by Admin | 17 July 2018 08:46 am07
Tunaposoma biblia tunajifunza mambo mengi sana, yahusuyo tabia za Mungu, na moja ya tabia ya kipekee sana ya Mungu ni “kutokumlazimisha mtu kufanya jambo Fulani”. Kuna kipindi nilitamani na nilimuomba sana Roho Mtakatifu anivae na kuniendesha pasipo mimi mwenyewe kujitambua kama vile mtu aliyepagawa na mapepo.
Kwasababu watu wenye roho za mashetani huwa wanaendeshwa mpaka wanakuwa hajitambui tena mfano vichaa. Niliendelea kuomba hivyo mpaka siku Bwana aliponipa ufahamu na kugundua kuwa Mungu hatendi kazi kwa namna hiyo japo anao uwezo huo, lakini hamvai mtu na kumfanya mateka kama vile pepo linavyofanya.
Roho Mtakatifu ni msaidizi na mshauri na pia ni mpole, kamwe hamlazimishi mtu kuchukua uamuzi Fulani, Na ndio maana mtu anapoamua kuwa mwovu, haendi kumlazimisha aokoke, yeye anachofanya ni kumshawishi na kumshauri na kumpa kila sababu ya kuacha dhambi, lakini akikataa anamwacha aendelee kufanya anachokitaka lakini akikubali anaendelea naye.
Na vivyo hivyo katika kuifanya kazi ya Mungu, wengi wanangojea waone maono kama mtume Paulo alivyoona, au watokewe na malaika, au washukiwe na uweza wa ajabu walazimishwe kama Yona, au wasikie sauti kutoka mbinguni ikiwaambia nenda, au watabiriwe n.k.
Napenda kukwambia ndugu ukitegemea njia hiyo mwisho wa siku utaishia kuvunjika moyo pale utakapoona hakuna jambo lolote lililotokea kwa kipindi ulichokuwa unasubiria na muda umeshakwenda. Njia kama hizo Mungu akizitumia ni kwa neema zake tu! Kwa kuonyesha uweza wake. Lakini sio njia aliyoikusudia kutumia kuwatuma watu wake katika kazi yake. Tunamtumikia Mungu kwa imani na sio kwa kuona, na Mungu anataka mtu afanye kwa moyo wake mwenyewe na sio kwa kulazimishwa.
Tunaweza tukajifunza mifano ya watu watatu katika biblia ambao wanaweza kutusaidia katika kujua njia sahihi ya kumtumikia Mungu.
Daudi alikuwa ni mfalme wa Israeli, aliyepitia taabu nyingi katika maisha yake lakini Bwana alipomstarehesha, na kumpa ufalme na vitu vyote, alifikia wakati akaanza kumtafakari Mungu wake, dhamiri yake ikaanza kumchoma..akasema mimi Daudi naishi katika jumba la kifalme wakati Mungu wangu anakaa kwenye hema liliochakaa tena kwenye giza katika kijiji Fulani huko Shilo??. (Kwasababu wakati huo sanduku la Agano la Mungu lilikuwa linakaa Shilo). Ndio Daudi akaazimu moyoni mwake kumjengea Mungu nyumba nzuri ya kukaa kwa hiari yake mwenyewe.. Na alipofikiria hivyo tu biblia inasema..
1 Samweli 7: 1 “Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo Bwana alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote,2 mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.
3 Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana Bwana yu pamoja nawe.
4 Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema,
5 Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake?
6 Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani.
7 Mahali mwote nilimokwenda na wana wa Israeli wote, JE! NIMESEMA NENO LOLOTE NA MTU YEYOTE WA WAAMUZI WA ISRAELI?, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, NIKISEMA, MBONA HAMKUNIJENGEA NYUMBA YA MIEREZI?.
8 Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, Bwana wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli;
9 nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani.”
Ukizidi kusoma mbele utaona Daudi kwa kufanya hivyo aliahidiwa kuwa kiti chake cha enzi na ufalme utathibitika milele, Na ndio maana Mungu aliuchagua uzao wa Daudi kupitia yeye Kristo atokee huko, na mji wake Yerusalemu kuwa makao makuu ya MASIHI duniani.. Na Daudi ndiye aliyeupendeza moyo wa Mungu kuliko watu wote.
Sasa je! DAUDI ALINGOJEA MAONO YAMJIE ILI AMJENGEE MUNGU NYUMBA??.. Hapana aliona kila sababu ya kwanini asifanye vile kwa Mungu angali anao huo uwezo?. Na ndipo Mungu akampa thawabu kuu kwa maamuzi ya busara aliyoyafanya.
Mfano mwingine tunamwona Nehemia, aliyekuwa mnyweshaji wa Mfalme wa Uajemi..Lakini siku moja ndugu zake walitoka Yerusalemu, na kumpasha habari kuwa nyumba ya Mungu, na Ukuta wa Mji umebomolewa. Habari zile zilimuhuzunisha sana hata akaamua afunge na kuomboleza na kulia kwa siku nyingi kwa ajili ya mji wake, na kumuomba Mungu dua na msamaha kwa Israeli, kumbuka Nehemia hakuwa nabii, alikuwa ni mtu tu! wa kawaida, mfanyaji wa kazi za ndani za mfalme wa mataifa.
Hivyo akawaza moyoni mwake tu, siwezi kukaa katika hali hii ya raha huku nyumba ya Mungu wetu kule Yerusalemu imekaa katika hali ya kuharibiwa. Kwa kufanya hivyo Mungu akamuhurumia na kumpa kibali cha mfalme kwenda Yerusalemu kukarabati nyumba na ukuta wa mji..
Japo alipitia taabu nyingi sana wakati wa kujenga ukuta, maadui waliwazunguka kila upande, mkono mmoja ulishika silaha na mwingine nyenzo za ujenzi, lakini kwa bidii yeye na wenzake walifanikiwa kumaliza kuujenga ukuta wa mji, mpaka akafikia kusema UNIKUMBUKE MUNGU WANGU, kwa taabu hizi..
Huyu naye pia hakuwahi kuona maono, wala kuota ndoto, au kuzungumza na malaika, au kushukiwa na upako aliona tu nyumba ya Mungu ipo katika hali mbaya inanipasa nifanye kitu!!.. Lakini leo hii tunaona ushujaa wa Nehemia Mungu kampa kumbukumbu lisilofutika leo tunakisoma kitabu chake japo hakuwa nabii wala kuhani wala mwandishi.
Mfano mwingine tunamwona Yule mwanamke mwenye dhambi aliyemwendea Yesu, pamoja na dhambi zake zote alizokuwa nazo aliona kuna mapungufu katika mwili wa Yesu, aliona kuwa miguu ya Yesu ni michafu, ndipo akaona kuna sababu ya kuiosha kwanza, hivyo akatumia machozi yake, badala ya maji, akatumia nywele zake kumfuta badala ya kitambaa, na baada ya kuona imesafishika akampaka mafuta yenye manukato ya thamani nyingi sana (thamani yake kwasasa ni sh. Milioni 6)…Kumbuka huyu hakuona maono aliamua tu mwenyewe kufanya hivyo baada ya kuona mapungufu, lakini baada ya tukio hilo Bwana Yesu aliwaambia..
Luka 7: 44 “Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake.
45 Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu.
46 Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu amenipaka miguu yangu marhamu.
47 Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo.
48 Kisha alimwambia mwanamke, Umesamehewa dhambi zako.”
Kumbe iliwapasa wajue wao wenyewe kuwa miguu ya Bwana ni michafu na inahitaji kuoshwa, lakini wao walisubiria waambiwe..ndugu nataka nikuambie kama na wewe leo unasubiria Mungu akuambie nenda kafanye kitu fulani angali unafahamu kabisa kuna huo uhitaji,..jua tu hatakuambia …Ni jukumu lako wewe kuchukua hatua.
Ipo mifano mingi ya namna hii katika biblia yupo mwanamke mwingine alifanya kama huyu wa kwanza ukisoma Mathayo 26:13, utaona alimmwagia Bwana mafuta katika nywele zake, japo wengine waliona kama anatapanya pesa lakini Bwana alimwambia kuwa kwa kuwa amefanya vile Popote itakapohubiriwa injili, tendo hilo litatajwa kwa kumbukumbu lake. Huyu naye hakusubiria neema imshukie, au asubirie nabii amtabirie.
Hivyo ndugu, mahali ulipo,au kanisa ulilopo au chochote unachokifanya..je! unaugua kwa ajili ya kazi ya Mungu au unasubiri jambo Fulani Mungu akutendee ndipo uanze kumtumikia Mungu?. Mungu amekubariki katika Mali zako, zitumie hizo kufanya kazi ya Mungu, habari njema ziwafikie wengi kama wakina Martha, sio lazima uwe muhubiri, Nehemia hakuwa muhubiri, lakini alimfanyia Mungu kitu kinachoonekana, unaona choo kichafu kanisani, nyasi zimeota, unangoja uone maono juu ya hilo?.
Unaona kuna umuhimu wa kuwavuta watu kwa Kristo unasubiria kuitwa?? Utaitwa lini na huku umeshakaa katika ukristo kwa miaka mingi?. Lakini mtu atasema mimi sijui wito wangu..ndugu tumeitwa wote kuwa mashuhuda wa Kristo?.
Wewe ni fundi wa nyumba au technician unaona kuna kasoro katika nyumba ya Mungu embu kuwa kama Nehemia usingojee maono yakushukie kwenda kufanya hivyo, usisubirie mtu mwingine aajiriwe kuja kuifanya hiyo kazi angali ipo katika uwezo wa mikono yako.
Umepata nafasi ya kukaa mitandaoni na unaona kabisa kuna uhitaji wa watu kumjua Mungu usisubirie lolote kwasababu kamwe Bwana hatakuambia au kukulazimisha kufanya hicho kitu.. Inahitaji hekima tu kulitambua hilo.
Ni maombi yangu utachukua hatua sasa kwa kila sehemu Bwana alipokuweka kwa ajili ya Kristo. Mungu atakusaidia na kumbukumbuku lako halitaondoshwa milele.
Mungu akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Kwa mawasiliano, maombi/ushauri/ubatizo/ whatsapp: Namba zetu ni hizi: +255693036618/ +255789001312
Mada Nyinginezo:
USIISHIE KUTAZAMA JUU, ENDELEA MBELE.
MAMBO AMBAYO MALAIKA WANATAMANI KUYACHUNGULIA.
JE! MKRISTO ANARUHUSIWA KULA NGURUWE, NA KUVUTA SIGARA NA KUNYWA POMBE?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/17/ni-maono-yapi-hayo-unayosubiria/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.