SADAKA YA MALIMBUKO.

by Admin | 6 November 2019 08:46 am11

Malimbuko ni nini?

Malimbuko maana yake “kitu cha kwanza kuja au kuzaliwa au zao la kwanza”, kwa lugha ya kiingereza “first fruits”…Katika Biblia agano la kale mtoto wa kwanza wa kiume kuzaliwa alikuwa ni malimbuko. Na huyo ni lazima awe malimbuko kwa Bwana.

Mwanzo 49:3 “Reubeni, u mzaliwa wangu wa kwanza, Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu”.

Na sio tu watoto wa kwanza wa kiume, Bali hata wanyama wa kwanza na mazao ya kwanza ya nchi yote hayo yaliitwa malimbuko, na yalipaswa yatolewe pia kwa Bwana.

Mambo ya Walawi 23:9 “Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapokuwa mmekwisha ingia hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtakapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu;”

Bwana alituoa maagizo kwa wana wa Israeli wote kutoa malimbuko katika mazao yao, yaani kupeleka sehemu ya kwanza ya mavuno yao nyumbani kwa Mungu, kuonesha shukrani zao mbele za Mungu kwa kupewa mazao..

Kama Bwana asingewapa mvua basi wasingepata hata hicho kidogo, kwahiyo “walimrudishia Bwana sehemu ya kwanza kabisa ya mazao yao”, kuonesha kuwa Mungu ni wa Kwanza na mengine yatafuata.

JE SADAKA YA MALIMBUKO ILIKUWA NA BARAKA YOYOTE?

Jibu ni ndio! ilikuwa na Baraka nyingi, kwasababu siku zote kitu cha Kwanza kumtolea Mungu kina nguvu kuliko cha Pili. Nguo mpya ambayo haijavaliwa na mtu ina thamani zaidi, na heshima zaidi kuliko ile ya Mtumba.

Raisi wa kwanza wa nchi, huwa anayoheshima kubwa Zaidi kuliko maraisi wengine wanaofuata. Kadhalika sadaka ya kwanza kabisa inayofika mbele za Mungu ina nguvu kubwa zaidi kuliko zinazofuata..Na sadaka hiyo ni ya “malimbuko”.

Kadhalika sadaka ya malimbuko ndiyo inayobariki kazi yote inayofuata, mshahara wa malimbuko ndio unaobariki mishahara mingine yote inayofuata. Tutakuja kuona hapo chini kidogo, ni kwa namna gani Kristo aliitwa limbuko lao waliolala, ikasababisha baraka kwa wote watakaolala kama yeye.

JE NI LAZIMA KUTOA MALIMBUKO KATIKA AGANO JIPYA?

Jibu ni ndio! Kama tunalipa sadaka za Zaka, Malimbuko nayo ni lazima..Na baraka zake ni zile zile…Kwamba cha kwanza ni bora kuliko cha pili, haijalishi cha pili kitakuwa na wingi gani..lakini cha kwanza ni cha kwanza tu.

Na pia Roho Mtakatifu ndani yetu anatushuhudia, kwamba hiyo kazi kama Mungu asingeibariki basi tusingepata chochote, kwahiyo tunamheshimu Mungu na kumwonyesha kuwa yeye kwetu ni wa KWANZA kwa vitendo! kwahiyo tunampa Malimbuko yetu.

TUNATOAJE MALIMBUKO?

Kama umeajiriwa au umejiajiri, Mshahara wa Kwanza unaoupata unaupeleka kwa Bwana. Usiogope kupungukiwa, wala usiwaze waze utapata vipi fedha, yeye aliyekupa hiyo kazi anajua zaidi kuliko wewe, anasema maua haifanyi kazi na bado hayasokoti yanazidi kupendeza tu. kitu ambacho hata Sulemani katika fahari yake, hajawahi kuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo!. Kama Mungu anayavisha maua ya kondeni vizuri hivyo je si zaidi sisi?. (Mathayo 6:28)…hivyo usiangalie mazingira yanayokuzunguka mtolee Bwana sehemu ya kwanza.

Kadhalika Faida ya kwanza ya Biashara yoyote iliyo halali uliyojiajiri ni hivyo hivyo, sehemu ya kwanza ya mazao yako ya shambani, kama umevuna debe 10 mpelekee Bwana, mifugo yako imezaa wazaliwa wa kwanza mpelekee Bwana, au ibadilishe katika fedha, uipeleke nyumbani kwa Bwana.

Kumbuka kama umeshatoa mzaliwa wa kwanza wa mfugo wako, hao wengine hupaswi kutoa kama malimbuko. Hao utatoa tu kama sadaka na kwa jinsi Bwana atakavyokujalia. Na kwa jinsi utakavyopenda wewe kutoa, haina masharti!

Kumbuka pia kama umeacha kazi fulani na kwenda kuanza nyingine, ambayo inazalisha kwa namna nyingine, na ina mkataba mwingine wa kukuingizia kipato, hapo ni lazima utoe tena limbuko kwa hiyo kazi mpya ulioanza. Kwa ulinzi wa kazi yako.

YESU KRISTO LIMBUKO LAO WALIOLALA.

Mtu wa Kwanza kufufuliwa alikuwa ni Kristo! Lazaro alifufuliwa lakini alikufa tena…Hivyo ufufuo wake haukuwa na nguvu ya umilele, lakini Yesu alifufuliwa na hawezi kufa tena yupo mpaka leo, kwahiyo yeye ndiye mzaliwa wa kwanza wa walio kufa, (LIMBUKO).

Na kutokana na Mungu kumtoa kaburini na kumleta juu kama Limbuko, amesababisha hata sisi tuliomwamini tutakaofuata kufa kama yeye, nasi pia tupate hiyo ofa ya bure ya kufufuliwa katika siku ile! haleluya!

Hivyo kama sio Mungu kumtoa Yesu kuwa limbuko, baraka ya kufufuliwa sisi wengine tusingekuwa nayo.

1Wakorintho 15:20 “Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.

21 Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu.

22 Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.

23 Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja”.

Na pia inasema..

Wakolosai 1:18 “Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote”.

Hiyo ndiyo faida ya “kutoa sadaka ya malimbuko”, Inakuwa inabariki mazao mengine yaliyosalia..Kama Bwana Yesu alivyotubariki sisi tutakaokufa katika yeye. Tunalotumaini la ufufuo, kwasababu yeye amefanyika kuwa mtangulizi wetu, Na wewe unalo tumaini la kufufuliwa kazi yako upya, au biashara yako, au kilimo chako endapo kitasuasua kama ulitoa limbuko(kama sadaka ya utangulizi)! siku ile ulipoianza hiyo kazi,

Lakini pamoja na hayo yote! haitakufaidia chochote, kama utatoa sadaka ya malimbuko na huku maisha yako yapo nje ya wokovu, huku bado ni mlevi, bado ni msengenyaji, bado ni mtukanaji, bado ni mfanyaji masturbation, na bado kahaba, bado mla rushwa..Mungu wetu hafanyi kazi ya ukusanyaji mapato kwetu,…Kwamba uwe mwovu au usiwe mwovu kodi ni lazima ulipe!.

Hapana Mungu wetu hayupo hivyo, yeye hakusanyi mapato kutoka kwetu kama wafanyavyo TRA kwasababu yeye ana kila kitu tayari, anataka tu! tujifunze kutoa kwa faida yetu wenyewe, kama yeye alivyo mtoaji, na hapendezwi na sadaka ya mtu mwovu, hivyo kama unatoa sadaka na bado mlevi, au kahaba..ni afadhali usitoe kabisa kwasababu ni machukizo mbele za Mungu. Hakuchukii wewe, bali unachotoa kinamchukiza, na anataka tufanye kilicho bora.

Biblia inasema

Kumbukumbu 23:18 “Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili”.

Hivyo kama hujampa Kristo maisha yako umechelewa sana, ni afadhali ufanye hivyo sasa kabla mlango wa Neema haujafungwa, unachotakiwa kufanya ni kutubu kwa kukusudia kuacha kufanya dhambi tena!!, Unaamua kwa vitendo! kuacha ulevi, anasa, uvaaji mbaya, rushwa, na mambo yote machafu kisha unaenda kubatizwa tena! kwasababu kama ulibatizwa na umerudia machafu ya ulimwengu huu, kiasi hata cha kufanya uzinzi na uasherati unapaswa ukabatizwe tena katika maji tele, na kwa jina la Yesu kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako kulingana na Matendo 2:38,

kisha baada ya kufanya hivyo Roho Mtakatatifu ataingia ndani yako, na kukupa uwezo wa kushinda dhambi kwa namna ya kipekee.

Baada ya kufanya hivyo, utakuwa umeokoka na kufanyika kuwa mwana wa Mungu, hivyo tafuta kusanyiko la kikristo linalomhubiri Kristo, na maneno yake ya kwenye biblia yenye vitabu 66 na sio vitabu 666, ujiunge hapo!, ili usizimike kiroho. Na Bwana mwenyewe atakusaidia kufanya yaliyosalia, kwasababu Neno lake ni mwanga wa njia zetu.

Ubarikiwe. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

ROHO HUTUOMBEA KWA KUUGUA KUSIKOWEZA KUTAMKWA!

NILIMWONA SHETANI, AKIANGUKA KUTOKA MBINGUNI.

BARAGUMU NI NINI?

Je! ni vema kwa mkristo kwenda hospitali au kutumia miti shamba anapougua?

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/11/06/sadaka-ya-malimbuko/