UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?

by Admin | 14 October 2019 08:46 pm10

Upendo ni kitendo cha kuonyesha hisia za tofauti za ndani kwa mtu mwingine, Ni hisia zinazoonyesha pengine umeridhishwa na mtu huyo, au umemkubali, au umemuhurumia, au unataka kumkaribia uwe karibu naye n.k.

Kibiblia kuna upendo wa aina tatu:

UPENDO WA KWANZA NI UPENDO UNAOTOKANA NA HISIA:

Upendo huu unajulikana kama “EROS” Ni upendo unaozaliwa na hisia, Upendo huu ni maarufu sana kwa mke na mume, katika biblia Sulemani alijaribu kuuleza upendo ya namna hii:

Wimbo 1:13 “Mpendwa wangu ni kama mfuko wa manemane Ukilazwa usiku maziwani mwangu.

14 Mpendwa wangu ni kama kishada cha hina, Katika mizabibu huko Engedi.

15 Tazama, u mzuri, mpenzi wangu, U mzuri, macho yako ni kama ya hua.

16 Tazama, u mzuri, mpendwa wangu, Wapendeza, na kitanda chetu ni majani;

17 Nguzo za nyumba yetu ni mierezi, Na viguzo vyetu ni miberoshi”.

Huu ni Upendo ambao hauwezi kufananishwa na upendo kama wa mtu na ndugu yake au Rafiki yake.

AINA YA PILI YA UPENDO NI UPENDO UNAOZALIWA KWA VITU VINAVYOENDANA:

Unajulikana kama “PHILEO”. Upendo huu unazuka kutokana na mahusiano Fulani mtu mmoja alionao na mwenzake, anaweza akawa ni ndugu, au rafiki, au mchezaji mwenzake, au mfanyakazi mwenzake. Ni upendo ambao kusipokuwa na mahusiano Fulani ya karibu au faida Fulani ambayo mtu anaweza kuipata kwa mwenzake, hauwezi kuzaliwa.

Tunapaswa tupendane sisi kwa sisi, biblia inatuambia hivyo katika (1Yohana 2:9-10), vilevile inatuambia tupendane sisi tulio ndugu katika Bwana, lakini upendo wa namna hii haupo tu kwa waaminio bali hata kwa watu waovu pia wanao..Bwana Yesu alisema:

Mathayo 5:46 “Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

47 Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo”?

Unaona kwahiyo upendo huu bado hujafikia vile viwango vyenyewe.

AINA YA TATU YA UPENDO NI UPENDO USIO NA MASHARTI. UNAOJULIKANA KAMA “AGAPE” (UPENDO WA KI-MUNGU).

Huu ndio upendo Yesu Kristo aliokuwa anauzungumzia, ni upendo unaompenda mtu bila ya sababu yoyote, Ni upendo wa kiwango cha juu sana, unampenda mtu kwa kutokujali kama na yeye anakupenda au hakupendi, kama anakuchukia au hakuchukii, kama anakusema vibaya au hakusemi vibaya, kama anafaida yoyote kwako au hana faida yoyote kwako.

Upendo huu ndio YESU alikuwa nao kwetu, biblia pale inaposema “alitupenda Upeo”(Yohana 13:1),  ilimaanisha kusema hivyo Alitupenda upeo kweli kweli, sio kwasababu tulikuwa ni watakatifu, au kwasababu tulikuwa waovu…au kwasababu alikuwa anatafuta ukubwa kwetu hapana, alitupenda tu, tena ile wa kutoka moyoni hadi kufikia hatua ya kuutoa uhai wake kwa ajili yetu.

Na upendo wa aina hii ndio Bwana anataka kila mmoja wetu awe nao, Ni ngumu kuufikia, hususani pale tunapoona mtu Fulani anayetuchukia au anatuzungumzia vibaya halafu huyo huyo ndio tunapaswa tumpende, kuna kama ugumu fulani..Lakini Huo ndio Mungu anataka kuuona kwetu haijalishi tutawapenda wake zetu na waume zetu kiasi gani, au ndugu zetu wengi kiasi gani au rafiki zetu wengi kiasi gani kama hatujaweza bado kuufikia huu upendo wa AGAPE, mbele za Mungu bado hatuna upendo..

Hizi ndizo tabia za upendo wa AGAPE.

1Wakorintho 13:4 “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;

5 haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;

6 haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;

7 huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.

8 Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika”.

Hivyo ili mimi na wewe tuweze kuufikia Upendo wa namna hii hatupaswi kuungojea kama hizo aina mbili juu, bali tunapaswa tuupapalilie kwa kuvumilia, kwa kutokurudisha baya kwa baya, kwa kutokusengenya, kwa kutokuhesabu mabaya ya mtu tu sikuzote, kuwaelewa watu ..n.k.

Tuombe Mungu atusaidie sote tufike hapo, kwasababu hapo ndipo Mungu mwenyewe alipo, na hiyo ndio inayojulikana kama karama iliyo kuu kuliko zote. Ukiwa nayo hiyo wewe ni zaidi ya nabii yoyote, au mwalimu yoyote, au mwinjilisti yoyote, au mtume yoyote duniani. Mungu anakuwa karibu sana na wewe.

Ubarikiwe sana.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

JIRANI YAKO NI NANI?

SAMEHE KUTOKA NDANI YA MOYO WAKO.

MPENDEZE MUNGU ZAIDI.

JE! UNAYO NAFASI MBINGUNI?

HERI, WALE MUNGU ASIOWAHESABIA MAKOSA YAO.


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/14/upendo-ni-nini-na-je-kuna-aina-ngapi-za-upendo/