Je! tunaruhusiwa kumuombea mtu ambaye haweki bayana kile anachohitaji kuombewa?

by Admin | 2 September 2019 08:46 pm09

SWALI: Je! Kwetu SISI WATAKATIFU mtu akikuambia umuombee anaTATIZO halafu ukimuuliza ni tatizo gani asikuambie tatizo(Anasema hilo ni siri yake moyoni)-Huyo Tumuombee hilo tatizo lake la siri yake moyoni au?? Karibuni wapendwa..


JIBU: Kuna maombi ya kuombeana sisi kwa sisi ambayo hayahitaji mtu kumuhadithia mwingine ili amwombee, kwamfano kumwombea ndugu yako, Mungu amlinde na Yule mwovu, Mungu asimsahau katika ufalme wake, Mungu ampe kuokoa, Mungu ampe afya njema, Mungu amsaidie asimame katika imani asitetereke, Mungu ampe Amani na Upendo, mafanikio n.k..hayo ni maombi ambayo kila siku tunatakiwa tuyatamke kwa ndugu zetu wote wa mwilini na rohoni, Ndio jambo ambalo Mtume Paulo pia alikuwa analifanya:

Wakolosai 1:9 “Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, HATUACHI KUFANYA MAOMBI NA DUA KWA AJILI YENU, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni;

10 mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu;’’ 

Lakini yapo mahitaji mengine ambayo ni LAZIMA mtu AYANENE kwa faida yake mwenyewe, kama amedhamiria kuhitaji msaada kutoka kwa wengine. Kama mtu anayehitaji kuombewa tatizo Fulani linalomsumbua halafu haweki bayana hitaji hilo, nguvu ya kuombewa itatoka wapi, ni wazi kuwa anajizuilia Baraka zake yeye mwenyewe.

Biblia inaposema tuchukuliane mizigo, inamaanisha kuwa tusaidiane kwa kuitambua mizigo ya wenzetu, ukubwa wake, na uzito wake, ili mtu ajue ni jinsi gani kwa sehemu ya neema aliyopewa atamsaidia kuubeba, lakini kama mzigo kauficha mwenyewe ndani yake, wale wengine hata wakimwombea hawataomba ipasavyo, kwasababu hawatajua ukubwa au uzito wa tatizo lenyewe. 

Jaribu kufikiria labda mtu ana ugonjwa ambao unamsumbua kwa muda mrefu, halafu hataki kuwaambia watu wanaomwombea kuwa anaumwa yeye anasema niombeeni tu..wale watu kweli wataomba pamoja naye lakini hiyo itaishia pale pale, lakini kama mfano kama angeweka bayana kuwa anasumbuliwa na ugonjwa Fulani (akautaja jina) na ameshahangaika muda mrefu bila matumaini yoyote, sasa kwa kuzungumza tu vile tayari katika roho anauchukua ule mzigo wake na kuwapa wengine, ndio hapo inatokea wale wenzake wanaguswa sana na shida yake, huruma zinawajaa ndani, wanaamua hata kutenga muda wao kufunga na kuomba kwa ajili ya shida yake, wengine wanampa maneno ya faraja ya kimaandiko, wanakuwa karibu naye kila siku, wengine wanaguswa wanamsaidia katika mahitaji machache ya mwilini kama kuna ulazima, na mwisho wa siku Yule mtu uponyaji wake unamfikia kwa haraka zaidi kwasababu walikuwepo wengine kuuchukua mzigo pamoja naye..

 Hivyo ni lazima tujue kuwa kuna aina ya mahitaji ambayo mtu anaweza kukuombea bila hata ya kueleza siri ya moyo wako, lakini kuna mahitaji mengine kwa faida yako mwenyewe, unapaswa uwaambie ndugu wengine waaminifu, kumbuka pia sisemi kuwa kila jambo umweleze mtu, hapana, yapo mengine hayapaswi kuwekwa hadharani bali kwa watu uliowathibitisha kuwa ni waaminifu kwa Mungu. Kuna vitu vitu kama ukimwi, kesi za mauaji, n.k. hizo tafuta tu watumishi waaminifu wa Mungu, lakini vitu vingine kama magonjwa ya kawaida, ndoa, migongano, uzinzi n.k. Zungumza kwa ndugu wengine.

Lakini usikae na tatizo lako moyoni ikiwa unahitaji kweli kuombewa na wengine. 

Ubarikiwe.


Mada Nyinginezo:

KWANINI KUNA WATU WANAFANYIWA DELIVERANCE LAKINI BAADA YA MUDA WANARUDIWA TENA NA HALI ILE ILE?

MUNGU NDIYE ANAYEISHAWISHI MIOYO.

VIFUNGO VYA GIZA VYA MILELE.

KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?

UAMSHO MKUU UMEKARIBIA!!

WAISRAELI WENGI SANA WANARUDI KWAO SASA.


 

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/02/je-tunaruhusiwa-kumuombea-mtu-ambaye-haweki-bayana-kile-anachohitaji-kuombewa/