by Admin | 11 September 2018 08:46 am09
Neno la Mungu limefananishwa na MBEGU (Luka 8:11), na siku zote mbegu ina uhai na inapopandwa ndani ya mtu, ule uhai wake unajidhihirisha ndani ya mtu huyo kulingana na umeaji wa mbegu hiyo. Hivyo kwa jinsi ile mbegu inavyoendelea kukua ndipo tabia ya Yule mtu inavyoendelea kubadilika kidogo kidogo. Kumbuka hapo sio mtu anajibadilisha kwa jitihada zake hapana bali ni ile mbegu iliyopandwa ndani yake ndiyo inayombadilisha kutoka hatua moja hadi nyingine kulingana na ukuaje wake.
Bwana Yesu alitoa mfano huu.
Marko 4: 26 “Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi;
27 akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, ASIVYOJUA YEYE.28 Maana nchi huzaa yenyewe; KWANZA JANI, tena SUKE, kisha NGANO PEVU, katika suke.
29 Hata MATUNDA yakiiva, mara atapeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika”.
Huu mfano unalinganishwa na jinsi Neno la Mungu linavyomea ndani ya mtu, kwanza linaanza kama mbegu, pale mtu anapoliruhusu lile Neno liingie ndani yake, hii inakuja kwa kutamani kujifunza kila siku Neno lile,kwa kutamani kumjua Mungu, na kujifunza maandiko, sasa kidogo kidogo, kwasababu ile mbegu imetengenezewa mazingira yanayostahili kumea yenyewe inaanza kukua taratibu taratibu pasipo hata yeye mwenye kuipanda kujijua ndio hapo unakuta mtu Yule anaanza kubadilika tabia zake na mwenendo wake, anaanza kujikuta anachukia mambo ya kidunia ambapo hapo mwanzo alikuwa hawezi, na hii haiji kwa jitihada za mtu hapana yeye mwenyewe tu anajikuta anapoteza hamu ya kufanya hivyo vitu, hapa mtu anajikuta vitu kama kiu ya sigara, pombe, uasherati, mavazi yasiyo na heshima n.k. vinakata vyenyewe, ataona tu ni kama vile kwa akili zake ameacha hayo mambo lakini hajui kuwa ni ile mbegu ambayo amekuwa akiiruhusu imee ndani yake ndiyo iliyotenda kazi ndani yake
Na kwa jinsi atakavyoendelea kuiwekea mazingira mazuri zaidi ya kukua, kwa kujifunza na kutamani kudumu zaidi katika Neno la Mungu sasa ile mbegu inageuka na kuwa JANI, hapa ni pale mtu ufahamu wake wa kumjua Mungu unaongezeka na kuwa mpana pasipo hata yeye mwenyewe kujijua kumbuka hii mbegu inachohitaji ni kuwekewa mazingira tu ya kutuzwa, kuhusu ukuaji huwa inajikuza yenyewe. Hatua hii inamfanya mtu ufahamu wake wa rohoni kuongezeka, yale mambo ambayo alikuwa hayaelewi kuhusu maandiko anaanza kuyaelewa taratibu taratibu.
Hatua inayofuata ni SUKE. Hatua hii mtu anakuwa anatoka katika ile hali ya “unyasi unaotikiswa na upepo”.
Waefeso 4: 14 “ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.
15 Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo”.
Hapa unakuwa umekomaa kutoka katika jani na kuwa suke gumu, hatua hii shetani hawezi kukuchukua tena na kila wimbi la mafundisho ya uongo kwa sababu Neno la Mungu limeshaweka mizizi migumu ndani yako. Unafika hatua ya kuwa na ujuzi wa kuitofautisha Kweli ya Neno na Uongo, kwasababu yale mafuta ya Roho yanakaa ndani yako. Mpaka hapo mtu anakuwa tayari kwa hatua inayofuata ya kuzaa matunda.
NGANO PEVU: Hii ni hatua ya kudhihirisha matunda, Hapa inatokea lile Neno lilipandwa ndani yako lenyewe linakupa uwezo wa kwenda kulipanda kwa watu wengine..na kuzaa matunda, Hapa ndipo Mungu kwa maarifa aliyoyaweka ndani ya mtu, anampa neema na uwezo wa kwenda kuwafundisha na wengine, na hii nguvu ya kufanya hivyo haiji kwa jitihada za mtu binafsi au kujilazimisha hapana bali mtu anajikuta anatamani mwenyewe kufanya hivyo kutoka ndani kwasababu ile nguvu za kuzaa matunda imeshajitengeneza ndani yake..,Ni kama tu vile mwanamke anapofikia wakati wa kuzaa, ule uchungu unapokuja hawezi kujizuia, vivyo hivyo na mtu akishafikia hatua hii, anajikuta mwenyewe anaanza kumzalia Mungu matunda.
Na hatua ya mwisho ni Mavuno: Hapa ndipo kazi ya kila mtu itavunwa na Bwana mwenyewe, na hii itakuja katika mwisho wa dunia.
Hivyo ndugu je! Ni mbegu gani imepandwa ndani yako?, Ni ya Neno la Mungu au ni ya Yule mwovu.?..Na kama ni ya Neno la Mungu, je! Mbegu hiyo imekuwa kwako katika hatua gani, ni jani?, ni suke au ni ngano?. Kama huna uwezo wa kushinda ulevi, uasherati, sigara, uzinzi, usengenyaji basi ujue ile mbegu imekufa ndani yako.. Kwasababu uliposikia Neno la Mungu hukutaka kuliwekea mazingira mazuri ya kukua lenyewe. Kumbuka mkristo yoyote anayezingatia kulitunza na kujifunza Neno la Mungu kila siku katika maisha yake, hatapata shida kuishida dhambi. Kwasababu Biblia inasema..
1Yohana 3: 9 Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao [MBEGU]wake wakaa ndani yake ; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu.
Ni maombi yangu sisi sote tujue nguvu ya Neno la Mungu, tukijua kuwa tukilipinga Neno la Mungu ndani yetu ni kujitenga na uzima wetu wenyewe. Hivyo nakutia moyo ndugu usomaye haya usichoke kujifunza Neno la Mungu kila iitwapo leo, jifunze Biblia. Kwasababu hujui wewe lile Neno linatendaje kazi ndani yako. Wewe jifunze na kulitii tu, hata kama hutaona leo mabadiliko lakini fahamu tu, linakuwa kwa njia usioijua wewe, wakati Fulani ukipita ukiendelea hivyo utaona tofauti ya leo yako na jana yako ilivyokuwa.
Mungu akubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Tafadhali share ujumbe huu kwa watu wengine na Mungu atakubariki.
Mada Nyinginezo:
NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.
ALIPO NA ATAKAPOKUWEPO BIBI-ARUSI WA YESU KRISTO.
NINI MAANA YA USIPUNGUZE WALA KUONGEZA NENO LA MUNGU?
JE! NI DHAMBI KUSHEREKEA SIKU YA KUZALIWA? BIRTHDAY!
JE! NI HALALI KWA MTU WA MUNGU KUTUMIA NJIA ZA UZAZI WA MPANGO?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/09/11/usiache-kujifunza-neno-la-mungu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.