by Admin | 22 May 2019 08:46 am05
Shalom, Mwana wa Mungu karibu tujifunze maandiko…Leo tutajifunza kwa Neema za Bwana namna ya kuokoa roho.
Bwana Yesu alisema “sikuja kuziangamiza roho bali kuziokoa (Luka 9:56)” sentensi hiyo aliisema baada ya wanafunzi wake kumwomba ashushe moto uwaangamiza wale watu wa Samaria waliokataa kumpokea…Lakini kwanini alisema vile kuwa hakuja kuziangamiza bali kuziokoa?…ni kwasababu alikuwa na uwezo wa kuziangamiza lakini hakutaka kufanya vile..kinyume chake alitafuta namna ya kuwafikishia wokovu na sio kuwaua.
Wakati mwingine tunaweza tukawa na silaha mikononi mwetu au midomoni mwetu tulizopewa na Mungu kihalali kabisa za kujeruhi na kuangusha watu wote wanaokwenda kinyume na sisi..lakini tukikosa hekima kama aliyokuwa nayo Bwana tutajikuta tunaangamiza roho badala ya kuokoa.
Hebu mtafakari Musa, wakati wana wa Israeli wanamkosea Mungu kule jangwani…Mungu alimwambia Musa ajitenge na wale watu ili apate kuwaangamiza…na atamfanya Musa kuwa Taifa kubwa, atampa uzao utakaoirithi nchi….ingekuwa ni mmojawapo wa sisi tungesema asante Mungu, kwa kuwa umeteta nao wanaoteta nami, lakini tunaona Musa, alilipindua wazo la Mungu na kuanza kuwaombea msamaha ndugu zake na kuwatafutia upatanisho na Mungu, na Mungu akalisikiliza ushauri wa Musa na kughairi mawazo yake…
Sasa tuchukulie mfano Musa, angekubali kujitenga nao, unadhani, kulikuwa kuna kosa lolote pale? hapana Mungu kweli angewaangamiza wale watu na angeenda kumfanya Musa kuwa Taifa kubwa kama alivyomwahidia..Lakini Musa angekuwa hajatenda kwa busara mashauri yale yalitoka kweli kwa Mungu, angekuwa hajastahili kuwa kiongozi bora kwasababu hakuizuia ghadhabu ya Mungu juu ya watu wake. Kwahiyo pengine hata Mungu asingemtukuza Musa kwa kiwango hichi alichomtukuza sasa.
Kutoka 32:9 “Tena Bwana akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu
10 basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu.
11 Musa akamsihi sana Bwana, Mungu wake, na kusema, Bwana, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu?
12 Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako.
13 Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele.
14 Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake”.
Kwahiyo hiyo inatufundisha kuwa siyo kila fursa au mamlaka tunayopewa na Mungu, tuyatumie tu bila kutafakari vizuri..Mungu wetu hajatuumba kama maroboti kwamba yeye ni wa kusema na sisi ni wakufuata tu pasipo kutafakari..hapana! huo ni utumwa na sisi sio watumwa sisi ni wana, tunazungumza na Baba yetu na kushauriana naye…ametuumba tuzungumze naye, tusemezane naye, tupeane naye mashauri.
Isaya 1: 18 “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”.
Ndio maana Musa alisemezana na Bwana na akasafisha dhambi za wana wa Israeli zilizokuwa nyekundu kama bendera, na akazifanya kuwa nyeupe kama sufu. Haleluya!
Mungu anaweza kumweka mtu anayekuchukia, au anayekupiga vita mikononi mwako, au mtu ambaye alikufanyia visa Fulani, ukapata madhara fulani…Mungu anaweza kumweka mikononi mwako kiasi kwamba ukisema tu neno moja umemmaliza, au ukifanya jambo Fulani tu, habari yake imekwisha ikawa ni kweli Mungu kamtia mikononi mwako ili kumlipizia kisasi, kwa ubaya aliokufanyia….kama vile Mungu alivyomtia Sauli mikononi mwa Daudi..akajua kabisa hii ni fursa ya kummaliza lakini hakufanya hivyo…nasi pia huo usiwe wakati wa kummaliza, badala yake uitumie fursa hiyo kumgeuza kwa Kristo, huo ndio wakati wa kusemezana na Bwana juu ya dhambi zake zote, na kumwombea Msamaha…hakika ukifanya hivyo na kuigeuza hasira ya Bwana, Bwana atakupenda zaidi ya anavyokupenda sasa…atakutukuza zaidi ya anavyokutukuza sasa…
Utasema hiyo habari ya Musa na Daudi ilikuwa ni ya agano la kale, vipi kuhusu agano jipya, je! Kuna mtu yeyote alishawahi kufanya hivyo..Jibu ni ndio! Hata katika agano jipya tunayo hiyo mifano.
Tunasoma habari za Paulo na wenzake, wakati mmoja walipokwenda Makedonia kuhubiri, walikutana na mtu mwenye pepo na walipomtoa Yule pepo, ndipo wakuu wa mji wakawakamata na kuwachapa bakora na kisha kuwatupa gerezani.
Sasa lile jambo halikumpendeza sana Mungu, na hivyo Bwana akawatengenezea njia ya kutoka mule gerezani, akamtuma malaika wake usiku ule wakati Paulo na Sila walipokuwa wanamsifu Mungu, ghafla vifungo vikalegea na milango ya gereza ikafunguka…sasa Lengo la Yule malaika kufungua milango ya gereza haikuwa tu kuwafurahisha wale watu , hapana ilikuwa ni ili Paulo na Sila watoke!!, waondoke mule gerezani,..Kama vile Yule malaika alivyomtoa Petro gerezani wakati Fulani alipokuwa amefungwa.
Lakini tunasoma Paulo na Sila walilitengua agizo la Bwana, badala ya kutoka na kwenda zao, waliendelea kukaa mule gerezani japokuwa Mungu aliwafungulia mlango wa kutoka…lakini walitafakari mara mbili mbili, endapo tukitoka na kwenda zetu tutakuwa kweli hatujatenda dhambi lakini tutaacha madhara makubwa huku nyuma, tutasababisha kifo badala ya kuokoa roho, na zamani zile utawala wa Rumi, mfungwa yoyote akitoroka kinachobakia kwake ni kifo tu, na ndio maana Yule askari ilikuwa nusu ajiue, lakini Paulo na Sila wakamzuia.
kwahiyo wakaitumia ile nafasi sio kwa faida yao bali kwa faida ya wengine, ndio tunaona wakaenda kumwuhubiria Yule askari injili pamoja na familia yake wote wakaokoka, na mwisho wa siku kesho yake asubuhi wakatolewa gerezani, kwahiyo ikawa faida kwao mara mbili.
Matendo 16: 22 “Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora.
23 Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana.
24 Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale.
25 Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.
26 GHAFULA PAKAWA TETEMEKO KUU LA NCHI, HATA MISINGI YA GEREZA IKATIKISIKA, NA MARA HIYO MILANGO IKAFUNGUKA, VIFUNGO VYA WOTE VIKALEGEZWA.
27 Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia
28 Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa.
29 Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila;
30 kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka?
31 Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.
32 Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake.
33 Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati uo huo.
34 Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu.
35 Kulipopambauka makadhi wakawatuma wakubwa wa askari wakisema, Waacheni watu wale waende zao.
36 Yule mlinzi wa gereza akamwarifu Paulo maneno haya akisema, Makadhi wametuma watu ili mfunguliwe; basi, sasa tokeni nje, enendeni zenu kwa amani”.
Sasa hebu fikiri endapo Paulo na Sila wangeondoka usiku ule mule gerezani, na kusema safi sana! Mungu katupigania! Kawaaibisha maadui zetu!…. ni wazi kuwa wangeshampoteza Askari na kusudi la wao kwenda makedonia lingekuwa ni sifuri kwa maana wenyewe walikwenda kwa nia ya kuhubiri injili, na sasa hapa ni sawa na wamemsababishia wengine mauti.
Kwahiyo ndugu tunajifunza, sio kila fursa ya kumpiga adui yako ni mapenzi kamili ya Mungu, sio kila mlango Mungu anaokufungulia ni wa kuutumia pasipo kutafakari, aliyekutukana, aliyekuaibisha, aliyekupiga, aliyekunyima kazi wakati Fulani tena akakufanyia na visa juu, aliyekurusha, aliyekuharibia mipango yako na maisha yako, sasa Mungu kamleta mikononi mwako..huo sio wakati wa kuitumia hiyo fursa Mungu aliyokuwekea mbele yako pasipo hekima!! Itumie hiyo KUOKOA ROHO, BADALA YA KUANGAMIZA. Hicho ndio kitu Mungu anachotaka kuona kwetu!.
Kuna muhubiri mmoja, ambaye alikuwa ni Nabii, siku moja wakati anahubiri kanisani kwake malaika wa Bwana alimwambia atazame mwisho kabisa wa kanisa, na alipotazama akaona watu wawili kwa mbali mwanamume na mwanamke wanafanya kitendo kichafu cha kunyonyana ndimi na hiyo ilikuwa ni katikati ya ibada…Yule muhubiri akakasirika sana, akawa anawaendea…wakati yupo njiani anawaendea Yule malaika aliyemwambia atazame nyuma ya kanisa, huyo huyo akamwambia sema Neno lolote na mimi nitalitimiza hilo neno saa hivi hivi kama ulivyosema…yaani maana yake angesema “Bwana naomba waanguke sasa hivi wafe, wangekufa saa ile ile”..na alipofika pale Yule muhubiri..kitu fulani kikamwingia ndani yake, kama huruma Fulani hivi… akasema “nimewasamehe”…Baadaye alivyomaliza ibada, sauti ikazungumza ndani ya moyo wake na kumwambia..”hicho ndio nilichokuwa nataka kusikia kutoka kwako”…msamaha…
Ni wazi kuwa hao watu kwa msamaha huo, baadaye walitubu na kumgeukia Mungu kwa kumaanisha.
Umeona? Epuka injili unazohubiriwa kila wakati piga adui yako, usiposamehe kuna wakati nawe utafika utamkosea Mungu, naye Mungu hatakusamehe.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Kwa Maombezi, Ushauri, au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba
+225693036618/ +225789001312
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/05/22/okoa-badala-ya-kuangamiza/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.