??. Hicho Ndicho kilichomtokea Adamu, pale Bwana alipomwonyesha kuwa hii dunia ni urithi wake, hakusubiria ule mwongozo ambao alikuwa anapewa taratibu taratibu, siku baada ya siku na Baba yake…yeye alikimbilia moja kwa moja kusikiliza mwongozo bandia wa Shetani, wa jinsi ya kuiendesha hii dunia kama Mungu anavyoiendesha, Biblia inasema..

Mwanzo 3:4 “Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa,
5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya”.

Unaona hapo ni kweli ulikuwa ni mpango wa Mungu Adamu kufahamu mema na mabaya, lakini ilikuwa sio kwa wakati ule, bali Mungu alikusudia kumpa mwongozo kidogo kidogo, lakini yeye kwa maneno machache tu ya shetani alidhana kuwa angeweza kuiendesha dunia kama Mungu, matokeo yake maarifa yale yalimsababishia KIFO. Hivyo Mungu asingeweza kuendelea kumpa mwongozo ule mtu ambaye yupo katika hali ya mauti. Kuanzia hapo Mungu AKAUFUNGA ule mwongozo kwa MIHURI asiweze mtu yeyote kuifungua mpaka atakapoonekana anayestahili.

Kwahiyo Huu mwongozo ni kitabu cha MAARIFA ya Mungu juu ya mwanadamu na urithi aliopewa, kimebeba siri zote za uumbaji wa ulimwengu, misingi yake ilipo, namna ya kuifanya idumu milele, namna ya kuifanya iwe na amani,furaha, namna ya kuifanya mwanadamu asiishi kwa taabu, shida, maumivu, kero, adha n.k..kimebeba siri zote zinazohusiana na sayari na magimba mengine huko angani, na mambo mengine mengi sana ambayo hata sasa hivi hatuyajui..Hayo yote yapo ndani ya hicho kitabu na ndio hicho tunakuja kukiona tena katika Ufunuo sura ya 5 kimeshikwa na yeye (ELOHIMU) mwenyewe katika kiti chake cha enzi kikiwa kimefungwa kwa mihuri saba huku kikiwa kimeandikwa NDANI na NYUMA.

Tukiendelea kusoma.

Ufunuo 5: 2 “Nikaona malaika mwenye nguvu akihubiri kwa sauti kuu, N’nani astahiliye kukifungua kitabu, na kuzivunja muhuri zake?

3 Wala hapakuwa na mtu mbinguni, wala juu ya nchi, wala chini ya nchi, aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama.

4 Nami nikalia sana kwa kuwa hapakuonekana mtu astahiliye kukifungua hicho kitabu, wala kukitazama.

5 Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba.

6 Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, ambazo ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote.

7 Akaja, akakitwaa kile kitabu katika mkono wa kuume wake yeye aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi”.

Unaona hapo? Hakuonekana mtu aliyestahili kukifungua hicho kitabu wala kukitazama, mara baada ya Adamu kuasi tu,tangu huo wakati hakuonekana mtu yeyote aliyestahili, na sio tu kikifungua bali hata kukitazama,! Hivyo Yohana alivyoona alilia sana, kuona kuwa dunia itaendelea kubaki vile vile katika hali yake ya ubovu, kama ilivyokuwa zamani, majanga, magonjwa, vifo, dhiki, taabu, shida, vitaendelea kuwepo, dunia itaendelea kuyumba yumba kama mlevi hivyo hivyo mpaka itakapofikia uharibifu wake.

Jaribu kifikiria hata ingekuwa ni wewe katika hali kama ile kuona hata malaika wa mbinguni hakuna aliyeonekana amestahili,..hakika ungevunjika moyo sana na kulia, ungeona hakuna tumaini tena, maisha hayana maana tena, …Lakini ashukuriwe Mungu wa mbingu na nchi, kwani alionekana MMOJA aliyestahili kukifungua kile kitabu na kuvunja mihuri yake naye si mwingine zaidi ya Simba wa Yuda, Bwana wa Mabwana, Mfalme wa Wafalme, YESU KRISTO Bwana wetu, sifa na utukufu vina yeye milele na milele Amina..yeye pekee ndiye aliyestahili kukitwaa kile kitabu, hivyo basi tumaini la marejesho lipo! Limeinuka tena! Haleluya!!.

Na ndio maana ilimpasa aje duniani kwanza ajaribiwe kama sisi tulivyojaribiwa, aishi kama sisi tulivyoishi, bila kutenda dhambi yoyote, afe msalabani bila shutumu lolote kisha aongezee kuwakomboa wanadamu kwa damu yake, ili siku ile asiwe peke yake bali pamoja na ndugu zake (yaani mimi na wewe) na ndipo apande mbinguni akajionyeshe mbele za Mungu kuwa amestahili yeye kukitwaa hicho kitabu na kuvunja mihuri yake..Lakini kama asingeyapitia hayo yote kuishi na kufa kwa ajili yetu, kadhalika yeye naye asingestahili hata kikutazama kile kitabu.Lakini alishinda ili sisi nasi tushinde pamoja naye, Utukufu na heshima anastahili yeye peke yake milele na milele amina.

Lakini kumbuka pia usisahau jambo hili Yesu Kristo ni Elohimu mwenyewe katika mwili,( soma 1Timetheo 3:16) na ndio maana utaona pale katikati ya kile kiti cha enzi anatoka mwanakondoo, ambaye ni Yesu Kristo, Ni Elohimu Yule Yule akijidhihirisha katika ofisi ya mwana (Ufunuo 5:6), Na ndio maana tukiendelea, kusoma tunaona viumbe vyote mbinguni na duniani vyote vinatambua kwamba amestahili yeye pekee kukifungua kile kitabu..

Ufunuo 5:8-14“8 Hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo, kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu.

9 Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa,
10 ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.

11 Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu,

12 wakisema kwa sauti kuu, Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka.

13 Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi ya juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele.

14 Na wale wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka, wakasujudu.”

Kumbuka Bwana Yesu alivyokuwa duniani, hakufahamu mambo yote, na ndio maana alisema siku ile hakuna mtu aijuaye, hata mwana bali Baba, lakini alipopaa juu mbinguni, alipewa funguo zote, ikiwemo funguo za mauti na kuzimu, pamoja na mamlaka yote ya mbinguni na duniani, na ukuu, na ufalme,kuteka vipawa na URITHI wote, n.k. mambo haya yote yalikuwa ndani ya kile kitabu cha mwongozo kilichokuwa katika mkono wa Mungu mwenyezi.

Hivyo alipopaa mbinguni ndipo alipokwenda kutwaa kile KITABU, na hapa Yohana anaonyeshwa katika maono siku aliyopokea Kitabu kile, Kumbuka kitabu kile kimeandikwa NDANI na NYUMA,. Ikimaanisha kuna mambo ya nje na ya ndani,..Ya nje! Ndio hayo tutakayoyajua tukiwa hapa duniani, bali ya ndani tutayafahamu vizuri tukifika mbinguni..ndio siku hiyo tutafahamu vizuri maana ya yale maneno Bwana aliyotuambia

Yohana 14: 1 Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.

2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.

3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.

4 Nami niendako mwaijua njia.”
Makao yanayozungumziwa hapo ni miili yetu ya utukufu, urithi wetu wa milele unaokuja.

Ndani ya kile kitabu kumeandikwa urithi wote umuhusuo mwanadamu na mambo anayopaswa kuyafanya ili dunia iwe katika hali ambayo Mungu aliikusudia tangu mwanzo, kuna siri nyingi na maarifa mengi Mungu ameyasitiri ambayo sehemu ya hayo yatakuja kufunuliwa kwa Bibi-arusi wa Kristo pekee! Tukiwa hapa hapa duniani itakuwa ni karibia sana na nyakati kufungwa (karibia na unyakuo), ndio zile ngurumo saba, ambazo hazijarekodiwa mahali popote katika biblia, hizo zitampa Bibi-arusi imani ya kunyakuliwa, na sehemu iliyobaki ya ndani ya kitabu hicho tutaijua tukifika mbinguni mara baada ya kubadilishwa miili yetu,

Kumbuka mbinguni tutaenda kwa kitambo tu! Urithi wetu ni hapa DUNIANI, Mungu ndio aliotupa,.Tutaenda mbinguni kisha tutarudi, na ndio maana maandiko yanasema Kristo atarudi tena, moja ya kusudi la sisi kwenda mbinguni, si tu kufunuliwa uzuri wa kule bali pia kufunuliwa siri za urithi wetu tuliopewa na BABA na mikakati ya kuiunda tena kulingana na ule mwongozo ambao Bwana Yesu aliutwaa katika mkono wa ELOHIMU. Na baada ya hayo Kristo atashuka na watakatifu wake kutoka mbinguni, kuisafisha dunia.(urithi tulioahidiwa na baba)

Ndugu yale mambo yote ambayo tulikuwa hatuna majibu nayo, kwanini hivi?..kwanini vile?..ingekuwa hivi..ingekuwa vile..n.k…yote haya tutapata majibu yake siku ile tukifika mbinguni. Na ndio maana ukisoma Ufunuo 20:5-7, utaona kuna utawala wa MIAKA 1000 wa Bwana wetu Yesu Kristo unazungumziwa pale..Sasa hii miaka 1000 itakuwa ni miaka ya matengenezo kwa hekima ya ki-Mungu, kuirejesha dunia katika viwango vya ule urithi unaopaswa uwe, kuanzia hali iliyokuwepo pale Edeni na kuendelea..bahari itaondolewa, uovu utadhibitiwa, majangwa yatabadilishwa na kuwa kama Edeni, wanyama watarejeshwa katika hali yao ya asili, samba atakula majani kama ngo’ombe hawatadhuriana n.k dunia itajaa Amani (soma Isaya 65:17-25 na Isaya 11:1-9) Na baada ya ile miaka 1000 kuisha ya Kristo kuijenga dunia pamoja na watakatifu wake, kwa wakati huo dunia sasa itakuwa tayari kustahimili UMILELE. Wakati huo wale waovu wote watahukumiwa katika kiti cheupe cha enzi cha Mungu, pamoja na shetani na malaika zake kwa pamoja watatupwa katika lile ziwa la moto.

Huko katika UMILELE kusikokuwa na muda, ni kuishi tu, kuishi tu, kusikokuwa na mwisho, raha isiyokuwa na kifani, kila siku kutakuwa na uvumbuzi wa mambo mapya kumuhusu Mungu, itatuchukua umilele kumaliza kumjua Mungu, kila siku tutamwona Mungu ni mpya kwetu,hakutakuwa na dhambi tena wala waovu, wala machozi wala magonjwa,wala uchungu, wala shida,wala njaa wala mateso..Ni raha isiyokuwa na kifani..Na siku hiyo ndipo tutakapojua maana ya mstari huu.

Isaya 55: 8 “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana.

9 Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu”. Na Maana ya mstari huu Yeremia 29: 11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”.

Tutampenda Mungu kwa viwango vingine, tutakapojua kuwa hakuumba kitu kinyonge wala kidhaifu bali kikamilifu ni sisi wenyewe ndio tuliojiharibu.

Ufunuo 21: 1 “Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena.

2 Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.

3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.

4 Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.

5 Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.

6 Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.

7 YEYE ASHINDAYE ATAYARITHI HAYA, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Tukiyajua hayo ndugu na mambo mazuri ambayo Mungu ametuandalia, hatutataka tupoteze URITHI huu ambao Mungu ametuandalia kwa mambo ya kitambo tu yapitayo,.Itakufaidia nini leo hii upate kila kitu, uwe wa kisasa kuliko watu wote, uwe wa kidunia kuliko watu wote, uwe maarufu kuliko watu wote halafu siku ile unakuwa hauna sehemu katika ule urithi wa watakatifu, Kama sasa hivi unaona uchungu kukosa utajiri tu wa kitambo itakuaje kule utakapoona unakosa URITHI NA UTAJIRI wa milele usioisha, hapo ndipo kutakuwa na majuto yasiyokuwa na mwisho, uchungu hautakuwa sana kwasababu unakwenda kuteketea katika ziwa la moto, uchungu utakuja utakapoona wenzako ndio wanaanza kuona maana ya maisha kwa kurithi yote hayo na wewe huna kitu haupo.

Bwana anasema Zaburi 147:4-5 “[Yeye] Huihesabu idadi ya nyota, Huzipa zote majina.
5 Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mpaka”.

Kila nyota ya mbinguni inayo jina, ikimaanisha kuwa zimepewa uhai, hazijawekwa kama urembo tu! Na kuna mabilioni ya nyota mbinguni na kumbuka kila nyota ina mfumo wake wa sayari, hivyo kuna mabilioni na mabilioni ya sayari na magimba angani ambayo hayo yote yana makusudi yake, ambayo yatapata kazi huko mbeleni (kwenye umilele), huo wote ni urithi wa watoto wa Mungu, Unaweza kuona ni jinsi gani itatuchukua umilele kummaliza Mungu na utajiri mkuu ulioko huko mbeleni.

Kwanini usitamani uwepo huko? Mpe Kristo leo maisha yako ayakomboe, ukabatizwe na umaanishe kabisa kumuishia Kristo naye ameahidi atakupa uwezo wa kushinda dhambi, na kuwa pamoja nawe siku zote.

Ubarikiwe

Katika sura ya sita tutaona hatua za awali kabisa wa kile kitabu kufunuliwa kimeshaanza, na sasa hivi tupo katika hatua ya mwisho ya kufunuliwa kwa muhuri wa saba, na siku yoyote utafunuliwa,

Tafadhali share kwa wengine ujumbe huu na Mungu atakubariki.Kwa Mwendelezo >>> Ufunuo: Mlango wa 6

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.


Mada Zinazoendana:

ACHENI MJUE YA KUWA MIMI NI MUNGU.

UNYAKUO.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Kifaru Malale
Kifaru Malale
3 years ago

asante mtumish wa Mungu kwa mafunuo aya, Mungu akubariki