by Admin | 10 July 2018 08:46 am07
Jina la mwokozi wetu YESU KRISTO litukuzwe.
Huu ni mwendelezo wa kitabu cha Esta. Katika sura hizi tatu (5,6 na 7), tunaona Malkia Esta akienda kijihudhurisha mbele ya mfalme kinyume cha taratibu ili awaombee watu wake dhidi ya adui wao Hamani aliyekusudia kuwaangamiza wayahudi wote waliokuwa dunia nzima. Lakini tunasoma badala ya Esta kuuliwa kinyume chake alipata kibali mbele ya mfalme kuwasilisha haja zake, na mfalme alipomuuliza Haja zake, Malkia Esta hakumweleza pale pale bali alimwalika kwanza kwenye karamu alizomwandalia, yeye na Hamani adui wa wayahudi. Tunasoma;
Esta 5: 2 “Ikawa, mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, yeye akapata kibali machoni pake; naye mfalme akamnyoshea Esta fimbo ya dhahabu aliyokuwa nayo mkononi. Basi Esta akakaribia, akaigusa ncha ya fimbo.
3 Mfalme akamwambia, Malkia Esta, wataka nini? Nayo ni haja gani uliyo nayo? Utapewa hata nusu ya ufalme.
4 Esta akasema, Mfalme akiona vema, na aje leo, mfalme na Hamani, kwenye karamu niliyomwandalia.
5 Basi mfalme akasema, Mhimize Hamani, ili ifanyike kama Esta alivyosema. Hivyo mfalme na Hamani wakafika katika karamu ile aliyoiandaa Esta.”
Hivyo Mfalme alipofurahishwa sana na sherehe aliyoandaliwa na Malkia Esta, alirudia tena kumuuliza ni nini anachohitaji kufanyiwa?..Lakini Esta hakumweleza mfalme chochote badala yake alimwandalia karamu nyingine nzuri zaidi na kumwalika mfalme pamoja na Hamani. Na Mfalme alipokula na kunywa na kufurahi ndipo akamuuliza kwa mara nyingine tena Esta ni nini haja ya moyo wake. Tunasoma;
Esta 7:2-10 “
2 Mfalme akamwambia Esta tena siku ya pili pale pale penye karamu ya divai, Malkia Esta, dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utafanyiziwa.
3 Ndipo malkia Esta alipojibu, akasema, Mfalme, ikiwa nimepata kibali machoni pako, na mfalme akiona vema, nipewe maisha yangu kuwa dua yangu, na watu wangu kuwa haja yangu.
4 Maana tumeuzwa, mimi na watu wangu, ili tuharibiwe, na kuuawa, na kuangamia. Kama tungaliuzwa kuwa watumwa na wajakazi, ningalinyamaza; ila hata hivyo msiba wetu haulinganishwi na hasara ya mfalme.
5 Ndipo mfalme Ahasuero aliponena, akamwambia malkia Esta, Ni nani huyu, tena yuko wapi, ambaye moyoni mwake alithubutu kufanya hivi?
6 Esta akasema, Ni mtesi, tena ni adui, ndiye huyu Hamani, mtu mbaya kabisa. Mara Hamani akaingiwa na hofu mbele ya mfalme na malkia.
7 Mfalme akaondoka katika ghadhabu yake kutoka kwenye karamu ya divai, akaingia bustani ya ngome. Hamani naye akasimama ili ajitakie maisha yake kwa malkia Esta; kwa kuwa aliona ya kwamba amekusudiwa madhara na mfalme.
8 Kisha mfalme akarudi kutoka katika bustani ya ngome hata mahali pa karamu ya divai. Ikawa Hamani amejitupa chini penye kitanda alipokuwapo Esta. Mfalme akasema, Namna gani! Je! Atamfanyia malkia jeuri hata machoni pangu nyumbani mwangu? Na neno lilipotoka kinywani mwa mfalme, wakamfunika uso Hamani.
9 Ndipo aliposema Harbona, msimamizi-wa-nyumba mmojawapo wa wale waliohudhuria mbele ya mfalme, Tazama, basi, mti wa mikono hamsini urefu wake, Hamani aliomwekea tayari Mordekai, ambaye alinena vema kwa ajili ya mfalme, upo umesimamishwa nyumbani kwa Hamani. Mfalme akasema, Mtundikeni juu yake.
10 Basi wakamtundika Hamani juu ya mti aliomwekea tayari Mordekai. Ghadhabu ya mfalme ikatulia. ”
Esta kama mfano wa Bibi-arusi wa Kristo, habari yake inatufundisha jinsi ya kumwendea Mfalme wetu (ambaye ni Bwana YESU) pale tunapokuwa na mahitaji yetu. Tunamwona Esta japokuwa alikuwa na uchungu mkubwa na shida kubwa ndani ya moyo wake, hakukimbilia moja kwa moja kuzungumza haja zake, japokuwa mfalme alifahamu kuwa ana mahitaji fulani. Lakini alitumia Hekima kwa kuufurahisha kwanza moyo wa mfalme, kwa kumuandalia karamu mbili, za thamani nzuri. Ndipo baadaye afunue yaliyokuwa ndani ya moyo wake.
Vivyo hivyo na sisi tunapomwendea Mungu ni vizuri kumfanyia kitu kwanza kinachompendeza moyo wake, kama Esta alivyomfanyia mfalme, swali ni je! katika wingi wa maombi unayompelekea Mungu kila siku je! ulishawahi kumfanyia kitu kinachompendeza kwanza?. Mfano kujitolea kwa ajili ya kazi yake?, au kumtolea Sadaka nzuri katika mali zako? au kuwasaidia wahitaji na maskini au mayatima?, au kuwavuta watu kwa Mungu? au kwenda kuwatazama wagonjwa?hususani wakristo wenzako? kumtolea shukrani kwa kumsifu na kumwabudu kwa bidii? n.k…kisha ndipo upeleke mahitaji yaako?. Kumbuka biblia inasema Mungu anafahamu haja zetu hata kabla hatujamwomba, kama tu vile mfalme alivyokuwa anajua kuwa Esta ana haja kabla hata hajamwomba. Hivyo tunapoenda mbele za Mungu tujifunze kuanza kumwandalia “karamu” impendezayo kwanza, na ndipo tuwasilishe mahitaji yetu. Kama alivyofanya Nuhu baada ya kumtolea Mungu sadaka nzuri Bwana akaibariki tena nchi na kuahidi hataiangamiza tena kwa maji.
Jambo lingine tunaona pia Esta hakujiombea ufahari bali alijiombea uhai wake pamoja na ndugu zake wayahudi. Ndipo akapewa alivyoviomba na zaidi ya alivyoviomba. Na sisi pia tunapomwendea Mungu ni vizuri kutanguliza kuwaombea watu wa Mungu na kanisa la Kristo kwa ujumla, kwasababu hao ndio ndugu zako wa daima, shetani akilidhuru kanisa, nawe pia ni lazima udhurike. Mungu anapendezwa na watu wanamwendea kwa namna hiyo, mfano Danieli alipomwendea Mungu kwa ajili ya makosa yake na watu wake Israeli tunaona Mungu alimsikia. Hivyo hivyo hata Bwana wetu Yesu aliomba siku zote kwa ajili yetu sisi na si kwa ajili yake peke yake, kadhalika na sisi tunapaswa tuchukue madhaifu ya wengine. Ili na sisi Bwana ayachukue madhaifu yetu.Wagalatia 6: 2 Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.
Biblia .inasema pia Kisasi ni juu ya Mungu yeye mwenyewe atalipa. Tunaona yule Hamani mti aliouchonga kumtundika Mordekai mtu aliyekuwa na haki ndio uliomtundikia yeye mwenyewe. Cheo alichokuwa anajisifia mbele ya Mordekai ndicho alichopewa Mordekai, Heshima aliyotafuta kutoka kwa Mordekai ndiyo yeye mwenyewe aliyokuja kumpa Mordekai pale alipoambiwa na Mfalme amchukue na kumzungusha mjini,pale alipotaka kumwangamiza Mordekai na watu wake, Mungu akageuza uteka yeye ndiye aliyeangamizwa pamoja na watu wake.
Mthali 26: 27 Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia.
Kadhalika dhambi atendayo mtu itamrudia mwenyewe wewe unayestarehe katika maisha ya dhambi na anasa, huku unajidhania unanawiri kwa kuwa na afya, mali, cheo au umaarufu, hujui kuwa uharibifu wako utakuja kwa ghafla ndani ya siku moja kama Hamani, leo hii unakejeli injili, unasema wokovu ni kwa watu waliokosa uelekeo wa maisha, biblia ni hadithi zilizotungwa na watu, hakuna mtu kuokoka duniani n.k. Injili inahubiriwa kila mahali lakini unabakia kuwa vile vile kwasababu mafanikio yako yanakudanganya fahamu kuwa utaanguka kama Hamani kama usipotubia uovu wako. Neno la Mungu linasema.
kufanikiwa kwa mpumbavu kutamwangamiza, ziwa la moto lipo halishibi kupokea watu..
Tubu umgeukie Bwana ukabatizwe katika ubatizo sahihi kwa jina lake YESU KRISTO upate ondoleo la dhambi zako.
Ubarikiwe.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312
Kwa mwendelezo >>>> ESTA: Mlango wa 8, 9 & 10. (SIKU KUU YA PURIMU)
Mada Nyinginezo:
NJIA MUNGU ALIYOIWEKA KWA KILA JAMBO.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/10/esta-mlango-wa-5-6-7/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.