KIELELEZO CHA MWANAMKE KATIKA NYUMBA.

by Admin | 7 October 2019 08:46 pm10

Wanawake wamepewa na Mungu huduma kubwa sana, na huduma yenyewe ni ULEZI, Mungu aliiweke huduma hii ya kipekee kabisa kwa wanawake kwasababu alijua ikitumiwa ipasavyo italeta faida kubwa sana katika ufalme wake kuliko huduma nyingine yoyote.. lakini cha kusikitisha ni kuwa jambo hilo halitambuliki katikati ya wanawake wengi, wanadhani kuwa kulea ni jambo jepesi lisilo na heshima, na hiyo imewafanya waichukie na kukimbilia kufanya huduma ambazo haziendani na maumbile yao.
 
Nataka nikuambie mwanamke anayetambua nafasi yake hapa duniani, shetani anamchukia zaidi ya kitu kingine chochote ulishawahi kukijua, Kama ukisoma vizuri kitabu cha Ufunuo sura ya 12 utaona pale kuna Ishara ilionekana mbinguni na ishara yenyewe ilikuwa ni ya mwanamke, na mwanamke huyo alikuwa ni mjamzito ambaye anakaribia kujifungua,..Na shetani (ambaye ndio lile joka), lilipojua kuwa yupo katika hali ile, lilisimama limeze kile kilichokuwa ndani ya lile tumbo, kwasababu lilijua vizuri kile mwanamke anachokwenda kukileta kitamletea madhara makubwa kiasi gani huko mbeleni, lakini liliposhindwa basi likasimama pale ili lifanya vita naye, likawa linamuudhi sana mwanamke Yule likawa linafanya visa vya kila namna limuangamize yule mwanamke kisa tu kamzaa Yule mtoto…Lakini ukiendelea kusoma utaona baadaye lilikuja kushindwa, na liliposhindwa biblia inatuambia LILIMKASIRIKIA mwanamke Yule…
 
Ufunuo 12:17 “Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari.”
 
Unaona hapo lilimkasirikia, Halikuwa na haja ya uzao wake, bali lilipambana na yule mwanamke kwasababu lilijua Yule ndio chanzo uzao huo ambao utakuja kumsumbua.
 
Sasa Habari hiyo sio tu inafunua juu ya kanisa la Israeli katika siku za mwisho, lakini pia inatuonyesha picha ya mwanamke halisi na uzazi wake, mfano wa kilichotokea wakati wa Bwana wetu Yesu Kristo kuzaliwa na Mariamu..Shetani alijaribu kumwaangamiza mtoto Yesu na familia nzima mpaka Mungu akawaambia wakimbilie Misri,..
 
Embu fikiria uzao wa Mariamu, mwanamke mwenye hekima ameleta ukombozi mkubwa kiasi gani leo hii duniani, Na hiyo yote ni kwanini? Ni kwasababu alitambua huduma aliyopewa ndani yake na hivyo akaitendea kazi ipasavyo kama wanawake wengine waliomcha Mungu..Mariamu kwanza alikuwa ni bikira hapo kabla hakuwahi kukaribiwa na mwanamume pili alikuwa ni mwanamke mwenye heshima, aliyemcha Mungu..
 
Hivyo Mungu kwa neema zake akamfanya kuwa kituo cha kupitisha majeshi yake ya wokovu..Tukimwangalia tena mwanamke kama Hana vivyo hivyo alisimama katika nafasi yake ya kulea vizuri akamleta Samweli ambaye sio tu alikuwa mwamuzi wa Israeli wakati ule lakini hadi leo tunasoma habari zake na zinatujenga kiimani..
Na leo tutawaangalia wanawake wawili kwenye biblia pengine hukuwahi kuwafahamu, mmoja ni aliitwa LOISI, Huyu Loisi alikuwa ni mwanamke aliyedumu katika imani kweli kweli aliyeilelea familia yake katika misingi yote ya Imani ya Kikristo, mwanamke huyu Paulo alimjua kwa uthabiti wa imani yake…
 
Mpaka alipofikia hatua ya kuzaa, akazaa mtoto wa kike ambaye aliitwa EUNIKE, huyu alifundishwa na mama yake misingi ya imani hivyo mpaka alipokuwa akairithi, Imani isiyokuwa na unafki, naye huyu Eunike akazaa mtoto mwanamume, akamrithisha IMANI ile ile iliyokuwa ndani yake na ndani ya mama yake, akamlea akakua na mtoto huyo ndiye aliyeitwa TIMOTHEO tunayemsoma leo kwenye Biblia…
 
Tunafahamu kuwa Timotheo ndiye aliyekuwa mwangalizi wa makanisa yote yaliyokuwa Asia baada ya Paulo kuondoka kwake..
 
Tukisoma katika ule wakara wa pili ambapo Paulo anamwandikia Timotheo alimwambia maneno haya:
 
Timotheo 1:4 “Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha;
5 nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo.”
 
Unaona Bibi aliilea familia yake vizuri, lakini matokeo yanakuja kuonekana kwa wajukuu zake.. Sasa thawabu za wanawake hawa ni kubwa sana mbinguni, hawa ndio Mbinguni watakaokwenda kuketi kama mamalkia waliowazaa majemedari wa wokovu…
 
Na wewe mwanamke, ambaye unayofamilia au unatazamia kuwa na familia, maisha yako unayoishi sasa, jinsi unavyojiweka sasa, ni wazi yanaeleza uzao wako utakuja kuwa wa namna gani huko mbeleni.. Ikiwa wewe wakati wote huna habari na Mungu, unachofahamu ni kuvaa vimini tu, na kukatisha barabarani, na kwenda saluni, na kutembea nusu uchi barabarani,na kuketi vibarazani kuoshwa miguu na wanaume usitazamie kuwa utamletea Mungu matunda yoyote katika ufalme wake kupitia uzazi aliokupa,..Mungu alitazamia kwa uzao wako wainuke akina Samweli, lakini wewe unavyojiweka uzao wako unawanyanyua akina Baraba Yule mwizi na muuaji..Usifikiri kwa kinywa tu ndio unaweza kuulaani uzao wako, kwamba utajizuia usiwanenee vibaya..hapana ndugu! Matendo yako ndio yanayowanenea vibaya wanao..
 
Ukisoma tena utaona licha tu ya Mitume kuwaandika waraka wanaume, utaona pia waliwaandika na wanawake ukisoma kitabu cha Waraka wa pili wa Yohana utaona mtume Yohana anamwandikia mwanamke mmoja, ambaye alimwona analea watoto wake vizuri ambao ndio hao baadaye wanaenda kuwa wakina Timotheo, hivyo akawa anamtia moyo na kumpa maonyo ajiepushe na baadhi wa watu ambao ni wapinga Kristo majoka wanaotaka kuwaangusha wasisimame katika Imani..
 
2Yohana 1:4 “Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba.
5 Na sasa mama, nakuomba, si kwamba nakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo, kwamba tupendane.
 
Mpaka hapo naamini utakuwa umeona ni jinsi gani huduma ya ulevi wa mwanamke ilivyo na nguvu sana katika ufalme wa mbinguni..
 
Na Ndio maana maandiko yanasema:
 
Mithali 14:1 “Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.”
 
Kumbuka nyuma inayozungumziwa hapo sio tu nyuma hii ya mwilini bali pia makao yake huko atakapokwenda baada ya kifo.
Sasa ikiwa wewe hauwi kielelezo kwa mabinti zako, unavaa nguo mbaya mbele yao, wataacheje kukuiga na wewe, unasengenye mbele yao, wataachaje kukuiga… ikiwa wewe sio mwombaji, wataache na wao kuwa sio waombaji, ikiwa hulitafakari Neno la Mungu wataachaje na wao kuwa vivyo hivyo..ikiwa akili zako zimejaa miziki ya kihuni, na wewe huna hata muda wa kuwafundisha nyimbo za kumsifu Mungu unatazamia vipi Mungu atajitwalia watoto kutoka katika hao?
 
Mtu mmoja alisema.. “si kwamba Watoto wa siku hizi wamebadilika, la! Hapana Watoto wa siku hawajabadilika ni wazazi ndio waliobadilika, kwasababu Watoto ni wale wale, wanakaa tumboni miezi 9, wanazaliwa hawana meno, wala hawaongei…lakini wazazi ndio wanaowajaza vitu visivyo sawa, ndio maana tunawaona Watoto wapo hivyo walivyo leo”
Hiyo ni kweli kabisa! Kama mtoto ana mwaka mmoja tu! Tayari Umeshaanza kumsikilizisha midundo ya ulimwengu huu, na unafurahia anavyoserebuka! Ni nani kabadilika hapo?..ni mtoto au ni wewe? Sasa kwanini ulalamike anapokuwa mtu mzima na kuvaa herein au kawa shoga?
 
Kumbuka tena Leo upo hivyo kesho utakufa, unadhani huko unapokwenda utajivunia nani? Wakati wanawake wengine mashujaa ambao walijitunza na kulea familia zao katika imani kama Sara wanajivunia akina Isaka, na Mungu kuwapa nafasi karibu nao, wakati huo wewe hutakuwa na lolote,..
Huduma uliyopewa wewe ni kubwa, ithamini, shetani hapendi uitumie,..Anza sasa kuishi kama mwanamke wa Kikristo, jenga nyumba yako, ambao kwa hiyo ndiyo itakayokupa thawabu ukifika kule.
 
Na hata kama hujajaliwa kupata Watoto wa kimwili…Pia Maisha yako matakatifu yatawajenga Watoto wengine wasio na wazazi, na hata ambao wana wazazi, lakini wameshindwa kutimiza wajibu wao….na hivyo na wewe kuwa umefanya kazi sawa tu, au hata kubwa kuliko ya walio na Watoto. Na siku ile mbinguni ukaoneshwa jopo la wanao walio mashujaa ulio walea katika Kristo.
 
Ubarikiwe sana.

Mada Nyinginezo:

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA.

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

MWAMBA WETU.

JIFANYIE RAFIKI KWA MALI YA UDHALIMU.

UCHUNGU WA KUIBIWA.

ROHO MBAYA KUTOKA KWA BWANA.


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/07/kielelezo-cha-mwanamke-katika-nyumba/