Habari ile ya Pilato kuchanganya zile damu za wayahudi na pamoja na dhabihu zao,(Luka 13) ilihusu nini?

Habari ile ya Pilato kuchanganya zile damu za wayahudi na pamoja na dhabihu zao,(Luka 13) ilihusu nini?

Tukisoma

Luka 13:1 “Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya DAMU YAO NA DHABIHU ZAO.

2 Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo?

3 Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.

4 Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu?

5 Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”  


JIBU: Kama ukiitazama kwa ukaribu habari hiyo picha utakayokujia hapo ni kwamba kwa wakati huo ambao Bwana aliokuwepo na hao watu, kulikuwa na habari iliyozagaa sana mjini kote, maeneo kadha wa kadha uko uyahudi,ni habari ya tukio ambalo sio la kawaida kutokea katikati ya jamii ya watu wa Israeli,nalo si lingine zaidi ya kuuawa kwa wayahudi kikatili tena kibaya zaidi na cha kushtusha ni kuchangwa damu zao na za wanyama.  

Tuchukulie kwamfano hapa Tanzania wakati ule tulivyosikia ajali ya wanafunzi wa Lucky Vincent kule Arusha, jambo lile liliwashutusha watu wengi sana, mpaka kupelekea tukio kama lile kuzungumziwa mara kwa mara katika vyombo vya habari Tanzania nzima, na tunajua habari za matukio kama hayo huwa kwa namna ya kawaida zinachua muda mrefu kidogo kuacha kuzungumziwa, Na ndio maana unaona hapo wale watu walimwendea Bwana Yesu kumuuliza ili waone kama na yeye anazo hizo taarifa au la! na kama anazo je! yeye naye analizungumziaje suala hilo? Ni kwanini Pilato aamue kufanya kitendo cha kikatili kama kile cha kuchanganya damu za wale wagalilaya na dhabihu zao wenyewe?. Hilo ni swali lililokuwa ndani ya vichwa vya watu wengi sana kwa wakati ule.

Lakini kama tunavyofahamu kwenye biblia Pilato alikuwa ni Liwali (Governor) wa Uyahudi,(Luka 3:1) chini ya utawala wa kikatili wa Rumi (Kumbuka kwa wakati ule Bwana akiwa duniani Dola ya Rumi ndio ilikuwa inatawala Dunia) Hivyo yeye kama Liwali aliyeteuliwa na Kaisari mkuu wake huko kutoka makao yao makuu Rumi, aiongoze Yudea, alikuwa na jukumu la kuhakikisha Maeneo aliyowekwa ayaongoze yanatulia kikamilifu chini ya utawala . kwahiyo jambo lolote ambalo lingeonekana kujitokeza aidha usaliti, au vurugu, au mapinduzi, au uvunjaji wa amani katika uyahudi lisingevumilika kwa namna yoyote chini ya utawala wa Pilato kwasababu naye pia alikuwa ni mkatili…tunamwona baadaye alikuja kuhusika hata na kifo cha Bwana Yesu.   Kwahiyo biblia haijaeleza sababu hasaa ya Herode kutaka kuwaua wale Wagalilaya waliokwenda kuabudu Yerusalemu wakati wa sikukuu. Inaeleza tu waliposhuka kutoka Galilaya kwenda kuabudu ghafla kikosi cha Pilato kiliwadondokea na kuwachinja na si mahali pengine zaidi ya Hekaluni kwasababu huko ndiko dhabihu zilikuwa zinatolewa , kisha kuchukua damu zao na kuzichanganya na damu za wanyama waliokuja nao kutolea dhabihu kwa Mungu wao..

Pengine Pilato alihisi kuna tukio la usaliti au uvunjaji amani lilipangwa na hao watu au vinginevyo hatujui lakini inaelekea itakuwa ni sababu ya kiusalama zaidi.   Na tunaona pia na wale{makutano} nao hakuwajua sababu hasaa ya Pilato kufanya vile, Wao WALIKISIA TU! mioyoni mwao, labda wale watu watakuwa na laana kutoka kwa Mungu na ndio maana wamekutwa na mambo kama yale, au walimkufuru Mungu katika mioyo yao,na ndio maana Mungu akaruhusu Pilato aje kuwaua, au walikuwa na dhambi sana zisizovumilika na ndio maana yakawapatwa mambo kama yale n.k.,  

Lakini Bwana akifahamu mawazo yao, akawaongezea kuwakumbusha kisa kingine cha kushtusha kinachofanana na hicho kilichowatokea pengine miezi michache tu! nyuma huko huko Israeli kabla ya tukio hilo, nacho ni kuhusu wale watu walioangukiwa na mnara kule Siloamu..,kwamba wasidhani na wale yaliwapatwa na yale mambo eti kwasababu walimuudhi Mungu kupita kiasi? jibu lake lilikuwa ni hapana.. … Na ndio maana ukiendelea kusoma utaona Bwana anawaambia sivyo kama wanavyofikiri..   Soma tena hapo hiyo habari utaona mawazo ya wale watu yalikuwa ni nini?…

Luka13:1 Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao.

2 Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo?

3 Nawaambia, SIVYO; lakini MSIPOTUBU, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.  

Unaona hapo Bwana Yesu alijua mawazo yao kwamba wanadhani kuwa yale mambo yaliyowakuta wale watu ni kutokana na dhambi zao kuwa nyingi sana. Lakini yeye aliwambia sivyo kama wanavyofikiri.   Bwana aliwaambia hata wao pia wasipotubu yatawapatwa na mambo kama hayo hayo. Kadhalika, tetemeko la ardhi lililotokea Kagera, tunadhani wale watu walikuwa na laana sana kuliko sisi??..Ile mvua ya mawe iliyouwa makumi ya watu kule Geita tunadhani wale watu walimkosea sana Mungu kuliko sisi?? ajali ya MV BUKOBA wale watu walikuwa waovu zaidi yetu sisi?..hapana Hakika na sisi pia tusipotubu yatatukuta kama hayo hayo.. Tsunami iliyotokea 2004 huko Indonesia na kuua maelfu ya watu duniani, na sisi kunusurika, tunadhani zile nchi zilimkosea Mungu sana zaidi yetu sisi …Sivyo, tusipotubu na sisi yatatukuta kama hayo..   Huyo jirani yako aliyekufa na ajali wiki chache zilizopita unadhani alikuwa anayo bahati mbaya sana kuliko wewe?..Sivyo lakini usipotubu siku moja yatakukuta na wewe kwa ghafla na kujikuta umeenda kuzimu.  

Hivyo tujichunguze kwanza sisi mioyo yetu, kisha tujue kuwa uvumilivu wa Mungu ni kutuvuta sisi tufikie toba. Mungu amekupa uhai na pumzi, sio kwasababu wewe ni mwema sana zaidi ya yule aliyekufa jana hapana..lakini fahamu kama usipomzalia matunda ya uhai wako sasa, yatakukuta hata pengine makubwa zaidi ya hayo yaliyowakuta hao wengine. Je! Umeokolewa? Je! Una uhakika wa kwenda mbinguni ukifa leo kifo cha ghafla?… yahakiki maisha yako tena, na umgeukie Mungu maadamu muda upo.  

Ubarikiwe sana .jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada zinazoendana:

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI:

USIISHIE KUTAZAMA JUU, ENDELEA MBELE.

JINSI EDENI ILIVYOKUWA.

MWENDO UNAOSHANGAZA SANA!

MUUNGANO WA DINI NA MADHEHEBU YOTE, UMEKARIBIA.


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments