NENO LA MUNGU NI TAA

by Admin | 11 November 2019 08:46 pm11

Biblia inasema katika Zaburi 119:105  “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.” Hivyo Neno la Mungu ni Taa!

Maisha ya Mtu aliyeokoka yanafananishwa na Mtu asafiriye (Waebrania 11:13 na 1Petro 2:11). Na safari mtu aliyeokoka asafiriyo ni safari ya USIKU na si Mchana.

Kama unavyojua safari za Usiku zinakuwa na hatari nyingi,

Hatari ya Kwanza: ni kukutana na wanyama wakali: Wanyama wote wararuao na wadhuruo huwa wanatembea Usiku, wanyama kama chui, simba, fisi, mbweha pamoja na nyoka huwa wanatafuta mara nyingi mawindo yao wakati wa Usiku.

Na viumbe vyote vinavyotembea usiku vinafunua viumbe vya rohoni vilivyo viovu ambayo ni mapepo..Ndio maana wanaojihusisha na uchawi wanatumia viumbe kama popo, bundi, fisi, chui, nyoka na viumbe vyote vinavyotembea gizani kufanya shughuli zao.

Hatari ya Pili:  Ya kusafiri usiku ni kupata ajali.

Wakati wa Usiku ni rahisi kupungukiwa umakini kutokana na Usingizi, au giza. Siku zote giza linaleta usingizi, wanaosafiri na magari usiku ni rahisi kupata ajali kuliko wanaosafiri mchana.

Hivyo ili kuzuia hatari zote hizi Msafiri asafiriye usiku anahitaji kuiongeza  umakini sana anapotembea usiku na pia anahitaji TAA ITAKAYOMWONGOZA NJIA YAKE. Hakuna  namna yoyote anaweza kukwepa matumizi ya Taa. Awe anatembea kwa miguu au kwa Gari, Taa  ni Lazima.

Na sisi wakristo tupo safarini. Dunia ndio NJIA yetu. Na dunia yote sasa ni giza Kutokana na matendo ya giza yanayoendelea ulimwenguni kote. Uzinzi ni matendo ya giza, ulevi ni matendo ya giza. Kadhalika uchawi, rushwa, utoaji mimba, ulawiti, uvutaji sigara. Mauaji, usagaji na uchafu wa kila aina..Mambo hayo yanakoleza giza lililopo ulimwenguni.

Na sisi hatuna budi kupita katikati ya hilo giza ili tutokezee ng’ambo ya pili, hakuna kuingia mbinguni pasipo kupitia duniani!.  Kwasababu hiyo basi tunahitaji Mwanga katika hili giza Nene!. Na Mwanga si kingine bali ni NENO LA MUNGU, Lililovuviwa na Roho Mtakatifu.

Neno la Mungu linaposema Usizini, ni kwa faida yetu! Neno hilo ni mwanga wa njia zetu, maana yake tukizini tumeizimisha taa. Na hivyo ni rahisi kupotea. Na kushambuliwa na wanyama wakali. Kadhalika na maneno mengine yote ambayo Biblia imekataza kama rushwa, usengenyaji, chuki, wivu, hasira, faraka, uchungu, wizi, uuaji, ulevi n.k hayo yote ni matendo yanayozima taa zetu na hivyo kutuweka hatarini katika safari yetu.

Neno la Mungu linazidi kutuambia katika

Zaburi 119:9 “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako”.

Hivyo ukitaka kuisafisha njia yako!. Utaisafisha tu kwa kulitii na kulifuata Neno la Mungu ambalo hilo ndilo Taa yetu.

Kumbuka Bwana Yesu anakuja, na wala hatakawia. Hivyo kama hujaoshwa dhambi zako kimbilia Kalvari haraka kabla mlango wa Neema haujafungwa. Na Bwana atakuokoa.

Bwana akubariki. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

BARAGUMU NI NINI?

USIPOLITENDEA KAZI NENO LA MUNGU.

JE KUJIUA NI DHAMBI?

Wakatoliki wanaabudu sanamu?

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/11/11/neno-la-mungu-ni-taa/