by Admin | 31 October 2019 08:46 pm10
Huu ni mfululizo wa maswali machache yamhusuyo Bwana Yesu, ambayo yamekuwa yakiulizwa na watu wengi hususani wale wasio Wakristo, ambao hawamjui Bwana Yesu kwa mapana, na Baadhi ya maswali hayo ni pamoja na 1)Bwana Yesu alizaliwa wapi? 2) Bwana Yesu alizaliwa mwaka gani? 3) Bwana Yesu alikuwa dini gani 4) Yesu alizikwa wapi? 5) Je Yesu aliteswa msalabani au juu ya mti ? n.k
Maswali yote na mengine mengi tutayapata majibu yake hapa, hivyo karibu!
Tukianza na swali la kwanza linalouliza
Swali la Yesu alizaliwa wapi..Jibu lake lipo wazi katika Biblia kwamba alizaliwa huko Bethlehemu ya Uyahudi…Bethlehemu ulikuwa ni mji aliozaliwa Mfalme Daudi, uliokuwepo maili chache sana kutoka mji wa Yerusalemu…Hivyo Kutokana na Daudi kuupendeza sana moyo wa Mungu, Mungu aliubariki mji wake aliozaliwa na kuufanya kuwa mji atakaokuja kuzaliwa Masihi yaani Yesu Kristo.
Mathayo 2:1 ‘Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu’
Sasa ingawa Bwana Yesu alizaliwa Bethlehemu lakini maisha yake yote hakuishi huko Bethlehemu bali aliishi mji mwingine uliokuwepo mbali sana unaoitwa Nazareti, hivyo alijulikana sana kama Yesu Mnazareti kuliko Mbethlehemu.
Biblia haijaeleza Bwana Yesu alizaliwa mwaka gani, lakini tukisoma hiyo Mathayo 2:1 hapo juu inasema…Yesu alizaliwa zamani za Mfalme Herode..Hivyo inaaminika na wanathelojia wengi kuwa Kristo alizaliwa kati ya mwaka 4-6 KK. Lakini katika Kalenda yetu tunafahamu kuwa umeshapita zaidi ya Miaka elfu 2 tangu Kristo awepo duniani…Hivyo ni kusema kwamba Kristo alizaliwa miaka 2019 iliyopita, kama leo hii ni mwaka 2019..
Ahadi ya kuzaliwa Mwokozi walipewa wayahudi (yaani Waisraeli) Lakini ahadi hiyo haikuishia kuwa Baraka kwa Waisraeli tu peke yao, bali kwa watu wote hata wa Mataifa kwasababu maandiko yanasema..Mataifa yote ulimwenguni yatamtumainia, na yeye atakuwa wokovu kwa mataifa yote…Lakini sharti kwanza Wokovu huo uanze kwa Wayahudi ambao ndio walioahidiwa kwanza na kisha uje kwa watu wa mataifa mengine.
Hivyo wayahudi walikuwa na Dini yao ya kiyahudi ambayo ndio ile waliyopewa na Musa, ya kushika sheria na Torati..Lakini Ahadi ya ujio wa Masihi ni kurekebisha pale palipopunguka..Hivyo alipozaliwa alizaliwa katika dini ya kiyahudi, lakini kwa uweza wa Roho aliitimiliza torati pale palipopunguka na pale palipoeleweka vibaya…Ndio maana akasema katika
Mathayo 5:17 ‘Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza’.
Hivyo dini ya kiyahudi Bwana Yesu alikuja kuitimiliza kwa kuwaambia amchukiaye ndugu yake ni sawa na muuaji, hivyo chuki haitakiwi kabisa, amtazamaye mwanamke kwa kumtamani tayari kashazini naye hivyo kutamani hakutakiwi kabisa licha tu ya kuua,..Hiyo ndiyo ilikuwa dini Bwana Yesu aliyokuwa nayo na ndio aliyokuwa anahubiri watu wawe nayo…Hakuhibiri Dini ya kiyahudi kwamba watu wawe wayahudi au wajina fulani…Bali alihubiri watu wabadilike na kuwa wema, watakatifu wenye upendo n.k…hiyo ndio Dini ya Bwana Yesu..
Yakobo 1:26 ‘Mtu akidhani ya kuwa anayo dini, wala hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hali akijidanganya moyo wake, dini yake mtu huyo haifai.
27 Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa’.
Kwahiyo dini ni matendo sio Jina! au kikundi fulani cha waabudio fulani..
Bwana Yesu alizikwa wapi? Jibu: alizikwa Yerusalemu, mji uliokuwepo karibu sana na mji aliozaliwa Bethlehemu…soma Luka 13:33 na Mathayo 27:60
Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa Msalaba unatengenezwa kwa mti, hivyo mahali popote kwenye biblia panaposema Bwana aliangikwa juu ya mti kama kwenye Wagalatia 3:13, basi fahamu kuwa inazungumzia msalaba kwasababu msalaba unatengenezwa kwa mti. Na msalaba ulikuwa unatengenezwa kwa vipande viwili vilivyokatana kama alama ya kujumlisha…na sio kipande kimoja kilichosimama wima kama inavyoaminika na ‘mashahidi wa Yehova’
Utamaduni wa kuwatundika Watu msalabani haukuanzia kwa Bwana Yesu bali ulikuwepo kabla yake, kwamba wahalifu waliokosa sana walikuwa wanauawa kwa kutundikwa msalabani vile vile kama Bwana Yesu alivyotundikwa, ndio maana utaona siku ile aliposulibiwa kulikuwepo pia kuna wengine wawili waliosulibiwa pamoja naye..Kwahiyo Bwana Yesu aliteswa msalabani wenye mfano wa alama ya kujumlisha.
Kumbuka Bwana YESU alikufa kwaajili ya dhambi zako na zangu, alisulubiwa na kuteswa na alikufa na siku ya tatu akafufuka, naye hatakufa tena..sasa hivi tunavyozungumza yupo hai, na anakutazama wewe na mimi, ametuma Neno lake kutuponya..Hivyo kama hujampa maisha yako ni vyema ukafanya hivyo sasa kama unatamani kuishi milele..
Yeye atakupokea na kukusafisha dhambi zako zote bure! alisema
Mathayo 11:28 ‘Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;
30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi’.
Je mzigo wako ni mzito? unasubiri nini usiende kuutua kwa Yesu sasa?
Bwana akubariki.
Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba
+225693036618/ +225789001312
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
Je! ni sahihi kwa Mkristo kusherekea siku yake ya kuzaliwa.[Birth day]?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/10/31/maswali-kuhusu-bwana-yesu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.