UAMSHO WA ROHO.

by Admin | 31 January 2019 08:46 pm01

Tukisoma kitabu cha Mwanzo biblia inatuambia “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi”, pia tukirudi kusoma tena maandiko biblia inatuambie vile vile “Mungu ni Roho” (Yohana 4:24), Hivyo katika mstari huo ni sawa na kusema hapo mwanzo “Roho wa Mungu aliziumba mbingu na nchi, 2 Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.”..

Kwahiyo hapo tunaona Roho wa Mungu alifanya kazi mara mbili, katika utengenezaji wa ulimwengu. ya kwanza ni kuumba mbingu na nchi, na ya pili ni kuja kuitengeneza tena nchi ili kutimiza lengo Fulani ambalo amelikusudia, na lengo hilo si lingine zaidi ya kuifanya nchi IZAE, isibaki tena katika hali ya ukiwa. Ipo sababu kwa nini Mungu aliacha nafasi kati ya kuumbwa kwa dunia baada ya kukaa katika ukiwa wa muda mrefu na kuja kutengenezwa tena Ipo sababu.

Lakini Mungu kutujuza hayo kwa ufupi ni kutufundisha kanuni zake utendaji kazi. Na kanuni hiyo hiyo Mungu anaitumia kwa mtu yeyote anayempa Kristo maisha yake leo.

Jambo la kwanza pale mtu anadhamiria kwa dhati kabisa kutoka moyoni mwake kumpa Kristo maisha yake, kwa kutubu na kuacha dhambi zake zote, na kwenda kubatizwa katika ubatizo ulio sahihi wa kimaandiko, basi mtu huyo anakuwa ni sawa kaumbwa kwa mara ya kwanza, Roho wa Mungu anakuwa amefanya kazi yake ya kumuumba na kuwa kitu halisi kinachoonekana,. Mtu kama huyo anakuwa ameshatiwa muhuri na Roho Mtakatifu kuwa ni milki halali ya Mungu. Ni kazi ya Mungu iliyo tayari kwa matumizi yake. Lakini hawi kitu kilichokamilika mbele zake, anakuwa anafananishwa na nchi iliyokuwa imeumbwa na Roho Mtakatifu ambayo ipo katika hali ya ukiwa.

Sasa ile hatua ya pili ambayo Roho wa Mungu anatua mwenyewe juu ya nchi ya kuifanya kuwa nchi izaayo, ni jambo lingine ambalo hilo lilichukua muda kidogo tofauti na lile la kwanza la uumbaji. Hali hiyo hiyo inakuwa pia na kwa mtu aliyezaliwa mara ya pili leo.Kumbuka kama biblia inavyosema Roho Mtakatifu ni ahadi kwa wale wote watakaomjia na kumpokea:

Matendo 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 KWA KUWA AHADI HII NI KWA AJILI YENU, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.

Hii ikiwa na maana kuwa mtu yeyote yule pindi tu anapompokea Yesu Kristo kwa kudhamiria kabisa kuacha maisha yake ya dhambi na kutaka kumwishia yeye basi siku hiyo hiyo Roho wa Mungu anaingia ndani yake kuyageuza maisha yake na kumfanya kuwa kiumbe kipya, hii haichukui nguvu, wala muda, ni jambo la kudhamiria na kuzingatia maagizo yote yanayoambatana na kuamini kwako. lakini hiyo haimaanishi kuwa Roho wa Mungu atatua juu ya mtu kama huyo siku hiyo hiyo aliyoamini.. Hilo ni jambo lingine.

Ukisoma biblia utaona Bwana wetu Yesu Kristo yeye alijazwa Roho Mtakatifu tangu alipokuwa tumboni mwa mama yake, lakini Roho Mtakatifu hakuwa juu yake tangu akiwa tumboni mwa mama yake, isipokuwa alipofikisha umri wa miaka 30, na ndivyo ilivyokuwa kwa Yohana Mbatizaji, yeye pia alijazwa Roho tangu akiwa tumboni mwa mama yake lakini Roho Alimfuata nyikani miaka mingi baadaye.. Vivyo hivyo na mitume wote wa Yesu Kristo, pale Bwana alipowachagua, siku ile wote walipochukua uamuzi wa kumfuata Bwana na kuacha mambo yao yote maovu na njia zao, na kazi zao, na familia zao kwa ajili ya Bwana, na kubatizwa walipokea Roho Mtakatifu ndani yao, ndiye aliyewapa uwezo wa kustahimili mambo yote kwa kipindi chote walichokuwa wanakipitia na Bwana. Lakini Roho Mtakatifu kuja juu yao haikuwa siku ile ile ni kitendo kilichowachukua muda wa miaka mitatu na nusu baadaye..

Kwasababu Kitendo cha Roho wa Mungu kutua juu ya mtu, ni lazima kwanza mtu ajue ni kwasababu gani Roho huyo aje juu yake, kwahiyo hakiji kiuwepesi kama kile cha kwanza cha kufanywa kuwa kiumbe kipya, bali hichi kinakuja kwa makusudi maalumu, hivyo yule atakaye kipokea ni sharti kwanza ayatambue makusudi hayo ni yapi na ndio hapo itamgharimu mtu apitie huyo hata madarasa Fulani fulani, ya kutosha pamoja na kuomba sana bila kukata tamaa kwa ajili ya Roho.

Na makusudi hayo tunayaona ndio kama yale Roho Mtakatifu alivyotua tena juu ya nchi tena, nayo si mengine zaidi ya kuifanya nchi IZAE na iwe mahali pa KUISHI wanadamu.

Na ndivyo itakavyokuwa pale Roho wa Mungu atakapotua juu ya mwamini baada ya kukamilishwa, atamfanya mtu huyo kuwa ni chombo cha kuzaa zaidi na cha kuhudumia kundi lake ziadi ya matakwa ya mtu binafsi. Tunaona mara baada ya Bwana kushukiwa na Roho juu yake ndio tunaona tangu huo wakati na kuendelea akaanza kuleta uamsho Israeli yote na dunia nzima, kadhalika ndivyo ilivyokuwa kwa Yohana mbatizaji na mitume wa Yesu Kristo siku ile ya Pentekoste. Kwasababu Roho ameshawatia mafuta na kuwafanya kuwa nchi izaayo kwa ajili ya kusudi lake.

Vivyo hivyo na sisi hatupaswi kuridhika na mahali tulipo, ni kweli tulipompa Bwana maisha yetu na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kimaandiko tulitiwa muhuri kwa Roho wake, tulizaliwa kwa Roho mtakatifu, tulifananishwa na nchi iliyoumbwa hapo mwanzo na Roho wa Mungu,lakini hiyo haitoshi kwasababu tukiendelea kubakia hivyo hivyo tutazidi kuwa katika hali ya UTUPU na UKIWA. Yatupasa sisi sasa tuongeze bidii katika kumwomba Mungu na kumtafuta Roho Mtakatifu kwa nguvu zetu zote, ili alete uhai katika kanisa lake kupitia sisi, alete uamsho tena katika kanisa lake kupitia sisi, auondoe ukiwa uliopo sasa duniani, inatupasa kila siku usiku na mchana tumwombe Mungu amlete Roho Mtakatifu aipindue tena dunia.

Kumbuka hatuzungumzii kumwomba atende miujiza na ishara hapana bali alete mageuzi katika kizazi chetu kama aliyoyaleta pale alipoitia mafuta nchi tena..kumbuka mitume walikuwa wanatenda miujiza hata kabla ya siku ya Pentekoste lakini biblia haitupi rekodi ya tunda lolote walilofanikiwa kulileta siku zote walizokuwa wanazunguka kufanya miujiza isipokuwa walipofikia kipindi cha Pentekoste, Roho wa Mungu aliposhuka juu ya kanisa na kuanza kuchoma mioyo ya watu,hapo ndipo badiliko kubwa lilionekana (yaani ndani ya siku moja waliokoka watu zaidi ya elfu 3), Nguvu hizo za uamsho ndizo tunazozihitaji siku za leo.

Embu fuatilia ushuhuda huu naamini na sisi utatupa jambo la kujifunza kwa kupitia hili.

EVAN ROBERTS.

Ni kijana aliyezaliwa katika nchi ya Wales huko bara la Ulaya mwaka 1878, Ni muhubiri mashuhuri sana anayejulikana katika vitabu vya historia za kidini, aliyesifika kwa kuletea uamsho mkubwa sana huko nchini Wales mwaka 1904-1905.

Inarekodiwa kuwa Evan tangu enzi za utoto wake alikuwa ni kijana aliyependa sana kuhudhuria kanisani , na aliyekuwa anakariri mistari mingi ya biblia. Ni kijana mdogo aliyejulikana kwa kutumia masaa yake mengi katika maombi binafsi hususani wakati wa usiku akimwomba Roho Mtakatifu ampe moyo usiogawanyika, na pia alijumuika katika vikundi vya maombi na watu wengine, Evan anasema alikuwa anamwomba Roho Mtakatifu kwa zaidi ya miaka 11 aitembelee tena Wales kwa nguvu ya uamsho wa kipekee watu wengi wamgeukie Mungu. Anasema tangu huo wakati alikuwa anaweza kukaa usiku kucha akitumia muda wake mwingi kusoma, na kuzungumzia tu habari za uamsho . Evans alikuwa akiungana na vijana wenzake wengine wakiomba juu ya uamsho wa Roho uje katika kijiji chao.

Mpaka ilipofikia wakati Mungu kusikia sauti yao, Mungu alileta Roho ya Mageuzi makubwa katika nchi ile ndogo ya Wales, watu ghafla wakawa wanachomwa na mafundisho ya Evan katika kanisa dogo alilokuwa anasali, watu wakaanza kumgeukia Mungu, hata wale ambao waliokuwa vuguvugu, kwa kuhudhuria tu mikutano ile katika kanisa lile dogo watu wote walikata shauri kwa moyo mmoja na kumgeukia Mungu kwa dhati kabisa, watu waliomtafuta Mungu waliongeza kwa haraka sana mikutano mingi ikaanza kupangwa katika miji mingine,na vijiji vingine na wote waliokuwa wanasikia walichomwa mioyo na kujihisi kumrudia Mungu wao kwa mioyo yao yote.

Magazeti na vyombo ya habari vikaanza kurekodi, badiliko kubwa la watu kumgeukia Mungu katika mji ule, watu walikuwa wanawahi kufunga maduka yao kabla hata ya wakati wao wa kawaida wa kufunga ili tu wawahi ibadani za kila siku jioni, makanisa yalijawa na watu mpaka yakawa hayana nafasi tena ya kuwahifadhi watu wanaofika makanisani, watu wanasimama nje, watu ambao walikuwa watukanaji, barabarani walikuwa wakitembea na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, Uhalifu ulishuka kwa asilimia kubwa sana katika mji wa Wales, hata mabaa mengi yaliyokuwa mashuhuri ya kuuza pombe yalifungwa kwa kukosa wateja, kwasababu mji mzima ni kama ulipigwa butwaa hata wakuu wa nchi walishangaa nchi ile imekumbwa na nini kwa uamsho mkubwa namna ile ulioletwa kijana mdogo tu Evan Roberts pamoja na vijana wenzake.

Kwa kipindi kisichozidi miezi 9, zaidi ya watu 150,000 katika nchi ile ndogo walitubu na kugeuka Mungu kabisa na kuwa wakristo waliosimama mbele za Mungu, uamsho ule ulizidi kuendelea mpaka nchi jirani za Wale.Jambo hilo lilimfanya Evan kuwa mtu maarufu sana duniani kwa wakati ule, Lakini Uamsho ule ulidumu kwa muda wa miezi 9 tu.(Mwaka 1904-1905).

Sasa hiyo yote ilikuja kutokana na maombi yasiyokoma ya Evans Roberts kwa ajili ya nchi yake. Vivyo hivyo na sisi, tunapokuwa wakristo haitoshi tu kusema Roho Mtakatifu ni wa kwangu tu peke yangu, yatupasa tuingie katika kuliombea kanisa , na kuwaombea wengine Mungu mwenyewe alete Roho ya mageuzi alete UAMSHO mpya katika jamii zetu ili watu waokolewe. Mungu aachilie Roho ya kuwavuta wengi kwake..Na tukiwa watu wa tabia hiyo basi hata siku hiyo ikifika, Mungu atakapoleta UAMSHO huo atatupa sisi kipaumbele cha kwanza kuwa vyombo vyake vya kuokoa watu, kuliko tukikaa tu hivi hivi..

Na ndio maana Bwana Yesu alisema:

Na ndio maana Bwana YESU alitoa mfano huu na kusema:

Luka 11.5 “Akawaambia, Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu,

6 kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake;

7 na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe?

8 Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.

9 Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.

10 Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.

11 Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?

12 Au akimwomba yai, atampa nge?

13 Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa ROHO MTAKATIFU HAO WAMWOMBAO?”.

Unaona hapo?. Mistari hiyo inatupa picha kuwa kumbe Roho mtakatifu sio ahadi tu kwa yeyote aaminiye bali pia anapaswa kuombwa, tena kwa kurudia rudia, bila kukata tamaa, Kama Bwana Yesu alivyokuwa, mtu wa dua sana na maombi kama biblia inavyosema katika Waebrania 5:7 Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu;

Unaona hapo? Aliendelea hivyo hivyo Mpaka siku ile Roho wa Mungu aliposhuka juu yake na kumtia mafuta zaidi ya watu wote duniani, siku hiyo ndiyo alipoachwa kuitwa YESU, na kuitwa YESU KRISTO. Nasi tunaona UAMSHO wake jinsi ulivyoleta madhara makubwa mpaka sasa katika vizazi vyetu.

Hivyo ni wajibu kwa kila mkristo anayeihurumia jamii yake na anayetaka jamii yake iokolewe, anayelipenda taifa lake liokolewe anayependa watu wengi waokolewe kuomba bila kukata tamaa Bwana ampe Roho Mtakatifu kwa lengo la kuzaa. Kwa lengo la kuleta Mageuzi, kwa Lengo la Uamsho,. Na kwakuwa yeye mwenyewe kashasema ikiwa sisi waovu tunaweza kuwapa watoto wetu vipawa vyema pale wanapotuomba je! si zaidi sana Baba yetu aliyembinguni?

Luka 18:7 “Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?8 Nawaambia, atawapatia haki upesi;” Hivyo sisi sote tuanze sasa, kuomba juu watu kuokolewa kwa bidii zote. Na Bwana atatusikia na kutujibu kwa wakati wake.

Bwana akubariki sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/01/31/uamsho-wa-roho/