JINSI YA KUACHA DHAMBI INAYOKUTESA.

by Nuru ya Upendo | 16 March 2026 08:46 pm03

Jina la Bwana YESU KRISTO libarikiwe, karibu tujifunze Biblia, Neno la Mungu wetu lilo njia na Mwanga wa njia yetu (Zab. 119:105).

Je! Umeokoka na kuna dhambi ambayo bado hujaiacha na hujui ufanye nini?.. Twende pamoja katika ujumbe huu utapata kitu au suluhisho la tatizo ulilo nalo.

Awali ya yote ni muhimu kufahamu kuwa, mtu anapoamua kwa dhati kabisa kutoka moyoni mwake kumfuata YESU, basi zile dhambi zote zilizokuwa zinamtesa ni lazima zife ndani yake!, lakini inapotokea mtu kaokoka lakini bado mambo ya kale yanamsumbua kuna SHIDA!

Fanya hivi ili upone hilo tatizo… ACHA HIYO DHAMBI!..ACHA KUITUMIA HIYO DHAMBI!. Huenda bado hujaelewa.. ni hivi.. ACHA HIYO DHAMBI.

Kitu chochote ukiacha kukitumia kinaisha nguvu na hatimaye kinakufa kabisa/kinapotea…hata chuma kisipotumika kinapata kutu na hatimaye kuharibika kabisa..Moto usipochochowa unakufa (Soma Mithali 26:20) na Dhambi isipotumika inakufa…Hiyo ndio tabia ya dhambi wengi tusiyoijua.. kuwa dhambi ina tabia ya KUFA.

Warumi 6:11 “Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa WAFU KWA DHAMBI na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu”.

Ukitaka kushinda dhambi ya “Kujichua”.. “Acha  Kujichua”… Ukitaka kuacha dhambi ya Uzinzi acha uzinzi, ukitaka kuacha dhambi ya ulevi, acha ulevi, ukitaka kuacha matusi, acha kutukana, ukitaka kuacha hasira acha hasira..

Mithali 28:13 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye NA KUZIACHA atapata rehema”.

 Utauliza.. “nitaachaje”.. Wazo linapokuja kichwani la kwenda kufanya hivyo, unaanza kulikataa likiwa huko huko kichwani, na kukubaliana na matokeo ya maumivu, kwasababu inakuhitaji kuingia gharama kushindani na dhambi….lakini ukijilegeza na kuitii dhambi itazidi kustawi ndani yako.

Ukishaikataa kichwani, ni wakati wa kuutiisha mwili wako, na kusema utafanya unachokisema wewe na unachokitaka na sio mwili unachokitaka!… nakuhakikishia ukimaanisha kufanya hivyo, dhambi itakosa nguvu ndani yako!.. Kwani unapoamka kila siku asubuhi na kukatisha usingizi wako ili uwahi kwenye majukumu yako, mwili huwa unapenda??..

Huwa haupendi  katika siku za mwanzo lakini unakuwa unajilazimisha tu…mpaka ile ratiba inapokaa akilini kiasi kwamba unafika wakati ukifika tu ule muda wa kuamka usingizi wenyewe unakata..kwanini!..ni kwasababu tayari umeshauua usingizi majira yale uliyozoea kuamka.. kwahiyo ukifika tu huo wakati hauhitaji kengele, tayari kengele ipo kwenye ubongo wako na usingizi unakuwa haupo huo muda..

Na dhambi ni hivyo hivyo, unaiacha na kuilazimisha isikae maishani mwako, na mwisho itakufa tu…  mahali pale ulipozoa kukutana ili kulewa, zikifika zile saa hata kiu haipo, mitaa ambayo ulikuwa ukikatiza ni lazima utamani kulewa, sasa utaikatiza bila shida yoyote.

Aina ya watu ambao ulikuwa ukiwaona huwezi kuvumilia, unawaka tamaa…utafika wakati utawaona ni watu wa kawaida sana, tena utajishangaa ulikuwa ni mtu wa namna gani?

Rushwa ulizokuwa unakula, ambazo huwezi kufanya jambo bila kuhonga, utajishangaa hutamani tena kuchukua/kutoa rushwa..

Lakini ni lazima uingie gharama katika hatua za awali, usikubali kujilegeza.. na kusubiri muujiza wa wewe kuacha hayo…amua kubadilika kwa  KUACHA DHAMBI.. ACHA DHAMBI, ACHA DHAMBI..Hakuna dawa nyingine zaidi ya hii ACHA!, na MUNGU atakusaidia..

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MADHARA YA DHAMBI YA UASHERATI.

Je tamaa ni dhambi kulingana na Yakobo 1:15?

Ipi tofauti kati ya sadaka ya dhambi na sadaka za hatia?

NITAACHAJE DHAMBI?.

Biblia inamaana gani iliposema “Dhambi ilipozidi, Neema ilizidi kuwa nyingi Zaidi”.

WhatsApp
DOWNLOAD PDF

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2026/03/16/jinsi-ya-kuacha-dhambi-inayokutesa/