MAOMBI KWA WENYE MAMLAKA.

by Admin | 27 April 2019 08:46 pm04

1 Timotheo 2 : 1-4

“1 Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote;

2 kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu.

3 Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu;

4 ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli”.

Shalom Mtu wa Mungu, karibu tujifunze maandiko, na leo kwa Neema za Mungu tutajifunza juu “Umuhimu wa kuombea wenye mamlaka”.

Biblia inasema katika Warumi 13:1

“Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.

2 Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.

3 Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake;

4 kwa kuwa yeye NI MTUMISHI WA MUNGU KWAKO KWA AJILI YA MEMA. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.

5 Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri”.

Katika mistari hiyo Mtume Paulo anajaribu kutueleza kwa uweza wa Roho kuwa watu wenye mamlaka ni watumishi wa Mungu,..sasa kuna utumishi wa Mungu wa aina mbili, wa kwanza na wa umuhimu ni ule wa KUHUDUMU KATIKA KAZI YAKE, Yaani kazi ya kuhubiri injili kwa kupitia karama alizoziweka ndani ya kanisa. Huo ndio utumishi wa Mungu wa Kwanza na wenye hadhi ya juu, na wenye thawabu kubwa kuliko zote.

Lakini pia upo utumishi usio wa madhabahuni, huo Mungu kauweka kwa ajili ya kuwapatia mema watu wake na kuwahukumu waasi…Kwa mfano vyombo vya dola, hivyo havihubiri injili ya wokovu lakini ni vyombo vilivyoruhusiwa na Mungu kuwepo ili kukomesha uasi na matendo mabaya katika jamii, n.k. Sasa leo hatutaingia kwa undani kuelezea juu ya utumishi huu, lakini tutajifunza kwa ufupi umuhimu wa kuwaombea wenye mamlaka.

Biblia imetuambia tuwaombee wenye mamlaka, naamini haikumaanisha tuwaombee matatizo yao binafsi, au shida zao binafsi, au mahitaji yao binafsi…ingawa hakuna ubaya wowote kufanya hivyo, sio dhambi ni vizuri pia kufanya hivyo, lakini naamini biblia haikumaanisha hivyo…bali ilimaanisha tuziombee zile nafasi walizopo kwamba zitumike katika njia inayopasa ili sisi tuishi kwa amani…

Kwamfano nafasi ya Uraisi inapaswa iombewe kwamba kila mipango yoyote isiyofaa ya yule adui isipate nafasi katika kiti kile, kwamba kwa yeyote aliyekikalia kile kiti iwe ni mwanamke au mwanamume, Bwana akafunike fikra zake atawale kulingana na mapenzi ya Mungu shetani asipate nafasi.

Kadhalika na katika nafasi zote iwe ni za wizara kwamfano wizara za fedha,afya, maliasili n.k au vinginevyo..zote hizo zinatakiwa ziombewe, kwamba shetani asipenyeze vitu vyake katika hizo nafasi zikatumika vibaya…kwasababu endapo zisipoombewa na shetani akapata nafasi basi matatizo yatatukuta sote, hususani kwetu sisi tunaoamini, kwasababu sisi ndio tageti kubwa ya shetani..

Hebu jaribu kufikiria, leo vita vitokee, mabomu yakapigwa huku na kule, barabara zikaharibika, miundo mbinu ya maji na umeme ikaharibika…unadhani na wewe mtu wa Mungu utaacha kuathirika kwa namna moja au nyingine?..utaathirika tu!

Kwasababu na wewe unahitaji barabara kwenda kazini kwako au kwenda kuhubiri, unahitaji umeme kuendesha biashara yako kama unayo, unahitaji maji kwa ajili ya kuishi, n.k sasa hivyo vyote vimeharibika unadhani na wewe utaacha kupata shida hata kama unamtumainia Mungu?..Ni kweli Bwana anaweza akakuhifadhi wewe kupona lakini kwa shida sana! Katika wengi watakaokufa kwa matatizo hayo unaweza usiwe mmoja wao kwasababu unamcha Mungu, lakini utakuwa katika dhiki nyingi…Nuhu alisalimika kwenye gharika lakini maisha ndani ya gharika hayakuwa ya raha kabisa..kukaa miezi mitano kwenye boti, ndani giza, hakuna kutembe tembea..wewe ni kitandani, kwenye kiti na kusikia sauti za wanyama tu, na watu wale wale uliowazoea! Yalikuwa ni maisha ya shida ingawa kasalimika.

Unakumbuka wakati wa Wana wa Israeli kuchukuliwa utumwani Babiloni? Kitu gani kilitokea?.. kabla ya kuchukuliwa mji ulizungukwa na majeshi ya Babeli kwa muda wa miaka 2, hakuna kutoka wala kuingia,chakula chote ndani ya mji kikaisha, njaa ikawa kali mno, na hiyo njaa iliwaathiri hata watu wa Mungu waliokuwemo ndani ya huo mji.

Mfano Nabii Yeremia alikuwepo ndani ya huo mji! Kuna wakati walimshika wakawa wanampa mkate mmoja tu kwa siku!…tengeneza picha Nabii wa Mungu, ambaye Mungu alimwambia “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.Yeremia 1:5”..Nabii wa mataifa!! Lakini leo hii anashindia mkate mmoja tu kwa siku, kwa kipindi kirefu.

Na tunaona baada ya miaka miwili kuisha, watu wakazidiwa njaa ndani ya mji ikabidi mfalme atafute njia ya kutoroka, siku hiyo hiyo ndio majeshi ya Babiloni yalipoingia ndani ya mji na kuwaua watu kama kuku..walikufa wayahudi wengi sana..na kibaya zaidi wachache waliosalia walichukuliwa mateka mpaka Babeli..Na Nabii Ezekieli alikuwa ni miongoni mwa waliochukuliwa mateka pamoja na Nabii Danieli…

Hebu fikiria Nabii wa Mungu Ezekieli aliyeonyeshwa na Mungu maono makubwa kama yale, na yeye anakuwa ni miongoni mwa mateka wale! Waliofungwa minyororo na kupelekwa utumwani! Na Danieli naye vivyo hivyo..sasa kama manabii wa Mungu yaliwakuta hayo pale nchi yao ilipovurugika unadhani yataachaje kutukuta mimi na wewe endapo nchi tunazoishi zitachafuka?!!…Ni wazi kuwa tutateseka tu! Hakuna namna! Inaweza isiwe kwa kiwango kikubwa kama watu wasiomjua Mungu, lakini tutateseka tu!

Ndio maana Paulo anasema…

“1 Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote;

2 kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu”.

Unaona hapo! Nia na madhumuni ni ili tuishi maisha ya Amani na Utulivu…Tusipoishi kwa amani hata Injili tutaihubiri kwa tabu, kama hakuna utulivu hata raha ya kuishi hakuna.

Biblia inatabiri, amani ya dunia kuvurugika, hiyo ni lazima itokee, lakini sio kabla ya unyakuo kutokea! Baada ya unyakuo kupita ndio mambo yote ya ulimwengu yataharibika, itakuja dhiki kuu juu ya nchi ambayo haijawahi kutokea mfano wake,lakini kabla ya unyakuo mambo hayo hayatatokea..utatokea utungu tu! Lakini sio uhalisia wa mambo yenyewe, kutatokea matetesi ya vita lakini sio vita vyenyewe..kama tunavyoona sasa, kuna matetesi ya vita mahali na mahali, hiyo ni kuonyesha kuwa tunaishi katika siku za kumalizia.

Kwahiyo ni wajibu wetu kuombea nafasi zote za uongozi, ili shetani asipate nafasi, na ili tuishi kwa amani katika hichi kipindi cha kumalizia, Na kumbuka shetani anapojaribu kushambulia hizi nafasi lengo lake kubwa si kuiletea dunia dhiki!! Hapana bali lengo lake kubwa ni kuwaletea Wakristo dhiki!..ndio maana Paulo anasema “ili tuishi kwa amani na utulivu”..sio “ili dunia iishi kwa amani” bali ili sisi (tulioamini-wakristo) tuishi kwa amani na utulivu. shetani siku zote hatafuti kuwatesa walio wake, bali wasio wake, anawawinda wakristo kuliko kitu chochote kile! Anawachukia kuliko!..

kwahiyo atatafuta kila njia ya kuwaangamiza, na njia mojawapo ndio hiyo kuvuruga ngazi za juu za mamlaka…utasikia leo, sheria imetoka hakuna kuhubiri mabarabarani, wala kwenye mabasi, unadhani hilo ni jambo la kawaida kwa kiongozi kusema hivyo kama sio roho ya ibilisi nyuma yake inamwendesha?. kesho utasikia hakuna ruhusa ya kujenga kanisa,..baada ya siku kadhaa utasikia mswada bungeni hakuna ruhusa ya kuhubiri kama hujapitia chuo Fulani cha biblia n.k hiyo yote ni mipango ya ibilisi kutumia ngazi za juu za utawala kupunguza nguvu za wakristo, na Injili ya Mungu kusonga mbele. Ndio maana dua na sala ni muhimu sana juu ya nafasi hizo ili shetani asipate nafasi.

Kwahiyo kila unaposali mtu wa Mungu, usisahau kuziombea hizi ngazi za utawala, kuanzia ngazi ya Uraisi mpaka ngazi ya mtendaji wa kata, mpaka ya balozi wa nyumba kumi. Zote hizo Bwana azifunike, na azilinde dhidi ya mipango yote ya Yule adui.

1 Timotheo 2 : 1-4  “1 Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote;

Bwana akubariki sana.

Tafadhali “share na wengine” Maran atha!

Mawasiliano: +255693036618 / +255789001312

Na pia kama utapenda masomo haya yawe yanakufikia kila siku kwa njia ya Whatsapp. Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

Sadaka ya Amani ilikuwaje?

Sadaka ya kutikiswa ilikuwaje?

Birika ni nini?, na yale Matao matano katika birika la Bethzatha ni nini?.

FAIDA ZA MAOMBI.

MAOMBI YA YABESI.

RABONI!

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?


Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/04/27/maombi-kwa-wenye-mamlaka/