USIPOLITENDEA KAZI NENO LA MUNGU.

by Admin | 30 October 2019 08:46 pm10

Luka 12:47b“………Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na Zaidi”.

Kila siku tunapolisikia Neno la Mungu tujue kabisa tunajiongezea deni mbele zake, kama vile biblia inavyosema Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu (Waebrania 4:12), inamaanisha kuwa pindi tu Neno la Mungu linapoingia ndani yetu linatazamiwa litoe matunda ya uhai, yaani lionyeshe mabadiliko ndani ya mtu, na pili watu wengine wabadilishwe kupitie Neno hilo hilo lililoingia ndani yetu.

Sasa kama inatokea leo hii tunalisikia Neno la Mungu, kisha hatulitendei kazi, tunasikia tu au tunasoma tu kama habari fulani ya kusisimua, tukitoka hapo, tunafikiria mambo mengine, tunaendelea na shughuli zetu kama kawaida, Kesho tena tunasoma vile vile kama habari fulani iliyojiri mpya, kisha baada ya hapo tunaendelea kuwa kama tulivyokuwa, Kesho kutwa nayo vivyo hivyo, tunasoma tunaondoka, siku zinakwenda, miezi inakwenda, miaka inakwenda, ukiangalia jumla ya mahubiri au mafundisho uliyosoma au kuyasikia hayahesabiki, na bado hakuna badiliko lolote ndani yako, leo hii tunaangalia kichwa cha somo ni kipi, tunasoma, tunapita, tunachukulia ni kawaida tu, tukidhani Mungu naye anachukulia hivyo kama sisi…..Ndugu Mungu anahesabu kila Neno lake linaloingia katika masikio yetu, kwasababu yeye mwenyewe anasema hakuna Neno lake linalokwenda bure bure (Isaya 55:11), ni lazima limrudishie majibu, na majibu hayo yatamrudia siku ile tutakaposimama katika kiti cha hukumu.

Biblia inasema kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na Zaidi…

Mungu anatazamia hicho unachokisikia na mwingine akisikie kupitia wewe kwa ile karama Mungu aliyoiweka ndani yako, lakini unakihifadhi tu, ni sawa na mtu anayetupa chakula wakati wengine wanakufa na njaa, ni sawa na kufuru, hujui kuwa mahali fulani kuna mama ambaye ni mwabudu sanamu, na anafanya vile kwa kutokujua laiti angefahamu ukweli huo kutoka kwako angebadilika na kuwa shujaa wa Bwana, lakini kwa kuwa hana wa kumwelezea habari hizo anakufa katika sanamu na kwenda kuzimu..

Mahali fulani yupo kijana ambaye anadhani kwa kushika dini yake fulani tu ndio tiketi ya kwenda mbinguni, lakini hajui kuwa hata pamoja na dini yake aliyonayo anaweza kwenda kuzimu kwasababu njia pekee ya kufika mbinguni ni kwa YESU tu, lakini kwasababu hakuna wa kumuhubiria yeye anaendelea kujitahidi na dini yake na mwisho wa siku anakufa na kwenda kuzimu na mtu wa kumweleza ulikuwepo..

Sehemu nyingine mtu fulani amekata tamaa ya Maisha, pengine kwa magonjwa anataka kujinyonga, anasema hakuna tumaini tena la kuishi, lakini hajui kuwa tumaini pekee lipo kwa YESU kwake huyo hakuna mzigo wowote usiotua, lakini anaenda kuishia kujinyonga kwasababu hakukuwa mtu wa kumsaidia…Vivyo hivyo wapo wengi wanateswa katika hali nyingi kama hizo na shetani..ambao wanahitaji maneno machache tu yahusuyo habari za YESU, ili wabadilike, lakini sisi ambao tumeshiba tukiachilia mbali ya kuwahubiria na wengine, sisi wenyewe hatulitendei kazi hilo tunalolisikia kila siku..

Hebu leo mwambie mtu amhubirie mwingine anayepotea kuhusu habari za Yesu, utasikia anakwambia hana karama ya kuhubiri au hana karama ya kichungaji, lakini hebu aone mtoto wake anazama kwenye matumizi ya madawa ya kulevya uone kama hatamhubiria kila siku kwa masaa mengi kwa uchungu na kwa kuhuzunika..

Siku ile tutaficha wapi nyuso zetu..wakati wale wengine ambao wamekuwa waaminifu wanapoambiwa Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako.(Mathayo 25:21)

Sisi tutaambiwa..

Mathayo 25:26 “Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;

27 basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.

28 Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.

29 Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.

30 Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.

Tunapaswa tusilizoelee Neno la Mungu,..Pale tunapolisikia tulitendee kazi, kwasababu utafika wakati ambao Bwana akitazama na asipoona matunda yoyote, basi tutakatwa na tukishakatwa ndio milele hivyo hakuna tumaini tena baada ya hapo…

Ndio maana biblia inatuambia..utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.

Wafilipi 2:13 “………utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.

13 Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.”

Kila siku tunapaswa tujitathimini, na tupige hatua moja mbele..

Maran Atha!.

Bwana akubariki sana.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali aua Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba 

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

KITABU CHA UZIMA

https://wingulamashahidi.org/2018/07/04/5-swali-je-kuna-dhambi-kubwa-na-ndogo-na-kama-hakuna-je-mtu-aliyeua-na-aliyetukana-je-watapata-adhabu-sawa/

Je! ni sahihi kwa Mkristo kusherekea siku yake ya kuzaliwa.[Birth day]?

YONA: Mlango 1

KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/30/usipolitendea-kazi-neno-la-mungu/