MPAKA UTIMILIFU WA MATAIFA UTAKAPOWASILI.

by Admin | 17 July 2018 08:46 am07

Hii neema tuliyonayo watu wa mataifa, haikuanzia kwetu, bali ilitoka kwa wengine lakini kwa huruma za Mungu walipokonywa wao tukapewa sisi. Israeli kama Taifa teule la Mungu walikuwa wameshafikia kilele cha kula matunda ya taabu yao kwa kuja kwake mkombozi ambaye ni Mesiya wao waliyemngojea kwa miaka mingi, ambaye angewaokoa na dhambi zao na maadui zao, lakini mambo hayakuwa kama yalivyo kwasababu badala ya wao kufaidi lile TUNDA, wakanyang’anywa na kupewa wengine ambao ndio sisi mataifa.

Hivyo mkombozi wa nafsi zao alipokuja Mungu aliwapiga upofu, wasiweze kumuamini kwasababu maalumu ili sisi (mataifa:mimi na wewe) tuweze kumwamini na kushiriki kipawa hicho cha neema.

Biblia inasema hivi juu ya Taifa la Israeli.

Warumi 11: 10 “Macho yao yatiwe giza ili wasione, Ukawainamishe mgongo wao siku zote.
11 Basi nasema, Je! Wamejikwaa hata waanguke kabisa? Hasha! Lakini KWA KOSA LAO WOKOVU UMEWAFIKILIA MATAIFA, ili wao wenyewe watiwe wivu.

12 Basi, ikiwa kosa lao limekuwa utajiri wa ulimwengu, na upungufu wao umekuwa utajiri wa Mataifa, je! SI ZAIDI SANA UTIMILIFU WAO?”.

Hii ni dhahiri tukiliangalia taifa la Israeli tangu kipindi kile Bwana Yesu alipokuja, mpaka sasa wayahudi wamekuwa wakiupinga ukristo, hawataki kumwamini Bwana Yesu kama ndiye Masia wao aliyetabiriwa, wanasema Yule ni mtu tu wa kawaida, Taifa zima haliamini habari za Yesu ni masalia tu (yaani watu wachache sana) waliopewa neema ndio wanaoamini lakini sio taifa, sio kwasababu ni waovu sana, hapana bali ni kwasababu Mungu mwenyewe kawapiga upofu makusudi wasilione hilo, kwa ajili yetu sisi mataifa, kwasababu mfano wangeamini sisi mataifa tusingekuwa na nafasi yoyote katika ufalme wa mbinguni. Kwasababu Mungu huwa hashughuliki na mataifa mawili kwa wakati mmoja. Alipotembea na Israeli, watu wa mataifa aliwaweka kando, vivyo hivyo na sisi.

Lakini hilo halitadumu milele, Mungu analipenda na analionea wivu taifa lake Israeli siku zote, ambalo hilo lingestahili kuwa la kwanza kupokea Baraka za mwokozi kwasababu hiyo basi utafika wakati Bwana atalirudia taifa lake tena, na watu wa mataifa waliobakia walioikataa neema watapigwa upofu wa mauti na kuondolewa. Ni kipindi cha hatari na kimeshaanza taratibu taratibu.

Ndugu tukishakifikia huo wakati hata uiweje watu hawataweza kuipokea injili tena, maana ili kuiamini inahitajika neema kutoka kwa Mungu mwenyewe, kwasababu biblia inasema

Yohana 6:44 “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho”.

Hivyo hiyo nguvu ya kuvutwa kwa Mungu haitakuwepo tena kwa mataifa, kitu kitakachobakia kwa watu wa mataifa ni NGUVU YA UPOTEVU inayotoka kwa Mungu soma..

2Wathesalonike 2: 10 na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.

11 KWA HIYO MUNGU AWALETEA NGUVU YA UPOTEVU, WAUAMINI UONGO;

12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu”.

Watabakia katika dini zao na madhehebu yao wakidhani kuwa ndio wanamwabudu Mungu, kama wale mafarisayo na masadukayo walivyokuwa wakati ule neema ya Kristo ilipotolewa kwao, badala ya kumpokea kinyume chake walimsulibisha, ndivyo itakavyokuwa kwa watu wanaokataa KUIAMINI KWELI sasa hivi. Sasa kama wayahudi ambao walikuwa ni watu wa Mungu yaliwakuta mambo kama hayo Na sisi je! Tutawezaje kupona tusipouthamini wokovu mkuu namna hii??(Waebrania 2:3).

Biblia imetufananisha sisi watu wa mataifa kama mizeituni mwitu, na Israeli kama mzeituni halisi, kwamba wao walikatwa ili sisi tupandikizwe tulio mzeituni mwitu na tuzae matunda halisi ya mzeituni. Kama Mtume Paulo alivyoandika katika.:

Warumi 11:15-24 “15 Maana ikiwa kutupwa kwao{ISRAELI} kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa?

16 Tena malimbuko yakiwa matakatifu, kadhalika na donge lote; na shina likiwa takatifu, matawi nayo kadhalika.

17 Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe MZEITUNI MWITU ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake,

18 usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe.

19 Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi.

20 Vema. Yalikatwa kwa kutokuamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope.

21 KWA MAANA IKIWA MUNGU HAKUYAACHIA MATAWI YA ASILI, WALA HATAKUACHIA WEWE .

22 Tazama, basi, wema na ukali wa Mungu; kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali.

23 Na hao pia, wasipokaa katika kutokuamini kwao, watapandikizwa; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena.

24 Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeituni mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa, kinyume cha asili, katika mzeituni ulio mwema, SI ZAIDI SANA WALE WALIO WA ASILI KUWEZA KUPANDIKIZWA KATIKA MZEITUNI WAO WENYEWE?.

Unaona hapo kuna wakati utafika ambao Mungu ameuamuru kwa watu wake Israeli, KUPANDIKIZWA TENA na sio siku nyingi. Na ukishafika huo wakati Israeli wote watafumbuliwa macho na kumpokea Bwana Yesu na kufahamu kuwa walifanya makosa kumsulibisha masihi wao, watamlilia na kumuombolezea biblia inasema hivyo (Soma Zekaria 12:9-14). Na neema hii itakaporudi Israeli itakuwa imebakia miaka 7 tu mpaka dunia iishe.

Kumbuka wakati huo Bwana atakuwa ameshamaliza kushughulika na watu wa mataifa, na shughuli hiyo itaishia na UNYAKUO wa kanisa, baada ya hapo ni giza kuu kwa mataifa yote na kufunuliwa kwa mpinga-kristo akitenda kazi katikakati ya wale waliobaki wasiokwenda kwenye unyakuo.

Ukiendelea mstari wa 25-27 utaona mtume Paulo anaendelea na kusema..

“25 Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, MPAKA UTIMILIFU WA MATAIFA UWASILI.

26 Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.

27 Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao.”

Kwa miaka 2000 sasa, Mungu amekuwa akilia katika mioyo ya watu wa mataifa, akiwaambia “waje wanywe maji ya uzima bure”. Neema imekuwa kubwa kiasi kwamba Mungu analithibitisha Neno lake kwa ishara na miujiza ya kupita kiasi, wengine anawavuta kwa njia ya ndoto, wengine kwa maono, wengine kwa wahubiri, n.k. ili tu waingie katika karamu ya Mungu aliyowaandalia watu wake wa mataifa. Wapo ambao wameitii injili na kuiamini na kuifuata lakini cha kuhuzunisha ni kwamba wapo ambao wanaitupilia mbali NEEMA hii, na kumbuka kukatwa kwa mataifa kumeshaanza, kama tu vile kupandikizwa kwa Taifa la Israeli kunavyoanza.

Hauoni mataifa mengi hususani ya magharibi ambayo hapo kwanza yaliitwa ya kikristo na kutuletea sisi injili sasa hivi yamegeuka kuwa ni mataifa yanayo mpinga Kristo?. Hizo ni dalili za kukatwa, Na ukiangalia injili inamalizikia na Afrika(chini ya jangwa la Sahara) kwasababu ndio waliokuwa wa mwisho kupelekewa injili, na ndio inamalizikia hivyo, Irejee ilikotoka Israeli. Embu fikiri ni wakati gani huu tunaoishi??. Israeli inarudiwa na maandalizi ya kujenga Hekalu la Tatu huko Yerusalemu yameshakamilika. Miaka 70 sasa imeshapita tangu Israeli kupata uhuru wake baada ya kukaa zaidi ya miaka 2500 bila taifa. Leo hii mataifa yote macho yao yanaelekea Israeli ni nini kinachojiandaa kutokea?.

Ndugu Unyakuo ni muda wowote tokea sasa, tumeambiwa “KWA MTINI JIFUNZENI(ambalo ni Taifa la Israeli)”..Hivyo jitahidi kuingia katika huo mlango wa NEEMA sasa kabla haujafungwa, Biblia inasema

 Luka 13: 23-24 “Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.”

Tujitahidi ndugu.

Unapohubiriwa injili na kuipinga ndani ya moyo wako..ni dalili za awali kuwa neema inaondoka kwako.

Maombi yangu ni ufungue moyo wako sasa, Kristo ayabadilishe maisha yako.

2Wakoritho 6:1-2“ Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure. (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;TAZAMA, WAKATI ULIOKUBALIKA NDIYO SASA; TAZAMA SIKU YA WOKOVU NI SASA)”.

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/17/mpaka-utimilifu-wa-mataifa-utakapowasili/