by Admin | 2 September 2019 08:46 pm09
JIBU: Biblia haijatueleza muda Ayubu aliokaa katika majaribu, Lakini tukisoma baadhi ya vipengele inatupa picha kukisia muda aliodumu, kwa mfano tukisoma ile sura ya Ayubu 7:2-6 Ayubu anasema..
“2 Kama mtumishi atamaniye sana kile kivuli, Kama mwajiriwa anayetazamia mshahara wake;
3 Ni vivyo nami NIMEPEWA MIEZI YA UBATILI iwe fungu langu, NAMI NIMEANDIKIWA MASIKU YENYE KUCHOKESHA.
4 Hapo nilalapo chini, nasema, Nitaondoka lini? Lakini usiku huwa mrefu; Nami nimejawa na kujitupa huku na huku hata kupambazuke.
5 Mwili wangu unavikwa mabuu na madongoa ya udongo; Ngozi yangu hufumba, kisha ikatumbuka tena.
6 Siku zangu hupita upesi kuliko chombo cha kufumia, Nazo zapita pasipokuwa na matumaini.”
Unaona hapo Ayubu anajaribu kujifananisha na mtu aliyeajiriwa ambaye kwa uvumilivu mwingi anasubiri mshahara wake kila mwisho wa kipindi Fulani labda tuseme wiki, au mwezi au mwaka,.apate faraja ya taabu yake, vivyo hivyo Ayubu naye anaonyesha amekaa katika hali hiyo ya kusononeka na kutaabika kwa MIEZI na masiku mengi, kama ya mwajiriwa vile, akisubiria faraja yake kutoka kwa Mungu ni lini atamrehemu na kumtoa katika mateso yale na majonzi yale.. Tunaona hapo Ayubu katamka neno MIEZI na sio MWEZI, hiyo ikiwa na maana ni zaidi ya mmoja, inaweza ikawa ni miwili au mitatu, au mitano au 12, au 20, au 100 hatujui kwasababu biblia haijaeleza jambo lingine la ziada.
Halikadhalika Pia hatujui ni muda gani ilimchukua Ayubu kukaa na wale marafiki zake, ambao tunasoma pia waliwasili kwake na kukaa siku 7 bila kuzungumza naye chochote, hivyo tukijumulisha na siku ambazo ziliwagharimu kufika kwa Ayubu kutoka majumbani kwao baada ya kupata taarifa za msiba wake, pamoja na siku ambazo walikuwa wanazungumza naye.. tukijumuisha na wakati ambapo Mungu anamwagiza Ayubu awaombee rehema wale marafiki zake kwa kwenda kuchukua ng’ombe 7 na kondoo 7 kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, tunaweza kukisia ni muda unaoweza kuchukua zaidi ya mwezi.. Lakini pia hatujui, kipindi Mungu alichotumia kumrejeshea Ayubu vitu vyote na mali zote alizozipoteza, je ilikuwa ni mara moja au kidogo kidogo, kama ni kidogo kidogo basi ni muda mrefu ulipita, lakini tunachofahamu ni kuwa Mungu alimburudisha Ayubu mara mbili ya alivyokuwa navyo pale mwanzo. Lakini hiyo ilikuwa ni kwa kusubiri na kwa kustahilimili na kwa kuvumilia.
Yakobo 5.10 “Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu.
11Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”
Hivyo na sisi tunafundishwa tujifunze kuwa wavumilivu maadamu tunajiona bado tupo katika njia sahihi ya wokovu,hatuna budi kuwa hivyo kama Ayubu, tabu, shida, misiba, dhiki, mateso, kupungukiwa, n.k. visituzimishe roho tukamkufuru Mungu kama mke wa Ayubu, hata kama itachukua mwezi, au miezi, au miaka, au miongo, hilo lisituzuie kuangalia ahadi za Mungu, sisi tunachofahamu tu ni kuwa mwisho wa siku tutamwona Mungu jinsi alivyo mwingi wa rehema na huruma…kama alivyokuwa kwa Ayubu.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
HUDUMA YA (ELIFAZI, BILDADI, NA SOFARI).
MAJARIBU MATATU YA YESU KRISTO
AYUBU 28 : HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?
TUTAWEZAJE KUMZALIA MUNGU MATUNDA?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/02/shalom-mtumishi-naomba-kufahamu-ayubu-aliteseka-katika-majaribu-kwa-miaka-mingapi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.