NI KITU GANI PETRO NA YOHANA WALIKIGUNDUA KABURINI?

NI KITU GANI PETRO NA YOHANA WALIKIGUNDUA KABURINI?

Shalom..

Asubuhi ile Mariamu Magdalene alipokwenda kaburini na kukuta jiwe limeondolewa na mwili wa Yesu haupo, aliondoka ghafla na kwenda kuwapa taarifa wanafunzi wa Yesu, na kuwaambia Bwana hayupo kaburini wamemwiba na hatujui ni wapi walipompeleka..

Taarifa hiyo ya kushtusha iliwafanya watu wawili waondoke mahali pale kwa kasi sana, mmoja alikuwa ni Yohana na mwingine alikuwa ni Petro ili kwenda kuthibitisha kama waliyoelezwa ni kweli au La..

Yohana 20:2 “Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka.

3 Basi Petro akatoka, na yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini.

4 Wakaenda mbio wote wawili; na yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza kufika kaburini.

5 Akainama na kuchungulia, akaona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia.

6 Basi akaja na Simoni Petro, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala,

7 na ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwa-zongwa mbali mahali pa peke yake.

8 Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na kuamini.

9 Kwa maana hawajalifahamu bado andiko, ya kwamba imempasa kufufuka”.

Sasa ukiangalia hapo, utagundua Yohana alipofika pale kaburini na kuchungulia kwa mbali, aliona kweli Bwana hayupo na vitambaa vya sanda vimelala pale chini, pengine hilo lilimpa uhakika kuwa kweli mwili wa Bwana uliibiwa usiku na kuhamishwa pale na kupelekwa mafichoni sawasawa na maneno ya Mariam Magdalene..

Lakini tunaona Petro alipokuja baadaye kidogo, yeye kuishia pale mlangoni tu, bali alipitiliza moja kwa moja mpaka ndani kabisa mwa kaburi pale Bwana alipokuwa amelazwa ili kuthibitisha jambo hilo, Lakini alipofika karibu aliona jambo lingine la kushangaza kidogo, ambalo ndio lililowapa uhakika kuwa Bwana hakuibiwa bali ni kweli alifufuka..

Jambo hilo pengine hata wewe hukuwahi kulifahamu, ukisoma huo mstari wa 7 utaona vitambaa vya sanda vilikuwepo kweli pale chini sawasawa na Yohana alivyoona kule nje, lakini ile LESO ya kichwani biblia inasema haikuwa Pamoja na vitambaa bali ilizongwa zongwa mbali kabisa mahali pake yenyewe.. Sasa hilo neno kuzongwa zongwa biblia inamaanisha KUKUNJWA VIZURI, yaani hiyo leso ya kichwani ilikunjwa vizuri kwa utashi na Bwana mwenyewe kisha akaenda kuiweka kwa mbali kidogo na vile vitambaa vilivyokuwa vimefungwa mwilini mwake, pengine kwenye mwamba wa juu kidogo, mbali na pale alipokuwa amelala..

Hilo ni jambo la kufikirisha sana… Kama kweli wezi walikuja kumuiba wasingekuwa na muda wa kuikunja leso na kuiweka sehemu yake yenyewe mfano wa mtu anayekunja shati lake na kuliweka kabatini.. mwizi hawezi kufanya kazi kama hiyo..

Hilo ni tendo linaloonyesha kuwa Bwana hakuibiwa, bali alifufuka, na alipofufuka alianza kujifungua yeye mwenye taratibu, alipoliza, akaichukua ile leso ya kichwa akaanza kuikunja bila haraka yoyote akaenda kuiweka ndipo akaondoka..

Hilo ndilo lililowafanya Petro na Yohana biblia iseme katika mstari wa nane, wakaamini..

Habari hiyo inatufundisha nini?

Hatuwezi tukaufahamu ukweli wa Kristo kwa kuambiwa ambiwa tu, vilevile bado hatuwezi kuelewa siri ya kufufuka kwake kwa kusimama mlangoni mwa kaburi lake, Tutaelewa siri za Kufufuka kwa Kristo kwa kuzama kabisa mule kaburini alipokuwepo kama Petro, yaani kuwa tayari kufa na Kristo na kufufuka Pamoja naye kwa Habari ya dhambi, ndipo tutakapoelewa siri za kufufuka kwake kwa mapana na marefu..

Tukubali tu tusipotaka kuzama ndani katika wokovu, kamwe hatutakaa tuelewe maana ya ufufuo maishani mwetu, tukiwa wakristo vuguvugu, au wakristo jina, au wakristo wa kusita sita, wakristo wa kuvutwa vutwa tujue kuwa wapo tuliowaacha nyuma mfano wa Petro watatutangulia siku moja kuzijua siri za Kristo kuliko sisi ambao tunajiona tumeshajua kila kitu, na huku bado tupo mguu mmoja nje mwingine ndani.

Naamini hatutakuwa wasikiaji tu wa hadithi, bali tutayatendea kazi, tutazama kaburini kuuthibitisha ufufuo,…hicho ndicho Bwana anachokitaka maishani mwetu.

Bwana atubariki sote.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

SHETANI ANAITHAMINI HATA MAITI YAKO.

JE! PAKA KULIA USIKU NI ISHARA YA UCHAWI?

ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI! NA MTU YEYOTE ASIUDHARAU UJANA WAKO.

Nitaitofautishaje sauti ya Malaika na ya Roho Mtakatifu?

HAPO NDIPO WATU WALIPOANZA KULIITIA JINA LA BWANA.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments