SIKU ZA MWISHO ZA UHAI WANGU.

by Admin | 15 October 2019 08:46 pm10

Kila mwanadamu atafikia ukomo wa siku zake, (yaani siku ya Mauti yake)..Lakini kabla ya siku yenyewe ya kuondoka ulimwenguni haijafika…Kinakuwepo kipindi fulani kifupi ambacho kinaweza kuwa ni miaka 10, au 5 kabla ya kuondoka kwako, au kinaweza kuwa mwaka mmoja au mwezi mmoja au wiki moja….Kipindi hicho kifupi ndicho kinachojilikana kama SIKU ZA MWISHO ZA UHAI WA MTU. 

Katika kipindi hicho, Kuna hali fulani mtu anakuwa anaanza kuipitia, mara nyingi inakuwa ni kumbukumbu ya mambo yaliyopita nyuma, ndio utakuta mtu anaanza kukumbuka mambo yake yote ya nyuma aliyoyapitia na jinsi alivyoyaishi, kipindi hichi sio kipindi kizuri kwa Mtu ambaye hakuwa ndani ya Kristo, kwasababu ni kipindi cha mashaka mazito, mara nyingi kwa mtu ambaye hajampa Kristo maisha yake huko nyuma, ni ngumu sana kushinda hali atakayopitia wakati wa hiki kipindi. Wengi wanaishia kujiua.

Ndio maana Biblia ikasema katika Mhubiri.

Mhubiri 12:1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo”

Umeona hapo? biblia haisemi mkumbuke muumba wako wakati wa siku zilizo mbaya..Hapana! bali inasema mkumbuke muumba wako siku za ujana wako, kabla hazijakaribia siku zilizo mbaya…Siku zilizo mbaya zinazozungumziwa hapo ndio hizi SIKU ZA MWISHO ZA UHAI WAKO.

Siku hizo ni ngumu kumrudia Muumba wako, kama katika siku za ujana wako ulikuwa unaichezea Neema, na kumbuka pia siku za ujana sio tu siku za miaka ya ujana kama vile miaka 15-45 hapana..bali siku za ujana ni siku ambazo ulikuwa unauwezo wa kumgeukia Mungu, na mazingira yote yalikuwa yanakuhimiza kufanya hivyo lakini  hukutaka!

Hivyo huu sio wakati wa kuzunguka huko na huko mitandaoni na mitaani kutafuta mambo ya ulimwengu huu yanayopita, huu ni wakati wa kutafuta wokovu kwa nguvu zote. Biblia inasema Ufalme wa Mbinguni unapatikana kwa nguvu na wenye nguvu ndio wauteka..Je! wewe nguvu zako unazipeleka wapi sasa katika ujana wako? katika ulimwengu au kwa Yesu?..Kama ni katika ulimwengu basi tambua kuwa SIKU ZA KUFA KWAKO ZINAKARIBIA na katika siku hizo, hazitakuwa siku za furaha bali huzuni.

Daudi aliziona siku zake na alikuwa na furaha..akafurahi akamwusia mwanawe kuzifuata njia za Bwana.

1Wafalme 2:1 “Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema,

2 Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume;

3 uyashike mausia ya Bwana, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako;”

Yakobo naye aliziona siku za kufariki kwake akafurahi, akawabariki wanawe…

Na siku hizo zinakuja kwako mimi na wewe! Umejiandaaje?..je zitakuja na huzuni au furaha kwako?

Tubu mgeukie Kristo sasa, angali mlango wa Neema bado upo..Angali u kijana.Na Kristo atakupa tumaini la maisha ya sasa, na yale yajayo!

Bwana akubariki.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

HUDUMA YA MALAIKA WATAKATIFU.

SIKU ZA MAPATILIZO.

WEWE NI HEKALU LA MUNGU.

JE! BAADA YA ULIMWENGU HUU KUISHA MALAIKA WATAKUWA NA KAZI GANI TENA?

JE! KUNA UBAYA WOWOTE KUWAOMBEA NDUGU ZETU WALIOKUFA KATIKA DHAMBI, MUNGU AWAKUMBUKE KATIKA UFALME WA MBINGUNI?


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/15/siku-za-mwisho-za-uhai-wangu/