INJILI YA MILELE NI IPI KATIKA BIBLIA?

by Admin | 16 July 2018 08:46 pm07

Licha ya kuwa na INJILI YA MSALABA,ambayo ndio kiini cha kila mwanadamu ipo injili nyingine pia ijulikanayo kama INJILI YA MILELE, hii ni tofauti na injili ya msalaba. Injili ya msalaba yenyewe inatangaza wokovu kwa mwanadamu tu, kwa kupitia mmoja naye ni YESU KRISTO BWANA wetu. Kwahiyo injili nyingine yeyote inayodai kumkomboa mwanadamu na haimweki Bwana Yesu kama kiini cha injili yenyewe, basi injili hiyo ni batili, kwasababu yeye pekee ndiye Njia, kweli na uzima, hakuna mtu yeyote atakayemwona Mungu, pasipo kupitia kwake yeye biblia inasema hivyo(Yohana 14:6).. Kwahiyo zipo injili nyingi zinazodai zinaweza kumkomboa mwanadamu lakini kati ya hizo ni moja tu itakayoweza kumkomboa mwananadamu! Nayo ni Kwa kupitia Yesu Kristo, na ndio maana Mtume Paulo alisema|:

2Wakoritho 11: 4 “Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au INJILI NYINGINE msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye!”

Unaona hapo? Biblia inasema kuna Yesu mwingine, roho mwingine na injili nyingine tofauti na ile iliyohubiriwa na mitume. Kwahiyo injili yoyote inayohusishwa na ukombozi wa mwanadamu inapaswa imlenge YESU KRISTO ALIYESULIBIWA,akafa na kufufuka kama kiini cha Ukombozi wenyewe, kwa asilimia mia yeye peke yake na sio pamoja mtu mwingine.

Lakini leo kwa ufupi tutaitazama INJILI YA MILELE ambayo ipo na imezungumziwa katika biblia..kama tunavyosoma katika;

Ufunuo 14: 6 “Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye INJILI YA MILELE, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa,

7 akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji”.

Sasa hii injili ya milele ni ipi?

Kama jina lake lilivyo “Milele” inamaana kuwa ni injili ambayo Ipo milele yote, ilikuwepo kabla ya mwanadamu kuumbwa, ipo sasa, na itaendelea kuwepo milele na milele, Kumbuka INJILI YA MSALABA ilikuwa na mwanzo, na itakuwa na mwisho, mwanzo wake ilikuwa ni Kalvari, na mwisho wake itakuwa katika Unyakuo. Baada ya hapo hakutakuwa na nafasi tena ya ukombozi, kwasababu mlango wa neema utakuwa umefungwa. Kitakachokuwa kimebaki ni ile ile injili ambayo ilikuwepo milele na milele.

Na ndio maana ukisoma mstari huo hapo juu utaona kuwa yule malaika(mjumbe) anapita kuitangaza hiyo injili ambapo kwa wakati huo unyakuo wa kanisa utakuwa umeshapita na mlango wa neema ya kuokolewa utakuwa umefungwa kwa watu wa mataifa.

Kwahiyo injili hii ni tofauti na ya msalaba tuliyonayo sasa, hii ya msalaba tunaifahamu kwa “kuhubiriwa”. Hatuwezi kuifahamu pasipo kuhubiriwa ndio maana biblia inasema katika;

Warumi 10: 13 “kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana{YESU KRISTO} ataokoka.

14 Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? TENA WAMSIKIEJE PASIPO MHUBIRI?

15 Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!{INJILI YA MSALABA}”

Kwahiyo unaona hapo, ni lazima awepo mtu wa kuihubiri ndipo watu waokolewe.

Tofauti na ilivyo INJILI YA MILELE. Injili hii haisambazwi kwa kuhubiriwa na mtu yeyote, Ni Mungu mwenyewe anaiweka ndani ya mtu, katika eneo maalumu la moyo wa mwanadamu linaloitwa “DHAMIRA”..ambayo kila mtu anazaliwa nayo. Na inafanya kazi ya kuhukumu njia zote mbaya zinazokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu ndani ya mtu..Na Injili hii haipo tu kwa wanadamu, ilikuwepo hata kwa malaika, kwasababu ni ya milele, ilikuwepo huko enzi na enzi, ipo na itakuwepo.

Kwahiyo sasa kitendo tu cha mtu kuwa mwanadamu, tayari moja kwa moja kuna kitu ndani yake kitakuwa kinamshuhudia mambo yanayofaa na yasiyofaa, bila hata kuhubiriwa  na mtu yeyote, au kukumbushwa na mtu yeyote, kwamfano, kila mtu anafahamu kuwa uuaji sio sawa, iwe anayo hofu ya Mungu au hana hofu ya Mungu, kila mtu anafahamu kuwa dhuluma ni mbaya, hata kama sheria isingesema hivyo, ndani ya moyo wake dhamira inamuhubiria kuwa kitendo hicho ni kibaya, Kadhalika haihitaji kuifahamu biblia kujua kuwa uonevu ni makosawizi ni makosautukanajiubakajirushwa ni makosa hayo yote hata kama mtu hajawahi kumsikia Mungu, au chochote kinachoitwa Mungu anajua kabisa hayo mambo hayafai kufanya, pia haihitaji kwenda katika vyuo vya biblia kutambua kuwa kulala na ndugu yako wa damu ni makosa, kadhalika na ushoga au usagaji ni makosa, utajikuta tu wewe mwenyewe unachukia kufanya hivyo au unalipinga hilo wazo ndani yako pale linapokuja kwasababu unajua kabisa kuwa hayo ni makosa.

Sasa hiyo ndio inayoitwa INJILI YA MILELE, Mungu anayoihubiri ndani ya moyo wa mtu. Na ndiyo hiyo siku za mwisho itakuja kukumbushwa kwa watu, wamche Mungu.wakati huo unyakuo utakuwa umeshapita.

Kwahiyo usidhani kuwa wale watu ambao hawajasikia habari za YESU(Injili ya msalaba) mahali popote, hawatahukumiwa. Hapana Watahukumiwa tu kama wale wengine kwa injili hiyo. Watu wa kipindi cha Nuhu hawakuwa na sheria waliyopewa na Mungu kama watu wa Musa na kuendelea,Na ndio maana Mtume Paulo alieleza habari za watu hawa kama tunavyosoma katika…

Warumi 1: 17 Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.

18 Kwa maana GADHABU YA MUNGU imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu.

19 Kwa kuwa MAMBO YA MUNGU YANAYOJULIKANA YAMEKUWA DHAHIRI NDANI YAO, KWA MAANA MUNGU.

20 Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; YAANI, UWEZA WAKE WA MILELE NA UUNGU WAKE; hata wasiwe na UDHURU;

21 kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.

22 Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika;

23 wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo.

24 Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao.

25 Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.

26 Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili;

27 wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.

28 Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.

29 Wamejawa na UDHALIMU, UOVU na TAMAA na UBAYA; wamejawa na HUSUDA, na UUAJI, na FITINA, na HADAA; watu wa NIA MBAYA, wenye KUSENGENYA,

30 wenye KUSINGIZIA, wenye KUMCHUKIA MUNGU, wenye JEURI, wenye KUTAKABARI, wenye MAJIVUNO, wenye KUTUNGA MABAYA, WASIOTII WAZAZI WAO,

31 wasio na UFAHAMU, wenye KUVUNJA MAAGANO, WASIOPENDA JAMAA ZAO, WASIO NA REHEMA;

32 ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao.

Umeona hapo ndugu, biblia inasema wakijua kabisa watendao mambo kama hayo wamestahili mauti lakini bado wanayatenda. Dhamira zao zikiwashuhudia ndani kuwa wanayoyafanya sio sahihi lakini wanaendelea kuyafanya, Na wewe je! Ambaye upo kwenye dhambi utahitaji mhubiri siku moja aje kukuthibitishia kwenye biblia kwamba, uvutaji sigara ni dhambi, au uasherati ni dhambi?? Angali ndani ya moyo wako dhamira inakushuhudia kabisa unachofanya ni makosa?..hakika unaweza usilione lakini fahamu kuwa hukumu inakungojea.!

Wewe unayevaa vimini, na kutembea nusu uchi barabarani unasema Mungu haangalii mavazi lakini moyo wako unakuambia kabisa hayo ni makosa unayoyafanya na bado unaweka moyo mgumu, wewe unayevaa suruali,unayepaka wanja, na kupaka lipstick, na kuvaa wig na hereni, Hukumu ipo mbeleni dada!, wewe unayesengenya, wewe ambaye ni shogawewe unayejisagawewe unayetoa mimba, wewe uliye mwasherati, wewe uliye mlevi, wewe unayetazama pornography, wewe unayefanya masturbation, wewe unayeabudu sanamu za watakatifu waliokufa zamani angalia biblia inavyokuambia hapo juu < wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu(sanamu), na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo >..Unaona unajua kabisa Mungu hawezi kufananishwa na mfano wowote wa kinyago cha kuchonga lakini wewe bado unakwenda kuvipiga magoti na kuviabudu..

2Wakorintho 6: 16 inasema “Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu?”..

Lakini biblia inaendelea kusema kwa jinsi utakavyozidi kuweka moyo wako mgumu, kuna kipindi kitafika Mungu anakuacha uendelee hivyo hivyo kwasababu umekataa kuitii hiyo sauti inayosema ndani yako, mpaka ile siku ya hukumu ije na utaingia kuzimu!! Alisema “”28 Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa”. 

Kwahiyo dada/kaka hukumu ya Mungu haikwepeki hata uwe nje ya kanisa, njia pekee ni kujisalimisha maisha yako kwa BWANA YESU ambaye yeye ndiye aliyetoa uhai wake ili akuokoe, Tubu geuka, ukapewe uwezo wa kushinda dhambi. Muda umekwenda kuliko unavyodhani, na Injili ya msalaba sio ya milele utafika wakati utatamani uingie utakosa, muda ndio huu, mpe Bwana maisha yako tangu sasa.

Ubarikiwe.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/16/injili-ya-milele-2/