Je! Kushiriki au kujihusisha kwenye michezo ni dhambi?..

by Admin | 2 September 2019 08:46 pm09

SWALI: Kama vile kutazama mpira (simba na yanga), au kucheza mipira ya kikapu n.k?

JIBU: Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa vimtokavyo mtu ndani ya moyo ndivyo vinavyomfanya kuwa najisi..Chochote mtu anachokifanya, au anachojihusisha nacho kinachomsababishia moyoni mwake kutoke ugomvi, ubishi, mashindano, hasira,matusi kitu hicho tayari ni najisi kwake…Biblia inasema.

Wafilipi 2: 3 “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake’’.

Swali je! Kuna mchezo wowote ambao ukiufuatilia haukupeleki kwenye mashindano(malumbano)?…kushindana mpaka wakati mwingine kutukana na kufanyiana mizaha. Kama upo basi huo sio najisi kwako. Biblia pia inasema… 

Wafilipi 2: 14 ‘’Yatendeni mambo yote pasipo manung’uniko wala mashindano, 

15 mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu’’. 

Jiulize kuna mchezo wowote ambao ukishaisha haukupeleki kwenye manung’uniko?..yaani kuwanung’unikia wahusika wa huo mchezo, au kumnung’unikia mwenzako? Neno linasema hapo, ‘’ambao kati yao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu’’…sasa ni mwanga gani utakaoonesha endapo ukiwa ni mshabiki, au mtu wa manung’uniko, au mtu wa mizaha, au mbishi, na mtu wa mashindano? Ni kitu gani hapo kitakachomfanya mtu asiyeamini avutiwe na Imani yako?…

Jiulize tangu uanze kuwa mshabiki wa mpira kuna mtu yeyote alishawahi kuokoka alipokutazama wewe wakati unaangalia mpira, au wakati wa wewe kumaliza kuangalia mpira? Au wakati magoli yanapofungwa?..kama ulishawahi kumbadilisha mtu kwa njia hiyo, basi kwako michezo sio najisi…Lakini kama bado ujue kuwa ni dhambi kujihusisha nayo. Hebu fikiria endapo Bwana Yesu yupo duniani angekuwa ni mshabiki wa mchezo Fulani, akishamaliza kuhubiria makutano anakwenda viwanjani kutazama michezo na akitoka hapo anashindana na wanafunzi wake kuhusu ule mchezo, tungewezaje kumwelewa?..angekuwa anatuchanganya…

Na sisi hatupaswi kuwachanganya watu walio nje ya Imani yetu. Wanapaswa wavutiwe na mienendo yetu ili watoke huko na kuja huku tuliko (2 Timotheo 2:24). Swali la mwisho kabisa la kujiuliza, ni juu ya muda unaotumia katika kushabikia au kuangalia hiyo michezo, jitathimini muda unaotumia kutazama hiyo michezo, ulinganishe na muda unaotumia kusali au kuomba au kusoma Neno. Kama unatumia dakika 10 kuangalia michezo na unatumia masaa matano au Zaidi kusoma Neno, basi ni wazi kuwa Michezo sio kitu kilichochukua nafasi moyoni mwako, na kinaweza kisiwe na madhara kwako, lakini kama unatumia masaa mawili kutazama michezo na Neno la Mungu au sala unatumia dakika tano au husali kabisa Hiyo ni Ashera ndani ya moyo wako, hivyo unaishi Maisha ya dhambi.

Kama kwenye ibada unasinzia halafu kwenye michezo unachangamka hilo Ashera kwako, Kama kwenye michezo unaouwezo wa kupiga kelele kwa nguvu kwa ujasiri wote, mpaka mtaa wa pili wanasikia halafu, ibadani kumsifu Mungu unaona aibu unanong’ona kwa sauti ya chini, ni machukizo mbele za Mungu. Kwahiyo kwa ujumbla michezo yote inayozaa magomvi, chuki, matusi, hasira, uchungu,mizaha,mafarakano, utani mbaya, vinyongo, manung’uniko, mashindano,visasi, vita, makwazo, tamaa, ulevi,wizi n.k..Yote ni kutoka kwa yule Adui kwahiyo ni dhambi kujihusisha nayo.

 Ubarikiwe.

Kwa mawasiliano/mafundisho zaidi kwa njia ya whatsapp, tutumie ujumbe kwenye
namba hizi: +255789001312/ +255693036618


Mada Nyinginezo:

KUCHEZA KARATA NI SAHIHI KWA MTU ALIYE MKRITO?

JE! UMEYABATILISHA MAMBO YA KITOTO?

INJILI YA MILELE.

KITABU CHA UKUMBUSHO

KWANINI USIICHAGUE TUZO ISIYOHARIBIKA?

KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/02/je-kushiriki-au-kujihusisha-kwenye-michezo-ni-dhambi/