KAMA MWIZI USIKU WA MANANE.

by Admin | 17 July 2018 08:46 am07

Kama tunavyofahamu wakati wa usiku kabla hatujalala, huwa ni lazima tufunge milango yetu yote, kwa makufuli na makomeo, na hii sio kwasababu tunapenda kujifungia tu hapana! bali ni kujiweka katika hali ya usalama dhidi ya WEZI usiku, Kwasababu hatujui ni wakati gani wataingia na kuleta madhara. Hii ni desturi kwa kila mtu,hakuna mtu asiyefahamu kuwa anapaswa kufunga milango yake wakati wa usiku.

Lakini pamoja na hayo kufunga mlango tu na kwenda kulala haitoshi, kwasababu mwizi anajua kabisa akienda atakutana na changamoto ya milango kufungwa hivyo atakuwa amekwisha jipanga kwa njia mbadala ili kuhakikisha kuwa zoezi lake la kuiba linafanikiwa kikamilifu, hivyo ni dhahiri kuwa atakuwa na vifaa husika vya kuvunjia nyumba.

Kwahiyo ili mwenye nyumba aweze kunusuru mali zake au roho yake sio tu KUBANA MILANGO yake bali anapaswa pia AKESHE, Kwasababu mwizi hawezi kuharibu kama mwenye nyumba yupo macho. Hivyo dawa pekee ya kudhibiti wizi usiku ni kubana milango pamoja na KUKESHA.

Ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Bwana Yesu Kristo,akifananisha kuja kwake na kama ujio wa mwizi wakati wa usiku alisema …

Mathayo 24:40-44″ Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;

41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.

42 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.

43 Lakini fahamuni neno hili; KAMA MWENYE NYUMBA ANGALIIJUA ILE ZAMU MWIVI ATAKAYOKUJA, ANGALIKESHA, wala asingaliiacha nyumba yake KUVUNJWA. 

44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa damu yuaja.

43 Lakini fahamuni neno hili; KAMA MWENYE NYUMBA ANGALIIJUA ILE ZAMU MWIVI ATAKAYOKUJA, ANGALIKESHA, wala asingaliiacha nyumba yake KUVUNJWA.

Tukisoma pia katika 

Marko 13:32 Bwana Yesu alisema maneno haya: Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.

33 Angalieni, KESHENI, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.

34 Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.

35 Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, KWAMBA NI JIONI, AU KWAMBA NI USIKU WA MANANE,au AWIKAPO JIMBI, au ASUBUHI;

36 asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.

37 Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, KESHENI.”

Kumbuka hapo Bwana Yesu hakusema “fungeni milango” bali alisema “kesheni” kwasababu inajulikana ni wajibu wa kila mtu kufunga milango yake, na kufunga milango ina maana kujiona umeokoka lakini maisha yako hayaendani na ukristo,umebatizwa na unaenda kanisani lakini umelala katika roho(vuguvugu), nje milango imefungwa lakini ndani umelala kwasababu hiyo basi mwizi atakapokuja hautajua lolote.

Mkristo aliyeridhika na dhehebu lake au mapokeo yake lakini hazingatii mambo ya muhimu yanayohusiana na wokovu wake na maisha yake ya umilele ni sawa na mtu aliyejifungia na kulala usingizi.

Dunia sasa hivi ipo katika GIZA NENE SANA ikiashiria kwamba huu ni wakati wa USIKU na ndio wakati uliokaribia wa BWANA kurudi tena, kuongezeka kwa maovu ulimwenguni kama vile anasa,ulevi,uasherati uliokithiri hususani katika ulimwengu huu wa sasa wa utandawazi,mauaji,uchawi,rushwa,dhuluma, kupenda ulimwengu zaidi ya Mungu,n.k. vinawafanya watu wazidi KULALA usingizi wa mauti, na jinsi giza linavyozidi kuongezeka ndivyo wakristo nao wanavyozidi kushawishika kulala.

Sasa katikati ya kilele hichi cha maovu hapo ndipo Kristo atakaporudi, alisema kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu watu walikuwa wakila na kunywa(ikiashiria kufanya anasa),walikuwa wakipanda na kujenga, hata siku ile ikawajilia kama ghafla, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adamu.

1Thesalonike 5:1 Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.

2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.

3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.

4 Bali ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.

5 Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza.

6 Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.

7 Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku.

8 Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu. “

Bwana Yesu pia alisema..

Ufunuo 16:15 “(Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.) “.

MAANA YA KUKESHA NI NINI?

Kukesha kunakozungumziwa ni KUKESHA KATIKA ROHO, kutokulala katika roho, kudumu katika utakatifu,huku matunda ya roho yakijidhihirisha upole,kiasi,upendo,uvumilivu,n.k pamoja na kuishi maisha ya kama mtu anayemngojea Bwana wake, kama msafiri duniani, asiyefanana na watu wa ulimwengu huu waliousingizini, huku macho yake yakitazama mambo ya mbinguni yanayokuja,

Utajisikiaje siku hiyo utakapoona wenzako wamekwenda kwenye unyakuo na wewe umebaki? ni uchungu usioneneka, mara nyingine Mungu anawaotesha watu ndoto kwamba unyakuo umepita na wenyewe wamebaki, hapo ni Mungu anajaribu kuwakumbusha watu kwamba maisha yao hayajakidhi vigezo vya kwenda mbinguni.Huu ni wakati wa kuamka usingizini biblia inasema..katika Waefeso 5:14 “Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.”

Amka ndugu utoke katika usingizi wa wafu wa ulimwengu huu, uasherati ni usingizi,kiburi cha uzima ni usingizi,ulevi,sigara,anasa,fashion,ushirikina,usengenyaji,rushwa,ulawiti,utoaji mimba,wizi,utukanaji vyote hivi ni usingizi wa kiroho, na kumbuka siku Kristo atakapokuja kulichukua kanisa lake hawa hawatajua lolote badala yake watabaki hapa wakingojea ile SIKU KUU YA BWANA inayowaka kama tanuru ndivyo biblia inavyosema,

2 Petro 3:10 “Lakini siku ya Bwana ITAKUJA KAMA MWIVI; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.

11 Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo,IMEWAPASA NINYI KUWA WATU WA TABIA GANI KATIKA MWENENDO WENU MTAKATIFU NA UTAUWA,

12 mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? “.

Kwa kuwa sisi sote hatujui ni saa gani Bwana atakayokuja , ni wajibu wa kila mtu aliye mkristo kukesha kwa kuishi maisha ya uangalifu katika giza hili nene lililopo dunian sasa.

Mungu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Kwa maombezi/Ushauri/Ubatizo/ Whatsapp. Tupigie namba hizi: +255693036618


Mada Nyinginezo:

JINSI ITAKAVYOKUWA KATIKA SIKU ILE

LENGO LA SHETANI KWA WATOTO WA KIZAZI HIKI.

UKOMA NA UJANE ULIO NDANI YAKO, UMEUPATIA TIBA?

BWANA ALIPOSEMA KUWA YEYE NI “MUNGU WA MIUNGU” ALIKUWA NA MAANA GANI?..JE! YEYE NI MUNGU WA SANAMU?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/17/kama-mwizi-usiku-wa-manane/