KUOTA UNAKULA CHAKULA.

by Admin | 14 December 2019 08:46 pm12

Kuota unakula chakula maana yake ni nini?


Ninakusalimu katika jina la YESU KRISTO.

Awali ya yote nitoe tahadhari, kuwa kuna wimbi kubwa la mafundisho mengi ya uongo kuhusu ndoto. Hivyo ukikosa uelewa wa tafsiri sahihi  kulingana na Mungu anavyozungumzia katika Neno lake..Utajikuta unapoteza kabisa dira ya Maisha yako ya rohoni kiujumla..na kujikuta unaacha kumtazama Mungu na Neno lake na unatazama ndoto unazoziota kila siku.

Kwa ufupi ndoto zimegawanyika katika makundi makuu matatu:

Kundi la Kwanza ni ndoto zinazotokana na Mungu:

Hizi zikija huwa zinakuja na ujumbe Fulani, au onyo Fulani, au tahadhari Fulani,  wala hazikufanya utamani kufanya mabaya, bali zinakufanya ujirekebishe pale ulipokuwa unakosea, , au ukaze mwendo katika safari yako ya kumtafuta Mungu, au kukuhimiza ukatende tendo la haki n.k.

Mfano wa ndoto za namna hii tunaweza kuiona kwa mke wa Pilato. Alipotaka kumzuia mumewe asimlibishe Bwana Yesu,..

Mathayo 27:19  “Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake.

Na hizi huwa haziji mara kwa mara kama zile ndoto zinazotana na mtu mwenyewe”.

Kundi la Pili ni ndoto zinazotokana na shetani:

Hizi huwa zinaambatana na vitisho, au tamaa za kutenda dhambi, au mambo maovu, au hofu..Kwamfano utakuta mtu anaota akifanya uzinzi na watu asiowajua au anaowajua, au anaota anafanya matambiko, au anacheza ngoma za kimila n.k. Zote hizo ni ndoto za kutoka kwa yule adui, Na hivyo mtu anaswa azikemee. Au arekebishe mwenendo wake, ni hiyo inakuja kwa kumpa Kristo Maisha yake.

Lakini kundi la tatu na la muhimu ambalo, watu wengi wanapaswa kufahamu ni kuhusu ndoto zinazotokana na mtu mwenyewe au mawazo yake mwenyewe

Hapa ndipo asilimia kubwa za ndoto za watu zinapoegemea..

Ndoto za namna hii, kimsingi hazipaswi kuchukuliwa kiuzito kama hizo ndoto za aina mbili tulizozizungumzia hapo juu, kwani hizi zinatengenezwa na ubongo wa mtu tu pale anapokuwa amelala.. hivyo ubongo unatengeneza ndoto kutoka katika kumbukumbuku za matukio yote aliyoyafanya siku za nyuma, au siku za hivi karibuni..

Ndio hapo utakuta mtu labda jana ameona ajali mbaya imetokea, leo usiku akaota ajali nyingi zinatokea tokea..Au jana alikuwa msibani usiku wa leo anaota ndoto ya mtu Fulani kafa na yeye yupo kwenye mazishi..Au jana alikuwa anacheza mpira, leo hii anajiona yupo uwanjani anafunga magoli mengi..Au Maisha yake yote ni ya udereva, usiku anajiona anaendasha magari mengi tofauti tofauti..n.k.

Sasa ndoto za dizaini hii, huwa hazitokani na Mungu au shetani, kwahiyo zinapokujia unachopaswa ni kuzielewa kwanza, kisha kuachana nazo usihangaike hata kutafuta maana zake, kwasababu hazina maana yoyote rohoni..

Andiko lake ni hili:

Mhubiri 5:3 “Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi.”

Vilevile aina nyingine ya ndoto zinatokana na ubongo wa mtu, ni ndoto za kula..biblia inasema.

Isaya 29:8 “Tena itakuwa kama mtu mwenye njaa aotapo, kumbe, anakula; lakini aamkapo, nafsi yake haina kitu; na kama mtu mwenye kiu aotapo, kumbe, anakunywa; lakini aamkapo, kumbe, anazimia, na nafsi yake inatamani…”

Unaona, kama ulilala jana na njaa ni jambo la kawaida kuota unakula usiku. Mfano kuota unakula nyama, au kuota unakula wali, au kuota unakula  samaki..au kuota unakula  matunda,.. au kuota unakula karanga,..  au kuota unakula keki,.. au kuota unakula  mayai..au kuota unakula hushibi n.k. zote hizo Ukiangalia kwa makini  utagundua kuwa pengine jana usiku ulilala na njaa..Au siku za hizi karibuni ulikuwa unakula aina hiyo ya chakula.

Hivyo ndoto kama hizo zikikujia zipuuzie tu, Endelea na Maisha yako ya kawaida, Jikite Zaidi katika kulitafakari Neno la Mungu kwasababu hilo ndilo linaloweza kukutabiria Maisha yako ya mbeleni ipasavyo.

Ndoto na Maono hazinusi hata chembe kwenye Neno la Mungu, Mungu anazifananisha na kama makapi katika Neno lake..soma

Yeremia 23:28 “Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana. 

29 Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?”

Hivyo penda kujifunza  Neno la Mungu Zaidi ya kujifunza tafsiri za ndoto, Na Mungu atakuwa na wewe.

Ikiwa hujaokoka, Mlango wa neema bado upo wazi kwako, japo hautakuwa hivyo daima. Tubu dhambi zako angali muda unao, ukumbuke kuwa tunaishi katika dakika za nyiongeza tu, Kristo yupo mlangoni kurudi kulichukua kanisa lake. Dalili zote zinaonyesha, pengine kizazi chetu hichi kitashuhudia tukio zima la unyakuo wa kanisa.

Hivyo unasubiri nini. Mgeukie Kristo.Naye atakupokea.

Ubarikiwe.

Group la whatsappjiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

FAHAMU TAFSIRI ZA NDOTO MBALIMBALI.

KUOTA NYOKA.

NENO LA MUNGU NI UFUNUO MKAMILIFU.

Ijumaa kuu ni nini? Na kwanini iitwe kuu?

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/12/14/kuota-unakula-chakula/