NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?

by Admin | 17 July 2018 08:46 am07

Karibu tuongeze maarifa katika Neno la Mungu,

Tukisoma kwenye biblia kitabu cha warumi 4 tunaona mtume Paulo anasisitiza kuwa mtu hahesabiwi haki mbele za Mungu kwa matendo yake bali kwa Imani, lakini tukisoma tena katika kitabu cha Yakobo 2, Yakobo anasisitiza kuwa mtu hahesabiwi haki kwa Imani tu, bali pia na kwa matendo. Tunaona sentensi hizi mbili zinaonekana kama kupingana, Lakini je! Biblia kweli inajipinga au ni sisi uelewa wetu ndio unaojipinga??..tuichambue mistari hii miwili kwa undani kidogo..

1) Warumi 4:1-6

“1 Basi, tusemeje juu ya Ibrahimu, baba yetu kwa jinsi ya mwili?
2 KWA MAANA IKIWA IBRAHIMU ALIHESABIWA HAKI KWA AJILI YA MATENDO YAKE, ANALO LA KUJISIFIA, LAKINI SI MBELE ZA MUNGU.

3 Maana maandiko yasemaje? Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki.

4 Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni.

5 Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki.

6 Kama vile Daudi anenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo,.

Ni dhahiri kuwa hapa mtume Paulo alipokuwa anazungumzia MATENDO, alikuwa analenga matendo yatokanayo na sheria  ya kwamba hakuna mwanadamu yoyote anaweza akasimama mbele za Mungu kwa matendo yake kuwa ni mema au amestahili kumkaribia Mungu.

Kwa mfano mtu kusema nimestahili kwenda mbinguni kwa matendo yangu mazuri, mimi sio mwasherati, sio mwizi, sio mtukanaji, sio mlevi, sio mwongo, sio mwuuaji n.k. kwa kusimamia vigezo kama hivyo hakuonekana hata mmoja aliyeweza kumpendeza Mungu isipokuwa mmoja tu naye ni BWANA wetu YESU KRISTO! wengine wote kama biblia inavyotaja kuanzia Adamu mpaka mwanadamu wa mwisho atakayekuja duniani Mungu alishawaona wote tangu mwanzo kuwa wamepungukiwa na utukufu wake,

Warumi 3:23″ kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; “

 na ukisoma pia Zaburi 14:2-3 inasema

 Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu.Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja.” 

Hivyo hii inadhihirisha kabisa hakuna hata mmoja atapata kibali mbele za Mungu kwa matendo yake mazuri.

 Lakini swali ni je! kama sio kwa matendo, basi mtu atapata kibali mbele za Mungu kwa njia gani tena??..

Ukiendelea kusoma mbele tunasoma mtume Paulo anasema ni kwa njia moja tu tunaweza kuhesabiwa haki mbele za Mungu nayo ni njia ya kumwamini BWANA YESU KRISTO tu!. Ndio njia pekee inayotupa sisi kupata kibali mbele za Mungu, kwa namna hiyo basi tunayo haki ya kuwa na uzima wa milele, kwenda mbinguni, kubarikiwa kwasababu tumemwamini mwana wa Mungu YESU KRISTO na sio kwa matendo mema tuyatendayo.

Kumbuka zipo dini nyingi zenye watu ambao wanatenda matendo mema lakini je! wanao uzima wa milele ndani yao? utakuta ni wema kweli wanatoa zaka, wanasaidia maskini, sio waasherati, sio  walevi n.k. lakini bado Mungu hawatambui hao. Lakini sababu ni moja tu, hawajamwamini mwana wa Mungu ili aziondoe dhambi zao.

Kwahiyo tunaona hapo jambo kuu Mungu analolitazama ni wewe kumwamini mwana wa Mungu, na ukishamwamini (yaani kumpa maisha yako) ndipo ROHO wake MTAKATIFU anakutakasa na kukufanya uishi maisha matakatifu ya kumpendeza.

2). Lakini tukirudi kusoma kitabu cha Yakobo 2:21-26 

“21 JE! BABA YETU IBRAHIMU HAKUHESABIWA KUWA ANA HAKI KWA MATENDO, hapo alipomtoa Isaka mwanawe juu ya madhabahu?

22 Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale.

23 Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu.

24 Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake.

25 Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine?

26 Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.

Katika kifungu kile cha kwanza ukiangalia kwa undani utaona kuwa mtume Paulo alikuwa anazungumzia juu ya MATENDO YATOKANAYO NA SHERIA. Lakini hapa Yakobo hazungumzii habari ya matendo yatokanayo na sheria bali ni MATENDO YATOKANAYO NA IMANI.. hivyo ni vitu viwili tofauti. 

MFANO WA MATENDO YATOKANAYO NA IMANI:  

Kwamfano: Mtu amepimwa na daktari na kuambiwa kuwa anaugonjwa wa kisukari, na hatakiwi kula vyakula vyenye asili ya sukari na wanga. lakini mtu yule akilishikilia lile Neno kwenye biblia Mathayo 8:17 linalosema ” ….Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu. ”

Na kuliamini na kuamua kuchukua hatua na kusema mimi ni mzima na sio mgonjwa kwasababu yeye alishayatwaa madhaifu yetu, na kusimama na kutembea kama mtu mzima asiyeumwa na kula vyakula vyote hata vya sukari na wanga ingawa daktari alimkataza, akiamini kuwa amepona kwa NENO lile atapokea uponyaji wake. sasa  kitendo cha yeye kuchukua hatua ya kuishi kama mtu mzima ambaye haumwi japo ni mgonjwa na kula vile vyakula alivyoambiwa asile hicho ndicho kinachoitwa MATENDO YA IMANI Yakobo aliyoyazungumzia..

Unaona hapo haki ya huyo mtu kuponywa haikutokana na matendo ya sheria (yaani utakatifu, kutokuwa mwasherati, au mlevi au mwizi n.k.). bali ni matendo yaliyotakana na kumwamini YESU KRISTO katika NENO lake ndio yaliyomponya. Na ndio jambo hilo hilo lililomtokea Ibrahimu pale alipomwamini Mungu na kumtoa mwanae kuwa dhabihu, kwahiyo kile kitendo cha yeye kumtoa mwanawe hayo ndiyo MATENDO yanayozungumziwa na Yakobo YA IMANI kwasababu hiyo basi ikampelekea yeye kupata haki mbele za Mungu.

Unaona hapo haikuwa sababu ya yeye kutokuwa mwongo, au mlevi, au muuaji n.k. ndio kulimpa haki yeye ya kubarikiwa hapana bali ni kumwamini Mungu na kuiweka ile imani katika matendo. Kwasababu kama ingekuwa kwa usafi wake Mtume Paulo asingesema Ibrahimu hana la kujisifu mbele za Mungu.

Vivyo hivyo kwa mambo mengine yote kwamfano haki ya kuzungumza na Mungu, haki ya kuponywa magonjwa,  haki ya kubarikiwa, haki  ya kwenda mbinguni, haki ya karama za rohoni, haki ya kuwa mrithi, n.k. havitokani na MATENDO YA SHERIA bali MATENDO YA IMANI. Kwa sisi kumwamini YESU KRISTO katika Neno lake ndipo tunapopata vyote.

Kwahiyo matendo yote mema ya sheria yanakuja baada ya kuwa ndani ya Kristo na hayo ndiyo yanayokupa uhakika kama upo ndani ya Kristo, ni kweli huwezi ukawa ni mkristo halafu bado ni mlevi, mwasherati, mwongo, mwizi n.k.. lakini jua katika hayo mtu hahesabiwi haki mbele za Mungu kama tukitaka tuhesabiwe katika hayo hakuna mtu atakayesimama mbele za Mungu.

Kumbuka Ibilisi anawinda IMANI yetu kwa Bwana pale tunapoiweka katika matendo na sio kingine, tunasamehewa dhambi kwa imani, tunaponywa kwa imani, maombi yetu yanajibiwa kwa imani, kila jambo tunapokea kwa Mungu kwa IMANI IPATIKANAYO KATIKA NENO LAKE.

Lakini shetani anaenda kinyume kukufanya udhani utasamehewa dhambi kwasababu unashika amri kumi, au  kwa kufunga na kuomba sana ndio utapata haki ya kuponywa, n.k. Bwana amesema Waebrania 10:38 ” Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. “

Wagalatia 2:16 ” hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki. “

Waefeso 2:8-9 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;  wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. “

Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Kwa msaada wa maombi/Ushauri/ubatizo/mafundisho/Whatsapp: Namba zetu ni hizi: 

+255693036618/ +255789001312


Mada Nyinginezo:

TOFAUTI KATI YA SHERIA YA ROHO WA UZIMA NA SHERIA YA DHAMBI NA MAUTI!

KUWAHUDUMIA MALAIKA PASIPO KUJUA

KUNA TOFAUTI GANI KATI YA SALA NA DUA?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/17/nini-tofauti-kati-ya-matendo-ya-sheria-na-matendo-ya-imani/